Wednesday, January 28, 2015


WIKI iliyopita Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilitangaza kumfungia refa Mohamed Teofile kuchezesha mechi za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), ikiwa ni saa chache baada ya uongozi wa Yanga kulitaka lifanye hivyo.

Uamuzi huo ulithibitishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi ya TFF, Salum Chama akieleza kuwa wamefikia hatua hiyo kutokana na refa huyo kushindwa kuimudu mechi ya raundi ya 11 ya VPL iliyomalizika kwa Yanga kutoka suluhu dhidi ya Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Januari 18.

Kufungiwa kwa Teofile kumekuja ikiwa ni muda mfupi baada ya uongozi wa Yanga kupitia Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano, Jerry Muro kutoa tamko la kuitishia nyau TFF wakilishinikiza kuwafungia na kutowapanga tena katika mechi za kikosi cha Jangwani marefa waliochezesha mechi pamoja na kuanika hadharani ripoti ya kamisaa wa mechi hiyo.

Uongozi wa Wanajangwani pia ulitoa masharti mengine mawili kwa TFF; kuchukua hatua kali dhidi ya wachezaji wa Ruvu Shooting waliodaiwa kumbagua, kumtukana matusi na kumkaba koo mshambuliaji Amisi Tambwe wa Yanga na kuwaadhibu maofisa wa Ruvu Shooting, hasa kocha mkuu wa timu hiyo, Mkenya Tom Olaba kwa kauli zake za kuwasifu wachezaji wake kwa kuibana Yanga katika mechi hiyo.

Katika kinachoonekana kuwa ni muingiliano wa matukio, ripoti ya mechi ya Yanga dhidi ya Ruvu Shooting imefanyiwa kazi kwa muda mfupi na kutolewa maamuzi ilhali Kamati ya Waamuzi ya TFF ilikaa kupitia mechi 49 za raundi saba za mwanzo za msimu huu wa VPL baada ya kusimama kwa ligi hiyo Novemba 9, mwaka jana.

Je, Kamati ya Waamuzi ya TFF imefanya hivyo kwa faida ya nani? TFF imehofu tishio la Yanga kutopeleka timu uwanjani? Shirikisho hilo lenye mamlaka ya juu kisoka nchini linaendeshwa na Yanga? Majibu ya maswali haya si rahisi kuyapata kwa muda mfupi bila kufanya tafakuri ya kina na kuangalia rekodi za marefa wa Tanzania kutupwa jela ya soka na TFF.

Kumbukumbu zinaonesha kuwa sehemu kubwa ya marefa wa Ligi Kuu waliowahi kuadhibiwa na TFF walichezesha mechi zinazohusisha timu kongwe nchini, Simba na Yanga. Baadhi yao ni refa wa kati Mathew Akrama wa Mwanza (Yanga vs Simba 2012/13), refa msaidizi mwenye beji ya FIFA, Ferdinand Chacha (African Lyon vs Simba 2012/13), Ephrony Ndissa (Yanga vs Simba 2012/13), Ronald Swai (Yanga vs Mtibwa Sugar 2012/13) na Alex Mahagi (Simba vs JKT Ruvu 2012/13).

Mwamuzi Bora wa VPL msimu wa 2011/12, Martin Saanya wa Morogoro alifungiwa msimu mzima baada ya kutoa penalti kwa Coastal Union iliyozaa bao la kusawazisha katika mechi ya kwanza ya msimu uliopita wa ligi hiyo ya Yanga dhidi ya Wagosi wa Kaya iliyomalizika kwa sare ya bao moja kwenye Uwanja wa Taifa Agosti 24, 2013. Afande huyo (Saanya) aliokolewa na msamaha kwa wafungwa wa TFF uliotolewa ma Jamal Malinzi muda mfupi baada ya kushinda kiti cha Rais wa shirikisho hilo usiku wa kuamkia Oktoba 28, mwaka juzi.  

Wapo marefa wachache wa Ligi Kuu waliowahi kufungiwa kwa madai ya kuchezesha chini ya kiwango mechi zisizohusisha vikosi vya Simba na Yanga. Waamuzi hao ni pamoja na Methusela Musebula (Toto Africans vs Coastal Union), Lingstone Lwiza (Toto Africans vs Coastal Union), Idd Mikongoti (Toto Africans vs Mtibwa Sugar) na Samson Kobe (Toto Africans vs Mtibwa Sugar), wote msimu wa 2012/13 pamoja na refa wa kati Othman Kazi wa Dar es Salaam aliyefungiwa mwaka maisha (baadaye kupunguziwa adhabu hadi miezi mitatu) klwa tuhuma za rushwa katika mechi ya Ligi Kuu (Majimaji dhidi ya Mtibwa 2008/9).  

Katika kile kinachoonekana kama TFF na kamati zake huwafungia marefa bila sababu kuntu, Akrama licha ya kuambiwa uwezo wake mdogo, alipangwa kwenye mechi nyingine ngumu iliyohusisha timu zenye uhasama mkubwa kwa sasa, Yanga dhidi ya Azam FC iliyomalizika kwa sare ya mabao mawili (2-2) kwenye Uwanja wa Taifa Desemba 28, mwaka jana.

