Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
Yanga SC imeachana na mpango wake wa kuweka kambi ughaibuni kabla ya kuivaa BDF XI ya Botswana katika hatua ya awali ya michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika mwezi ujao, imefahamika.
Januari 3, Yanga SC kupitia kwa Katibu Mkuu, Jonas Tiboroha ilisema imepata mualiko wa kwenda Zambia kushiriki michuano maalum nchini humo itakayohusisha timu nyingine kutoka Msumbiji, Rwanda, Afrika Kusini, Malawi na timu mwenyeji Zesco. Michuano hiyo imepangwa kuanza Januari 28 hadi Februari 4 mwaka huu.
Hata hivyo, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga SC, Jerry Muro amesema leo Dar es Salaam kuwa uongozi uliokutana jijini jana, uliamua timu yao icheze mechi zote za mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) kabla ya kuikabili BDF XI.
"Uongozi ulikutana jana na kuamua tucheze mechi zote zilizopo kwenye ratiba ya Ligi Kuu kabla ya kukaribia kwa tarehe ya kuanza kwa michuano ya kimataifa.
"Kwa maana hiyo tutacheza mechi zinazofuata dhidi ya Polisi Morogoro (Jumamosi), Coastal Union (Feb 4), Ndanda FC (Feb 11) na Mtibwa Sugar (Feb 8). Baada ya hapo tutahamia kwenye michuano ya kimataifa," amesema Muro na kuongeza kuwa kikosi chao kitatinga Morogoro keshokutwa kikitokea kambini Bagamoyo, Pwani.
Mechi ya Yanga dhidi ya Mtibwa Sugar itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa Februari 8 ni ya mzunguko wa pili wa VPL. Wanajangwani watamenyana na BDF XI kwenye Uwanja wa Taifa Februari 14 na itakuwa na mechi moja ya kiporo ya mzunguko wa kwanza wa VPL dhidi ya Mbeya City itakayochezwa kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine mjini Mbeya Februari 21.
0 comments:
Post a Comment