![]() |
Ibrahim Hajibu |
Na Baraka Mbolembole, Dar es Salaam,
Simba SC wametuma salamu kwa mahasimu wao Yanga SC baada ya
ushindi ‘ mkubwa’ zaidi katika msimu dhidi ya Tanzania Prisons ya Mbeya jioni
hii katika uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mshambulizi kinda, Ibrahimu Hajibu alifunga mara tatu ‘ hat-trick’ na
kuisaidia timu yake kuibuka na ushindi wa mabao 5-0.
Hajibu alifunga bao la kwanza akiwa ndani ya eneo la hatari katika dakika
ya 16 akimalizia pasi ya Danny Sserunkuma ambaye alimpiga chenga mlinzi Nurdin
Chona na kumpasia mfungaji. Dakika tano baadaye mshambulizi huyo chipukizi
alifunga goli la pili akimalizia mpira uliotemwa na mlinda mlango, Yussuph
Mohammed ambaye alishindwa kuumiliki ‘ kiki kali’ iliyopigwa na Emmanuel Okwi.
Mlinzi, Lugano Mwagama aliunawa mpira ndani ya eneo la hatari na kijana huyo
kutoka Simba B, akafunga ‘ hat-trick’ yake ya kwanza katika ligi kuu dakika nne
kabla ya kumalizika kwa kipindi cha kwanza.
Simba ilikwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 3-0, ni mara
ya kwanza kwa timu hiyo kufunga idadi kubwa ya mabao katika nusu ya kwanza ya
mchezo tangu walipofanya hivyo dhidi ya Yanga, Oktoba, 2013 katika mchezo ambao
ulimalizika kwa sare ya 3-3. Jonas Mkude na Said Ndemla walitawala katika eneo
la kiungo kati mwa uwanja, huku Okwi na Ramadhani Singano wakiwapa wakati mgumu
walinzi wa pembeni wa Prisons, Laurian Mfalile na James Mwasote.
Kiujumla, Simba ilicheza kwa kujiamini huku wakipasiana pasi
za uhakika. Okwi alifunga bao la sita katika ligi kuu msimu huu baada ya
kufunga bao kali akiwa nje ya eneo la hatari kwa shuti la ufundi katika dakika
ya 75 na kuandikia Simba bao la nne, kisha Singano akafunga bao la mwisho na la
tano kwa timu yake zikiwa zimesalia dakika sita mchezo kumalizika akimalizia
pasi ya mlinzi wa kushoto, Mohammed Hussein ‘ Tshabalala’. Ushindi huo ni kama
‘ onyo’ kwa mahasimu wao Yanga ambao watakutana siku ya Jumamosi ijayo.
Kitendo cha kufunga mabao matano ni kama kimewasaulisha
wapenzi wa timu hiyo ‘ mwendo usioridhisha’ msimu huu, hata kama Prisons si
timu bora sana ni wazi sasa wapenzi, wachezaji, benchi la ufundi na uongozi
watakuwa na furaha na sasa wataenda kucheza na mahasimu wao wakiwa na hali
kubwa. Yanga ndiyo viongozi wa ligi kuu hadi sasa wakiwa na alama 21, nane
zaidi ya Simba walio katika nafasi ya nne na alama zao 23 katika michezo 16.
Nahodha wa zamani wa timu hiyo, Joseph Owino alicheza kwa
mara ya kwanza baada ya miezi miwili na mlinzi huyo wa kati aliweza kuongoza
vizuri ngome, alikuwa kiongozi halisi na mara zote alionekana akimkumbusha
nahodha wake kijana Hassan Isihaka. Simba ilichea vizuri katika safu ya ulinzi,
safu ya kiungo na ile ya mashambulizi ambayo mkufunzi, Goran Kopunovic aliamua
kuwaanzisha Danny na Hajibu.
0 comments:
Post a Comment