Na Bakana, Dar es salaam
MLINDA mlango wa zamani wa klabu ya Dar es salaam Young Africans (Yanga SC) ambaye kwa sasa anakipiga ligi kuu nchini Oman (Omantell Professional League) ndani ya Al Seeb Club, Juma Mpongo huenda akalamba shavu la kusakata kabumbu ligi kuu India.
Akizungumza akiwa Oman, Mpongo ambaye amewahi kuzichezea timu za Tanzania Prisons, Twiga sports, Coastal Union na Ashanti United amesema kuwa mchakato wa kutimkia India upo kwenye njia na hiyo imekuja baada ya kuwepo na fununu za kutaka kuzuia magolikipa kutoka nje ya Oman kucheza ligi za nchi hiyo.
“Kwa kiasi fulani naweza sema ndoto zangu zimetimia, lakini bado nina ndoto ya kupata changamoto nyingine, Pia bado napambana ili niende mbele zaidi kadiri Mungu atakavyo niwezesha".
"Kama mipango inaenda vizuri naweza kuhamia ligi kuu ya India, Mipango inaendelea kaka, bado sijaambiwa ni timu gani kwa sasa, Hapa inawezekana sheria zikabadilika baada ya msimu huu kumalizika, Kuna tetesi msimu ujao wanaweza kufuta kuingiza Magolikipa kutoka nje ya nchi hii” Amesema Juma Mpongo ambaye timu yake ya mwisho kuichezea Tanzania ni Ashanti United iliposhuka daraja mwaka jana.
Mpongo ambaye pia amewahi kucheza soka la kulipwa nchini Congo kunako klabu ya DC Virunga, na Rwanda katika timu za Kiyovu sports na Rayon sports, amezungumzia kwa ujumla Maisha ya mpira Oman na tofauti iliyopo kati ya Soka la Tanzania na kwa waarabu hao ambapo ametiririka kama hivi.
“Maisha ya huku sio mepesi sana kama ambavyo tunafikiria japo ugumu upo tena mkubwa tu. Tofauti kwenye soka sio kubwa Sana, Lakini huku wenzetu kila kitu wanacho pia kuna mashindano Mengi ambayo yanamfanya mchezaji awe bize muda wote, Ligi inaushindani Mkubwa sana, huwezi amini kaka, sisi tumecheza mechi 6 ndani ya siku 11 mashindano tofauti” Amesema Mpongo ambaye timu yake ya Al Seeb inashika nafasi ya 10 katika msimamo wa ligi ikiwa na pointi 13 huku kinara wa ligi hiyo akiwa na alama 32.
Alituaje Oman?
Kipa huyo ambaye ni mzaliwa wa Nzega mkoani Tabora, ametoboa siri ya kupata nafasi ya kukipiga Oman na kusema kuwa, mlinda mlango wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Peter Manyika ambaye ndio mwalimu wake aliyekuwa akimnoa katika kituo chake cha makipa kilichopo Karume Jijini Dar es salaam, baada ya kuridhishwa na kiwango chake akaamua kumpatia ulaji huo na kuwaacha wakongwe kama Juma Kaseja akibakia Tanzania.
“Kwa kweli nafasi hii nilipewa na aliyekuwa kocha wa Makipa wa Timu hii msimu uliopita, Coach Peter Manyika, Aliona uwezo wangu kwani nilikuwa nafanya mazoezi katika kituo anachokiendesha hapo Dar uwanja wa Karume ndipo akavutiwa na mimi, Ni kweli tulikuwa wote pale kituoni mimi, Kaseja na wengineo na wao bado wanaendelea” Amesema Juma Mpongo ambaye unaweza kumuita Baba Halidi.
Kuhusu familia yake, Je, anaishi nayo Oman?
Mlinda mlango huyo namba moja wa klabu ya Al Seeb, amesema kuwa licha ya kuwa na majukumu ya kuhakikisha analinda lango la timu yake isivamiwe na wapinzani, lakini bado ana majukumu ya kulea familia yake ya Watoto watatu, pamoja na mke mmoja, licha ya kuwa mbali nao akimaanisha kuwa Familia yake ipo Dar es salaam.
“Familia yangu ipo Dar es salaam kaka, Namshukuru Mungu Nina Watoto watatu wote wakiume, Wa kwanza anaitwa Halidi Juma Mpongo huyu ana umri wa Miaka 10 sasa, Wa pili anaitwa Mohamed Juma Mpongo ana umri wa miaka 7 sasa na Wa tatu ambaye Ndio mdogo anaitwa Rahim Juma Mpongo ana umri wa Miaka 5, Wote wa napenda Sana soka ila huyu mdogo yeye huwa anataka hadi gloves zangu nimpe” Amefunguka Juma Mpongo.
Kuna Watanzania wengine wanao cheza Oman?
“Kwenye ligi kuu ni Mimi peke yangu ila madaraja ya chini yupo Thomas Moris ila sijajua anacheza Timu gani na daraja gani kwani Timu yao ipo nje kabisa ya Muscat” Amesema Baba Halidi.
Ushauri wake kwa wachezaji na TFF
“Cha msingi ni kujituma na kufanya kazi kwa bidii kwa Magolikipa mwenzangu, pia TFF na wadau wote wa soka tupambane ili kuinua soka la nchi yetu maana bado tuko chini, na ligi yetu iendeshwe kwa misingi ya haki zaidi ili bingwa anayepatikana aweze kutuwakilisha vizuri kimataifa, TFF iandae mashindano mengine ili wachezaji wasiwe wanakaa muda mrefu bila kucheza, kuwepo na vikombe, kwa mfano hapa Oman, kuna kumbe linaitwa Mazda cup Hili limeandaliwa kwa ajili ya kufanya wachezaji wasikae muda mrefu bila kucheza pindi Timu ya taifa inapokuwa na majukumu ya Kimataifa, Hayo Ndio maono yangu kaka” Amefunga kazi mtu mzima Baba Rahim.
0 comments:
Post a Comment