Refa Israel Nkongo wa Dar es Salaam mwenye beji ya FIFA alishambuliwa na kupigwa na baadhi ya wachezaji wa Yanga wakati wa mechi yao ya VPL dhidi ya Azam FC kwenye Uwanja wa Taifa miaka mitatu iliyopita. Kwa nini TFF ikampanga Akrama (ambaye ilimuona hana kiwango kikubwa cha uchezeshaji) kuchezesha mechi kati ya timu hizo?

Aidha, Saanya aliyetupwa jela ya uamuzi kwa msimu mzima mwaka juzi, Alhamisi aliaminiwa na TFF na kupewa jukumu la kuchezesha mechi ya kimataifa ya kirafiki ya Taifa Stars Maboresho dhidi ya timu ya taifa ya Rwanda (Amavubi) iliyomalizika kwa sare ya bao moja kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.

Baada ya TFF kutangaza adhabu ya kumfungia Teofile, Msemaji wa Ruvu Shooting, Masau Bwire, alihoji kuhusu uhalali wa adhabu hiyo. Bwire alitaka kujua kama Teofile hajafikisha alama 6.5 kati ya 10 katika mechi yao iliyopita dhidi ya Yanga (kwa mujibu wa Kanuni za Ligi) ama ameadhibiwa ili kuuridhisha upande wa pili.

"Kama refa ameadhibiwa kwa kushindwa kupata alama zinazotakiwa, hakuna tatizo. Lakini kama uamuzi wa TFF umefanyika ili kuuridhisha upande wa pili kwa maana ya wenzetu klabu ya Yanga, ni janga kwa soka letu kwa sababu waamuzi watakuwa wakichezesha kwa hofu mechi zinazohusisha timu hii ambayo inaiitwa timu kubwa," anasema Bwire.

Pengine, Teofile hakuwa katika kiwango kizuri Jumamosi lakini sehemu kubwa ya makosa yaliyofanyika katika mechi hiyo, hasa vurugu za kukabana koo kwa Tambwe na beki kisiki George Michael wa Ruvu Shooting, yalifanyika pasi na mpira, hivyo yalipaswa kuonwa na wasaidizi wake Michael Mkongwa na Yusuph Sekile pamoja na Kenneth Mapunda aliyekuwa mezani.

Binafsi ninafikiri Teofile ameponzwa na wasaidizi wake katika mechi hiyo na ninaamini ndiyo waliopaswa kuwa namba moja kuchukuliwa hatua. Tutaendelea kupoteza waamuzi wazuri bila sababu za msingi hadi lini?" Teofile ni refa mwenye msimamo asiyeyumbishwa na ukubwa wa jina la timu.  

Oktoba 31, 2013 refa huyo kutoka Morogoro alifanya kile kilichofanywa na Saanya Agosti 24 mwaka juzi alipowapa tuta Kagera Sugar dhidi ya Simba dakika moja kabla ya kumalizika kwa mechi yao ya raundi ya kwanza ya VPL msimu wa 2013/14 ambayo matokeo yalikuwa sare ya bao moja huku kukitokea vurugu kubwa zilizosababisha kung'olewa kwa viti vya Uwanja wa Taifa na baadhi ya mashabiki wa Simba. Ni waamuzi wachache wenye utashi wa kutoa maamuzi hayo dakika ya mwisho ya mchezo.

Kwa mantiki hiyo, kauli ya Bwire ina mashiko kutokana na utata ulioibuliwa na Kamati ya Marefa ya TFF katika kumhukumu Teofile. Mechi iliyomtia hatiani ilichezwa Jumamosi na ripoti ya kamisaa na waamuzi inapaswa kuwasilishwa kwa Katibu Mkuu wa TFF ndani ya saa 24 baada ya mechi kumalizika, kwa mujibu wa Kanuni za Ligi za TFF toleo la 2014.

Kamati ya Chama ilikuwa na muda mwingi wa kupitia ripoti ya marefa na kamisaa wa mechi ya Yanga dhidi ya Ruvu Shooting kuanzia Jumapili na kutoa uamuzi mapema lakini uamuzi ulitoka Alhamisi na kuonekana kama kulikuwa na shinikizo kutokana na tamko la Yanga la Jumatano.

Katika hali kama hiyo, kunaibua maswali mengi na hisia kwamba huenda TFF inazibeba baadhi ya klabu, hivyo kuonekana kama shirikisho hilo linapanga matokeo. Ni kutokana na dhana hiyo, Bwire wa wadau wengine wa soka tunaingiwa na hofu kwamba huenda timu kama Yanga zikabebwa na marefa kwa hofu ya kufunguliwa mashtaka na kufungiwa pindi wanapochezesha mechi zinazokuwa na matokeo mabaya kwa timu hiyo ya Jangwani.

Makala haya yameandikwa na Sanula Athanas, Mwandishi Mwandamizi wa gazeti la NIPASHE.

CHANZO: NIPASHE la Jumatatu Januari 26, 2015

0 comments:

 
voyeur porn porn movies sex videos hd porno video