KAMA mikwara ya nje ya uwanja ni ubingwa, basi
Simba ni bingwa wa Kombe la Mapinduzi hata kabla ya fainali ya leo Jumanne
usiku dhidi ya Mtibwa kwenye Uwanja wa Amaan hapa Unguja, Zanzibar.
Simba ambayo ina uzoefu na mechi zaidi za fainali
kuliko timu yoyote nchini, imebadilika ndani na nje ya uwanja baada ya kufuzu
hatua hiyo.
Tangu wikiendi iliyopita, viongozi wote wa juu wa
Simba pamoja na wajumbe wa kamati zake, wamehamia karibu na kambi ya timu yao
mjini hapa na kumekuwa na vikao vya mara kwa mara na wachezaji pamoja na kocha
katika kuhakikisha wanazima kiburi cha Mtibwa ambayo katika siku za hivi
karibuni imekuwa ikiitesa Simba kwenye michezo ya ligi na ile ya kirafiki.
Simba wamepandwa na mzuka hasa baada ya Yanga na
Azam kung’olewa kwenye michuano hiyo ambayo waliokuwa mabingwa mtetezi KCCA ya
Uganda walitolewa hatua ya robo fainali.
Habari za ndani zinadai kwamba vigogo watatu wa
klabu hiyo wamevuka mipaka kwa kumpa kocha mpya, Goran Kopunovic kikosi ambacho
wanataka kianze jambo ambalo vibosile wengine wakiongozwa na Rais Evans Aveva
wamelikemea vikali na kumtaka kocha kutotoa ruhusa kwa watu kuingilia kazi
zake.
Mashabiki wa Simba wameanza kumwagika kwenye
viunga vya Zanzibar tangu juzi Jumapili jioni na jana Jumatatu bendera za rangi
nyekundu zilitawala maeneo mengi ya Unguja ingawa Mtibwa nao walikuwa wajanja
kwa kufanya mazoezi na programu zao sirini sana.
Mchezo huo utakaoanza saa 2:15 usiku,
utazikutanisha timu zenye historia tofauti katika michezo mbalimbali ya fainali
ambayo wameshinda mara 15 wakipoteza mara 7.
Wekundu hao wamecheza fainali za Mapinduzi mara
nne na kuchukua mara mbili wakizifunga Mtibwa mwaka 2008 na 2011 wakiwafunga
Yanga 2-0 huku wakipoteza dhidi ya Azam kwa mabao 2-1 mwaka 2012 na mwaka jana
Mnyama alichapwa na KCCA mabao 2-0.
Mbali na mashindano hayo makali ya Simba katika
mechi za fainali pia yalionekana katika Kombe la Kagame ambalo walichukua mara
6 ambazo ni nyingi kuliko klabu yoyote ya Tanzania hata Afrika Mashariki yote.
Rekodi za Simba kwenye fainali pia zinaonyesha
Simba ilichukua kombe katika mechi za Kombe la Nyerere miaka ya 1984,1995,2000.
Mtibwa wameingia fainali ya mapinduzi mara mbili miaka ya 2007 alifungwa na
Yanga na 2008 ambapo walifungwa na Mnyama.
Mwaka 2009 ilichukua Kombe la Tusker dhidi ya URA
ya Uganda, pia Mtibwa ikalichukua tena kombe hilo mwaka 2010 kwa kuifunga Ocean
View, pia wamewahi kuingia fainali ya Kombe la ABC Bank mara moja na kufungwa
na Simba mabao 3-2.
Simba iliyoweka kambi katika eneo lao la Mbweni
Unguja na ikijifua katika Uwanja wa Chuo cha Ualimu Chukwani, itaingia uwanjani
ikiwa na kikosi tofauti na kile kilichokubali kipigo cha bao 1-0 dhidi ya
Mtibwa katika mechi ya kwanza ya hatua ya makundi.
Hiyo ni kutokana na kuwasili kwa nyota wake
wawili; Simon Sserunkuma na Emmanuel Okwi.
Ikiwa chini ya kocha Mserbia Kopunovic, Simba
imekuwa ikiongeza dozi ya mazoezi yake ambapo tangu ikijiandaa na mechi ya nusu
fainali timu hiyo imekuwa ikifanya mazoezi makali mara mbili kwa siku huku
kocha huyo akitamka kwamba sasa timu yake ipo tayari kwa pambano.
“Kichwani kwangu kuna mambo mawili muhimu, kwanza
maandalizi ya ligi ambayo ndiyo muhimu kwetu lakini la pili ni hii mechi ya
kesho (leo Jumanne) ambayo endapo tutachukua ubingwa utakaotusaidia kuingia
katika mechi za ligi tukiwa na morali mpya,”alisema Kopunovic.
