Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
Subira ya muda mrefu sasa imekatwa gembe; televisheni ya kulipia ya Tanzania, Azam TV imenunua rasmi haki za matangazo ya televisheni ya Ligi Kuu ya Uganda (UPL).
Katika mkutano maalum na waandishi wa habari leo Jumatatu asubuhi kwenye Ukumbi wa Nile Hall, Serena jijini Kampala, Uganda, Azam TV imetangazwa rasmi kuwa mdhamini wa ligi hiyo miaka ijayo.
Ofisa Mtendaji Mkuu CEO wa kampuni ya Azam Media, Rhys Torrington amepongeza ushirikiano uliooneshwa na Shirikisho la Soka la Uganda (FUFA), klabu na pande zote zilizofaniklisha Azam TV kukubaliwa kudhamini ligi hiyo.
“Hii ni siku muhimu kwa soka la Uganda. Tumejitoa kusaidia maeendeleo ya soka la nchi hii. Tuko hapa kufanya kazi," Torrington amesisitiza.
Torrington alikabidhi hundi ya dola za Marekani ($) 1.9M (Ush. 5.4 Billion) kwa Rais wa FUFA, Moses Magogo kwa ajili ya timu zote 16 za UPL.
MILANGO IKO WAZI KWA LIGI NYINGINE
Torrington amesema Azam TV iko tayari kudhamini ligi nyingine za Uganda zikiwamo Kombe la FA la Uganda na Ligi Kubwa ya Fufa (FUFA Big League).
Imeelezwa pia na baadhi ya mitandao ya Uganda ya michezo leo kuwa Azam TV imewekeza $4M ndani ya nchi hiyo kuonesha michezo mbalimbali Uganda na kutoa ajira zaidi ya 30 kwa Waganda katika kipindi cha udhamini wake.
Mechi ya kwanza kuoneshwa moja kwa moja na Azam TV nchini Uganda itakuwa Februari 17, 2015 ya mabingwa mara 16, Sports Club Villa iliyomkuza Emmanuel Okwi wa Simba SC dhidi ya Sadolin Paints kwenye Uwanja wa Nakivubo.
Azam TV pia wamenunua haki za matangazo ya televisheni ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) kwa misimu mitatu kwa thamani ya Sh. bilioni 5.5.
0 comments:
Post a Comment