Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
MABINGWA watetezi wa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Azam FC kinaondoka jijini hapa leo kuelekea mjini Khartoum, Sudan kwa ajili ya mechi yao ya marudiano na hatua ya awali ya Ligi ya Klabu Bingwa Afrika dhidi ya wenyeji wao El Merrikh FC.
Mechi hiyo ya marudiano itapigwa Jumamosi usiku Uwanja wa Khartoum mjini humo.
Ofisa Habari wa Azam FC, Jaffar Idd Maganga, amesema jijini hapa jana kuwa kikosi hicho kitahusisha nyota wote waliosajiliwa.
Mchezo huo unatarajiwa kufanyika kuanzia saa mbili usiku kwa saa za Afrika Mashariki.
Azam FC ilishinda 2-0 katika mechi yao ya kwanza Uwanja wa Azam wiki juzi kupitia magoli ya Mrundi Didier Kavumbagu na John Bocco 'Adebayor' na inahitaji kuepuka kipigo cha goli zaidi ya moja kusonga mbele katika raundi ya kwanza michuano hiyo mikubwa zaidi ya ngazi ya klabu barani Afrika.
YANGA SC KESHO
Yanga SC itakwea pipa kesho Jumatano kuelekea Botswana kuivaa BDF XI ya huko katika mechi yao ya marudiano ya hatua ya awali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Katika mechi yao ya awali iliyofanyika Uwanja wa Taifa jijini hapa, Yanga SC ilishinda kwa mabao 2-0 yaliyofungwa kwa kichwa na mshambuliaji Mrundi Amisi Tambwe.
Yanga inahitaji kuepuka kipigo cha goli zaidi ya moja ili kuingia raundi ya kwanza ya michuano hiyo na itapambana dhidi ya mshindi kati ya Sofapaka FC ya Kenya na Platnumz ya Zimbabwe.
Platnumz ilishinda 2-1 dhidi ya Sofapaka FC katika mechi yao ya kwanza iliyochezwa nchini Kenya.
0 comments:
Post a Comment