Kocha wa Mbeya City fc, Juma Mwambusi ambaye ni kocha bora wa Msimu uliopita
KUNA msemo maarufu uliotumika sana mwaka jana
usemao: “Jiamini, jitathimi na jiongeze” .
Kujiamini kwa kila jambo unalofanya ni silaha ya
mafanikio, lakini lazima uwe unajitathimini kila baada ya muda ili kuona
umefanikiwa kiasi gani na umekwama wapi, halafu unajiongeza kwa kutafuta njia
mbadala na kuongeza juhudi zaidi ili kufikia malengo yako.
Mbeya City walianza ligi vibaya msimu huu tofauti
na msimu wa mwaka jana. Kumbukumbu zinaonesha mechi ya kwanza iliyopigwa
septemba 20 mwaka jana walitoka suluhu (0-0) dhidi ya Maafande wa JKT Ruvu
katika uwanja wa Sokoine Mbeya.
Mechi ya pili waliifunga Coastal Union bao 1-0.
Bao hilo la penalti lilifungwa na Deogratius Julius. Kipute hicho kilipigwa
uwanja wa Sokoine septemba 27 mwaka huu.
Baada ya mechi hiyo Wagonga Nyundo hao wa Mbeya
wakasafiri kwenda Matabini Mlandizi, Pwani ambapo walitoka suluhu (0-0) na
wenyeji wao Ruvu Shootings.
Suluhu mbili na ushindi katika mechi tatu za
kwanza hayakuwa matokea mabaya kimpira, lakini watu wengi wakaanza kuhoji
kiwango cha Mbeya City wakiamini kimeshuka kufananisha na msimu uliopita ambapo
walitikisa nchi kwa kandanda murua.
Balaa lilianza kuwaangukia ‘Wanyampara’ hao wa
Mbeya katika mechi ya nne ambapo walifungwa goli 1-0 na Azam fc katika uwanja
wao wa nyumbani, hii ilikuwa Oktoba 18 mwaka jana. Nakumbuka bao hilo
lilifungwa kwa mpira wa adhabu ndogo na nahodha msaidizi wa Wanalambalamba,
Aggrey Morris.
Kipigo hicho hakikuwashitua wengi kwasababu Azam
walikuwa na rekodi ya kupata matokeo uwanja wa Sokoine na moja ya chachu ya
ubingwa wao msimu uliopita ilikuwa ushindi wa 2-1 waliovuna dhidi ya City
katika uwanja huo.
Kufuatia kipigo hicho, minong’no ikaendelea na
Oktoba 26, Mbeya City ikafungwa mabao 2-0 na Mtibwa Sugar katika uwanja wa
Nyumbani.
Kipigo hicho kilizidi kutibua rekodi ya City ya
kubana katika uwanja wake. Kilikuwa kipigo cha tatu katika historia ya klabu
hiyo kwenye michuano ya ligi kuu.
Kikosi cha Mbeya City fc
Wakiwa katika maumivu hayo, City walisafiri kwenda
Tanga, Novemba 2 mwaka jana kucheza na Mgambo JKT ambapo walifungwa mabao 2-1.
Kutoka Tanga pengine wakadhani wataifunga Stand
United Oktoba 8 mwaka jana katika uwanja wa CCM Kambarage Shinyanga, lakini
wakaambulia kipigo cha bao 1-0.
City walimaliza raundi ya 7 ya ligi kuu wakiwa na pointi 5 katika nafasi ya
mwisho ya msimamo.
Matokeo haya yaliwaumiza viongozi, wachezaji na
mashabiki wa timu hiyo pendwa nchini.
Wakati wa mapumziko ya mwezi mmoja na zaidi
kulizuka taarifa za klabu hiyo kuachana na kocha Juma Mwambusi na yeye mwenyewe
alitangaza kujiuzulu kazi yake akidai amechoshwa na maneno ya watu kutokana na
matokeo mabaya.
Uongozi wa klabu ulikaa na kocha huyu bora wa
msimu uliopita na kumaliza tatizo na hatimaye akaendelea na kazi ya kusuka
kikosi chake.
Kama unajua mpira, tatizo kubwa la Mbeya City
lilikuwa katika safu ya ulinzi, ndani ya mechi saba iliruhusu nyavu zake
kuguswa mara 6. Safu ya kiungo na ushambuliaji pia haikuwa na makali.
Mwambusi aliongeza wachezaji kadhaa katika dirisha
dogo akiwemo beki kisiki Juma Said Nyosso.
