MWANASOKA bora wa dunia, Cristiano Ronaldo amekuwa miongoni mwa wafungaji watatu bora katika historia ya Real Madrid baada ya kufunga goli lake la 290 mwishoni wa wiki tangu atue klabuni hapo mwaka 2009 kwa ada ya paundi milioni 80 akitokea Manchester United.
Ronaldo alifunga goli hilo katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Elche huku goli lingine la matajiri hao likifungwa na karim Benzema katika mchezo huo uliopigwa Estadio Manuel Martinez Varelo jana.
Mshindi huyo wa Ballon D'or mara tatu sasa ameifikia rekodi ya gwiji wa klabu hiyo Carlos Santillana ambaye alifunga magoli 290 katika mechi 645 alizoichezea Real Madrid lakini Ronaldo ametumia mechi 281 kufunga magoli hayo.
Aidha Ronaldo amebakisha magoli 17 kumfikia Alfredo Di Stephano anayeshika nafasi ya pili lakini pia amebakisha magoli 33 kumfikia Raul Gonzalez ambaye yupo kileleni katika orodha hiyo ya wafungaji katika klabu hiyo akiwa na magoli 323 katika mechi 741 alizoichezea Real Madrid.
Ushindi huo wa jana unaifanya Real Madrid kuwa juu ya msimamo wa ligi hiyo kwa tofauti ya pointi 4 na Barcelona ambao walichezea kichapo kutoka kwa Malaga katika mechi iliyopigwa juzi katika uwanja wao wa nyumbani Camp Nou.
0 comments:
Post a Comment