“Bado hatujapata uhakika wa kumtumia Simon
Sserunkuma, anaonekana kuwa na maumivu lakini kila kitu tutajua kesho (leo)
endapo atakuwa bado na maumivu hatutamtumia, sitaki kumpa madhara makubwa kwa
ajili ya mchezo huu kwa kuwa sasa tunaye Okwi,”alisisitiza kocha huyo.
Mtibwa yashtukia ishu
Mtibwa imehofia hujuma zozote zinazoweza kufanywa
dhidi ya wachezaji wake na ilichofanya ni kutibua ratiba zake za mazoezi ili
kuichanganya Simba.
Mtibwa ambayo kwa msimu huu tayari imeshaifunga
Simba mara mbili na kutoka nayo sare moja, imejipanga kuhakikisha inaendeleza
rekodi yake hiyo ambapo katika maandalizi yake imelazimika kufanya mazoezi kwa
siri kubwa.
Timu hiyo inayofundishwa na kocha mzalendo, Mecky
Maxime, iliuanza msimu huu ikipata sare na Simba katika mechi ya Ligi Kuu Bara
iliyopigwa mjini Morogoro na baadaye kuibuka na ushindi wa mabao 4-2 katika
mchezo wa kirafiki uliopigwa katika Uwanja wa Chamazi kabla kuishinda tena
Simba bao 1-0 katika hatua ya makundi ya Kombe la Mapinduzi.
“Tunawaheshimu Simba, haina maana kwamba
tulipowafunga mchezo ule ulikuwa mteremko, tumeshasahau matokeo yaliyopita sasa
tunaanza upya,” alisema Maxime.
Mshindi kukabidhiwa kombe jipya
Kamati ya Maandalizi ya mashindano hayo kupitia
Katibu wake Hamis Abdallah, imesema kuwa mshindi wa mchezo huo ambao mgeni
rasmi atakuwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dr. Ali Mohamed Shein,
mbali ya donge la na Sh10 milioni, pia atapatiwa kombe jipya tofauti na lile
lililobebwa na mabingwa waliopita KCCA ya Uganda na medali za dhahabu
Mshindi wa pili atajizolea Sh5 milioni bila kombe
na medali za shaba kwa wachezaji wote 25 huku pia kukiwa na zawadi kwa mfungaji
bora, kipa bora na mchezaji bora wa mashindano hayo
Phiri ashauri
Kocha wa Simba aliyepigwa chini, Mzambia Patrick
Phiri, ameitakia kila la kheri timu hiyo katika fainali za Kombe la Mapinduzi
zitakazochezwa leo Jumanne usiku, lakini ametahadharisha kwamba wasipokuwa
makini wanaweza kufungwa na Mtibwa.
Akizungumza na Mwanaspoti kutoka Zambia, Phiri
alisema: “Mtibwa ni wazuri sana, lakini katika soka hiyo haijalishi sana kwani
inaweza kuwa nzuri na ikafungwa, kikubwa Simba watulie ili washinde mechi hiyo
vinginevyo ubingwa utaenda Mtibwa, nawajua Mtibwa kwani nimekutana nao kwenye
ligi na mechi ya kirafiki.”
Phiri hakuacha kuwazungumzia wachezaji wake nyota, Waganda Emmanuel Okwi na
Joseph Owino ambaye anatarajia kurejea nchini muda wowote wiki hii.
“Nafurahi kusikia Okwi yupo kambini na timu, ni
mchezaji mzuri ila anatakiwa kubadilika sasa, amekuwa mkubwa, anatakiwa kuwa na
nidhamu ili aendelee kuwa nahodha, Owino ni mchezaji muhimu kwenye timu,
viongozi watatue matatizo yake kwa kipindi, najua tofauti zilizopo kati ya
Owino na viongozi, ligi bado ngumu na uwepo wake unahitajika.”
Mgosi atishia nyau
STRAIKA wa Mtibwa Sugar, Mussa Hassan ‘Mgosi’
amesema endapo atashindwa kuifunga Simba kwenye mchezo wa fainali utakaochezwa
Uwanja wa Amaan Zanzibar leo Jumanne, basi washambuliaji wenzake Ally Shomary
na Ame Ally lazima watafunga kwenye mchezo huo.
“Tumejipanga kutwaa ubingwa wa Mapinduzi,
hatutazembea nafasi yoyote tutakayoipata kwenye mchezo wetu na Simba, tutacheza
kama timu kuhakikisha tunapata matokeo,” alisema straika huyo.
“Nisipowafunga mimi najua wenzangu watawafunga, safu
yetu ya ushambuliaji ni nzuri na tumekuwa tukicheza kama timu kwa muda mwingi,
hatuchezi kuangalia mtu mmoja anafanya nini, hata hivyo beki ya Simba
haijabadilika sana tangu tulipocheza nayo mechi ya mwisho.”
Source: Mwanaspoti
0 comments:
Post a Comment