Na Bertha Lumala
Simba SC na Mtibwa Sugar FC zimeambulia mgawo wa Sh. milioni 1.7 kila moja kutokana na mapato ya mlangoni katika mechi yao ya fainali ya Kombe la Mapinduzi ambayo Simba SC walishinda kwa penalti 4-3 dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar Januari 13 usiku.
Licha ya Uwanja wa Amaan kufurika watazamaji kila upande kiasi cha baadhi yao kulazimika kukaa ndani ya uzio nje kidogo mwa eneo la kuchezea (pitch) kinyume cha taratibu za soka, imebainika kwamba mechi hiyo kali ya fainali iliingiza Sh. milioni 27 tu.
Uongozi wa Simba Simba umeeleza kuwa mechi hiyo iliingiza kiasi hicho kiduchu kutokana na mauzo ya tiketi za Sh. 10,000 na Sh. 3,000.
"Inashangaza sana, Simba ndiyo ya kuambulia mgawo wa shilingi milioni moja na lakini saba (Sh. milioni 1.7), hapa tunatakiwa tupate shilingi milioni sita za kusafirisha timu kwa ndege kwenda Mtwara," alisema Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hanspope baada ya kupewa taarifa za mapato hayo.
Msemaji wa Simba, Humphrey Nyasio amesema wameambiwa na Kamati ya Mashindano hayo kuwa Sh. milioni 10 ni gharama za mechi na Simba SC imepata Sh. milioni 1.7 ikiwa ni asilimia 10 ya mgawanyo wa mapato.
Mtibwa Sugar FC, waliokuwa wenyeji wa mechi hiyo, walipata mgawo wa Sh. milioni 1.7 sawa na Simba SC.
Katibu wa Kamati ya Mashindano, Khamis Abdallah Said amesema kuwa mechi hiyo iliingiza Sh. 27,145,000 na wanafainali Mtibwa Sugar FC na Simba SC walipata asilimia 10 ya mapato yaliyobaki baada ya gharama za mechi kukatwa.
Baada ya kumalizika kwa hatua ya robo fainali, katibu huyo wa kamati alisema waliingiza Sh. milioni 116 katika mechi zote za hatua ya makundi hadi robo-fainali huku mechi zilizohusisha kikosi cha Yanga zikiongoza kwa kuingiza 'mpunga' mwingi.
0 comments:
Post a Comment