Nyosso, beki wa zamani wa Simba, Coastal Union na
Taifa Stars siku zote anajua kazi yake na amekuwa mjanja sana anapokuwa
katika eneo la ulinzi.
Usajili huo umewafanya Mbeya City wacheze mechi
mbili za ligi bila kufungwa goli. Walishinda 1-0 dhidi ya Ndanda fc desemba 28
mwaka huu uwanja wa Sokoine na jana wameibuka na ushindi wa kwanza ugenini
msimu huu kwa kuifunga Kagera Sugar 1-0 uwanja wa CCM Kirumba.
Katika mechi hiyo niliangalia mambo mawili
makubwa, moja ni namna kocha Mwambusi alivyojenga upya kikosi chake kimbinu na
kiufundi pamoja na nidhamu ya mchezo kwa wachezaji.
Mashabiki wa Mbeya City fc kwenye moja ya mechi ya timu hiyo uwanja wa Sokoine Mbeya
Pili nilijikita zaidi kuona namna mashabiki
wanavyoiunga mkono timu yao.
Jambo la kwanza, niligundua Mbeya City
wamebadilika, wamekuwa kwenye kiwango kizuri. Walicheza vizuri safu ya kiungo
na ulinzi.
Mabeki wa pembeni John Kabanda (kulia) na Hassan
Mwasapili (kushoto) walikuwa wanakaba vizuri katika nafasi zao, walijitahidi
kupandisha timu na nidhamu yao ilikuwa juu. Walijua wakae wapi, wafanye nini
kuwazuia mawinga wa Kagera Sugar. Walifanikiwa kwa kiwango kikubwa na kuwafanya
Juma Nyosso na Yusuph Abdallah wawe na kazi rahisi katikati.
Nyosso na mwenzake hawakuwa na kazi kubwa ya
kwenda kuwasaidia mabeki wa pembeni, walikuwa na uhakika na Kabanda na
Mwasapili. Safu ya ulinzi ilicheza vizuri sana.
Pia akina Nyosso walikuwa bora kutokana na kiungo
wa ulinzi Steven Mazanda na mwenzake Rafael Daud kulimudu dimba la kati.
Viungo walicheza pasi rahisi, fupi na pasi ngumu
kuwafikia viungo washambuliaji ambao waliongozwa na Cosmas Fredy aliyecheza
nyuma ya Paul Nonga.
Them Felix aliyeanzia kulia, huku Deus Kaseke
akiwa kushoto walicheza vizuri na kufika mara nyingi eneo la mwisho la Kagera
Sugar na isingekuwa umakini wa mabeki wa wakata miwa hao,wangefungwa magoli
mengi.
Mbeya City fc walikuwa na kasi nzuri, walicheza
vizuri wanapomiliki mpira na cha kufurahisha zaidi walijitahidi kukaba vizuri
wanapopoteza mpira.
Jambo la pili nililoliona ni amsha amsha za
mashabiki kwa muda wote. Hawa ni mashabiki ninaowafahamu mimi. City
wamefanikiwa kuwa na mashabiki wa kweli.
Hawa watu wanaipenda sana timu yao, walikuwa zaidi
ya 200 uwanja wa CCM Kirumba. Lugha ya miili yao ilionesha wanaipenda timu yao
na hawaoni shida kupoteza pesa kusafiri kwenda popote pale nchini.
Unapocheza mpira halafu kuna watu wengi nyuma yako
wanakusapoti hata kama ulikuwa na matokeo mabaya nyuma, kunaongeza morali
kubwa.
Siku zote mashabiki ni mchezaji wa 12, mchezaji wa
uwanjani hana uwezo wa kuwalipa mshahara kwa kushangiliwa, fadhila pekee
wanazopokea ni wachezaji kuucheza mpira kwa kiwango cha juu.
Wachezaji wa Mbeya City, viongozi na benchi la
ufundi, jikumbusheni kuwa kuna watu wengi wapo nyuma yenu. Mna wajibu mkubwa wa
kuifanya timu iwe bora.
Kinachotakiwa kufanyika ni kuifanya timu iwe bora
muda wote ili kurudisha fadhila kwa mashabiki. Mpira una matokeo matatu,
kufunga, kufungwa na kutoa sare.
Matokeo yoyote yanayopatikana ni sawa katika
mpira, lakini linapokuja suala la kiwango cha timu lazima lionekane wakati
wote.
Sina shaka na uwezo wa kocha Mwambusi kimbinu na
kiufundi, lazima apewe sapoti kubwa ili kuendeleza mazuri aliyokuwa nayo.
Siku njema!
0 comments:
Post a Comment