Okwi (kulia) hachezi leo
Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
Wakati kikosi cha Mserbia Goran Kopunovic cha Simba SC kinawakosa viungo Emmanuel Okwi na Said Hamis Ndemla, wapinzani wao Mbeya City FC wanawakosa nahodha wao beki Hassan Mwasapili katika mechi yao ya leo.
Simba SC na Mbeya City FC zilizoambulia sare katika mechi zake za mwishoni mwa wiki, zitachuana vikali katika mechi pekee ya kesho ya kiporo ya raundi ya 10 ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) itakayochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam saa 10 jioni.
Kocha Mkuu wa Mbeya City FC, Juma Mwambusi, ameuambia mtandao huu jana mchana jijini hapa kwamba kikosi chake kiko vizuri kuwavaa Simba SC kesho licha ya kuwa hatarini kuwakosa nyota hao wawili.
Kwa mujibu wa ratiba ya VPL msimu huu, mechi hiyo ilipaswa kuchezwa Januari 11 lakini ikapigwa kalenda na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutokana na ushiriki wa Simba SC katika michuano ya Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar ilikoibuka bingwa.
Mwambusi amesema: "Tumejiandaa kwa mechi zote za msimu huu, kikubwa mashabiki wetu waje uwanjani kesho kuona soka safi maana kikosi chetu sasa kiko vizuri."
"Tuna wachezaji wengi ambao tumekuja nao hapa Dar es Salaam, kuna uwezekano mkubwa wa kuwakosa Mwasapili na Mwagane ambao leo wameshindwa kufanya mazoezi kutokana na matatizo yanayowakabili lakini hilo haliwezi kutudhoofisha kwa sababu tuna wachezaji zaidi ya 20," amesema Mwambusi.
Kocha Bora wa VPL msimu uliopita -- Mwambusi, amesema Mwagane anasumbuliwa na malaria wakati nahodha Mwasapili ana majeraha ya kifundo cha mguu.
Yeya anaikosa mechi ya leo
Mwagane ndiye mchezaji pekee wa Mbeya City FC mwenye rekodi ya kufunga mabao matatu peke yake katika mechi moja 'hat-trick' tangu timu hiyo ipande Ligi Kuu msimu uliopita.
Mkali huyo wa kupiga vichwa vitamu kuliko washambuliaji wengine wote Tanzania, alifunga hat-trick hiyo katika mechi yao ya mwisho ya mzunguko wea kwanza msimu uliopita walitoka sare ya 3-3 dhidi ya Azam FC Uwanja wa Azam, Dar es Salaam Novemba 7, mwaja juzi.
Mwasapili ni beki tegemeo na kiongozi katika kikosi cha Mwambusi, hivyo kukosekana kwake kesho huenda kukaiathiri timu hiyo ya Jiji la Mbeya.
Simba SC ambayo Jumapili ilishikwa kwa sare YA 1-1 dhidi ya vinara Azam FC, iko nafasi ya 10 katika msimamo wa ligi ikiwa na pointi 13 na itaingia Uwanja wa Taifa ikiwana kumbukumbu ya kutoka sare ya 2-2 dhidi ya Mbeya City FC msimu uliopita.
Mbeya City FC iko nafasi ya 12 ikiwa na pointi 12 baada ya kucheza mechi 10 sawa na Simba. Timu hiyo inayomilikiwa na Halmashauri ya Jiji la Mbeya, haijawahi kufungwa na Simba tangu ipande Ligi Kuu msimu uliopita wakitoka sare katika mechi zote mbili za VPL msimu uliopita.
Simba SC iliyoshinda mechi mbili tu katika mechi 10 zilizopita za VPL ikitoka sare mara saba na kupoteza mechi moja, itaingia Uwanja wa Taifa ikisaka ushindi wa pili nyumbani msimu huu dhidi ya kikosi cha Mwambusi ambacho kimeshinda mechi tatu tu kati ya 10 kikitoka sare mara tatu na kupoteza mechi nne.
Kiungo mshambuliaji wa Simba SC, Mganda Emmanuel Okwi hatakuwamo katika kikosi hicho cha Msimbazi kesho kutokana na maumivu ya shingo ambayo aliyapata katika mechi yao iliyopita alipopigwa kiwiko na kupoteza fahamu na beki kisiki Mzanzibar Aggrey Morris wa Azam FC.
Kiungo mwingine Ndemla ataikosa mechi hiyo baada ya kupimwa na daktari wa Simba SC, Yassin Gembe na kubainika kwamba atakaa nje ya uwanja kwa wiki mbili kuuguza majeraha ya nyama za paja aliyoyapata katika mechi ya fainali ya Kombe la Mapinduzi 2015 walilolitwaa baada ya kuifunga Mtibwa penalti 4-3 Uwanja wa Amaan, Zanzibar Januari 13.
Licha ya maumivu hayo, Ndemla aliendelea kupangwa katika kikosi cha Simba SC kilichoshinda 2-0 dhidi ya Ndanda FC Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara wiki mbili zilizopita, akapangwa pia katika kikosi cha Taifa Stars Maboresho kilichotoka sare ya 1-1 dhidi ya timu ya taifa ya Rwanda 'Amavubi' Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza Alhamisi kabla ya kujitonesha katika mechi iliyopita dhidi ya Azam FC Jumapili.
0 comments:
Post a Comment