Ibrahim Hajib (katikati) alishindwa kuiokoa Simba na kipigo cha 2-1 kutoka kwa Mbeya City fc licha ya kufunga goli la kuongoza
MABINGWA wa kombe la Mapinduzi 2015, Simba SC
kesho wanasaka pointi tatu kwa kila namna ili kupunguza machungu waliyopata kwa
kutandikwa mabao 2-1 dhidi ya Mbeya City katika mechi ya ligi kuu iliyopigwa
juzi, januari 28 uwanja wa Taifa Dar es salaam.
Simba watavaana na Maafande wa JKT Ruvu Stars wanaonolewa na kocha wa zamani wa Yanga, Fredy
Minziro, katika mechi ya VPL itayopigwa uwanja wa Taifa, Dar es salaam.
Huu ni mtihani wa tatu kwa kocha wa Simba SC,
Goran Kopunovic kwani tayari ameshaiongoza timu hiyo katika mechi mbili za ligi
kuu.
Kopunovic alianza ligi kuu kwa ushindi wa mabao
2-0 dhidi ya Ndanda fc, Januari 17 mwaka huu, kabla ya kulazimisha sare ya 1-1
na Azam fc, Januari 24 mwaka huu. Juzi wakalala 2-1 dhidi ya Mbeya City.
Tayari baadhi ya wanachama na mashabiki wa Simba
wameanza chokochoko wakimtaka Rais wa Simba, Evans Aveva ajiuzulu kutokana na
kushindwa kuweka umoja katika klabu hiyo.
Aveva ambaye haamini kama mgogoro wa Simba na
wanachama wake wa UKAWA ndio chanzo cha kuboronga kwa timu, amekaririwa mara
kadhaa kuwa uongozi wake hauko tayari na hauna mpango wa kukutana na kundi hilo
maarufu nchini.
Lakini jana, Mwenyekiti wa kamati ya usajili wa
Simba, Zacharia Hans Poppe ambaye alifungua milango kwa UKAWA kurudi klabuni
kama watafuta kesi yao Mahakamani alisema wanasimba hawana haja ya kuwalaumu
viongozi kwa matokeo mabaya.
“Mchezaji kukosa penalti (Masoud Nassor Cholo) unamlaumu
vipi kiongozi. Labda yeye ndiye aulizwe amekosaje penalti”. Alikaririwa Hans
Poppe akiwatetea viongozi kutohusika na matokeo hayo.
Hata hivyo alisema kuna haja ya kufanya uchunguzi
ili kubaini kama kuna hujuma klabuni hapo.
Simba inakabiliwa na matokeo mabaya ambapo mpaka
sasa wameshinda mechi mbili tu dhidi ya Ruvu Shootings na Ndanda fc katika
mechi 11 walizocheza.
Wamefungwa mara mbili dhidi ya Kagera Sugar na Mbeya
City na kutoka sare saba.
Tayari kocha Kopunovic ameshatoa kauli ya
kuwakatisha tamaa Wanasimba kwamba wasahau kutwaa ubingwa mwaka huu.
Kocha huyo alisema kama Simba wanawaza Ubingwa basi
nayeye atafukuzwa kama ilivyotokea kwa makocha wengine waliomtangulia kwani
haamini kama ana kikosi cha Ubingwa.
Mpaka sasa Simba wapo nafasi ya 11 wakijikusanyia pointi 13 katika mechi 11 walizocheza.
0 comments:
Post a Comment