Licha ya kushindwa kuibuka na ushindi katika mchezo ata mmoja kwenye michuano mifupi iliyoandaliwa na Tp Mazembe nchini Drc Congo,
mabingwa watetezi wa ligi kuu Tanzania Bara Azam FC, wamesema kuwa ziara hiyo
ilikuwa na mafanikio katika maandalizi yao ya mechi ya awali ya ligi ya
mabingwa barani Afrika dhidi ya vigogo wa Sudan, El-Merreikh.
Msemaji wa Azam, Jaffar Idd ameiambia Mpenja Blog kuwa wamepata mazoezi ya kutosha licha ya kutoshinda.
“Tumejua
makosa yetu na udhaifu wetu, kocha tayari amerekebisha na tupo tayari
na mechi yetu dhidi ya El-Merreikh”, alisema Iddi.
Azam imerejea
Dar es Salaam usiku wa kuamkia Jana(Alhamisi) ikitoka Lubumbashi na baada ya kurudi
wanajiandaa na mechi kadhaa za ligi kuu ya Tanzania kama maandalizi yake
ya mwisho kabla kuwavaa Wasudan.
Wakiwa Congo, walicheza na mabingwa mara nne wa ligi ya mabingwa Afrika, klabu ya TP Mazembe na kufungwa 1-0.
Pia walitoka droo ya 2-2 na timu ya Zesco na kufungwa 1-0 na Don Bosco katika mechi yao ya mwisho.
Iddi alisema wana matumaini makubwa ya kuanza vyema michuano ya kimataifa baada kuyafanyia kazi mambo kadhaa.
Hii
ni mara ya kwanza kwa Azam kushiriki michuano hii ya ligi ya mabingwa
Afrika na itacheza na El Merreikh ya Sudan Februari 15 jijini Dar es
Salaam. Mechi ya marudiano itachezwa Khartoum, Sudan baada ya wiki
mbili.
Wawakilishi wengine wa Tanzania Bara ni Yanga ikipangiwa
kuanza na Botswana Defence Force (BDF) ya Botswana katika Kombe la
Shirikisho.
Kwa upande wa Tanzania Visiwani, Polisi ya Zanzibar
itacheza na CF Mounana ya Gabon katika Kombe la Shirikisho huku KMKM
ikipangiwa kucheza na Al Hilal ya Sudan katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
0 comments:
Post a Comment