ROBO fainali ya kwanza ya kombe la Mapinduzi
inapigwa leo majira ya saa 2:15 usiku uwanja wa Amaan Zanzibar baina ya Simba
na Taifa ya Jang’ombe.
Mechi hii imetabiriwa kuwa tamu kutokana na
kiwango kikubwa walichoonesha Simba katika mechi ya mwisho ya makundi dhidi ya
JKU ambapo walishinda goli 1-0.
Siku hiyo Simba waliuanza mchezo kwa kasi katika
vipindi vyote, wakicheza pasi za haraka haraka na kutumia njia ya pembeni
kuipenya ngome ya JKU.
Kocha Goran Kopunovic alitumia muda mwingi
kuwaelekeza wachezaji wake namna ya kucheza mpira ambapo alisisitiza kwa ishara
akiwataka wachezaji wapigiane pasi na kushambulia kupitia mawinga na kukaba kwa
uangalifu.
Kocha huyo ameonekana kupenda kucheza mpira wa
kasi muda wote na amekuwa akiwapa wachezaji wake mazoezi magumu ya kuongeza
nguvu na pumzi.
Robo fainali nyingine tatu zitapigwa kesho uwanja
wa Amaan ambapo majira ya saa 9:00 alasiri, mabingwa watetezi, KCC ya Uganda
watachuana na Polisi Zanzibar.
Azam fc watashuka dimbani katika robo fainali ya
tatu majira ya saa 11:00 jioni kuonesha kazi na Mtibwa Sugar.
Hii itakuwa mechi kali kutokana na ubora wa timu
zote hususani Mtibwa Sugar wanaoongoza katika msimamo wa ligi kuu Tanzania
bara.
Robo fainali ya mwisho
itawakutanisha Yanga na JKU majira ya saa 2:00 usiku.
0 comments:
Post a Comment