Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe amesema kuondoka kambini kwa kiungo mkongwe Shaban Kisiga hakuwaumizi kichwa.
Shaban Kisiga aliripotiwa wiki iliyopita kutoweka kambini kutokana na kuchoshwa na benchi la benchi la ufundi la Simba SC linaloongozwa na Mserbia Goran Kopunovic na msaidizi wake, Seleman Matola.
Katika mahoajino na mtandao huu muda mfupi uliopita, Hanspope amesema: "Kisiga hatuumizi kichwa, tunajua tabia zake."
"Tulimwacha miaka kadhaa iliyopita kutokana na tabia zake hizo hizo, amekuja tena Simba baada ya baadhi ya watu ndani ya klabu kumpigia debe lakini ninaona ameanza tena.
"Sisi (Simba SC) hatudai, lakini anajiona yeye ni 'super star' (nyota wa matawi ya juu), kwa nini hachezi? Kuondoka kambini bila taarifa maana yake amejondoa mwenyewe. Tutampa barua na kuachana naye," amesema zaidi Hanspope.
Kisiga amekuwa akisotea namba katika kikosi cha kwanza cha Simba, hali inayomfanya akose amani kiasi cha kufikia hatua ya kukiuka miiko ya maadili ya klabu.
Oktoba 26 mwaka jana aliunganishwa na kiungo mwingine mkongwe Amri Kiemba na winga Haroun Chanongo katika kundi l;a 'watovu wa nidhamu wa Simba SC' na kuamuliwa kurudi Dar es Salaam mara moja kutoka Mbeya baada ya timu yao kutoka sare ya 1-1 na Tanzania Prisons.
Kisiga kwa sasa ana mabao mawili katika Ligi Kuu ya Bara msimu huu sawa na Aggrey Morris wa Azam FC, Amisi Tambwe wa Yanga, Deus Kaseke wa Mbeya City, Ibrahim Hassan wa Tanzania Prisons, Jabir Aziz wa JKT Ruvu Stars, Jacob Masawe wa Ndanda FC, Mussa Mgosi wa Mtibwa Sugar, Najim Magulu wa JKT Ruvu Stars na Nicholas Kabipe wa Polisi Moro.
0 comments:
Post a Comment