Na Bertha Lumala, Dar esc Salaam
Uongozi wa Yanga SC umesema kikosi chake kitaweka kambi maalum kwa michuano ya kimataifa kisiwani Pemba na kitacheza mechi moja ya kirafiki dhidi ya Vipers ya Ligi Kuu ya Uganda kabla ya kumenyana dhidi ya BDF XI katika hatua ya awali ya Kombe la Shirikisho barani Afrika mwezi ujao.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga SC, Jerry Muro amesema jijini hapa leo kuwa kikosi chao kitaweka kambini kisiwani Pemba kujiandaa kwa mechi za mbili za hatua ya awali ya michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika dhidi ya BDF XI.
Amesema wametuma maombi kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) mechi yao ya Februari 8 dhidi ya Mtribwa Sugar ipigwe kalenda ili wapate muda wa kutosha wa kukaa visiwani Zanzibar kujiandaa kwa michuano ya kimataifa.
Yanga SC itacheza mechi yake ya kwanza dhidi ya timu hiyo ya Jeshi la Ulinzi la Botswana Febuari 14 kwenye Uwanja wa Taifa jijini na kurudiana mjini Gaborone wiki mbili baadaye.
Muro amesema wanatarajia kucheza mechi ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya Vipers (zamani Bunamwaya) ya Ligi Kuu ya Uganda kabla ya kuivaa BDF XI.
Amesema mechi hiyo inatarajiwa kuchezwa Uganda na kama timu hiyo ikija Tanzania, mechi hiyo itachezwa Uwanja wa Amaan, Unguja visiwani Zanzibar ambako kambi yao itawekwa.
Awali Yanga SC iliripotiwa kuwa inataraji kuweka kambi maalum Afrika Kusini, Namibia na Zambia kabla ya kuwavaa maafande hao.
0 comments:
Post a Comment