Na Bertha Lumala
Baada ya kufanya vizuri katika michuano ya Kombe la Maopinduzi mwaka huu visiwani hapa, nyota sita wa timu za Ligi Kuu ya Zanzibar wameungana na mshambuliaji Amour Omary Janja wa JKU kugombewa kusajili na klabu kongwe nchini Simba SC na Yanga SC.
Mwishoni mwa wiki Janja aliyefunga mabao matatu katika mechi tano za michuano hiyo likiwamo bao bora lililowatoa Yanga robo-fainali, aliweka wazi kwamba klabu nne za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), Azam, Mtibwa, Simba na Yanga zimeshaanza kumtumia watu kwa nia ya kumsajili msimu ujao.
Hata hivyo, Janja si mchezaji pekee anayewania na vigogo hao wa soka nchini kwani kuna wachezaji wengine sita wanaowindwa vikali na timu hizo.
"Yanga wanamtaka kiungo wa Mafunzo FC ambaye alipasuka usoni wakati wa mechi yao ya Kundi C dhidi ya Simba (Ali Mbarouk Khamis). Azam FC wanamtaka Janja na kipa wa JKU aliyeibuka mchezaji bora wa mechi yao ya nusu-fainali dhidi ya Mtibwa (Mohamed Abrahman Mohamed).
"Kuna wachezaji wengine wanne wa Polisi Zanzibar wanaotakiwa na Simba, Yanga, Mtibwa na Azam lakini ninaona uhamisho wao utakuwa mgumu kutokana na kuwa waajiriwa wa jeshi," amesema kiongozi mmoja wa soka visiwani Zanzibar ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Chama cha Soka Zanzibar (ZFA).
Lakini, Simba SC, Yanga SC na Azam FC zimekuwa zikikatisha ajira za kijeshi za wachezaji wanaong'ara katika soka, miongoni mwao akiwa ni beki wa kati Aggrey Morris wa Azam FC.
Ingawa uongozi wa Azam FC haukutaka kukiri kusaka saini za baadhi ya nyota waliong'ara visiwani hapa katika michuano ya Kombe la Mapinduzi mwaka huu, mtandao huu unatambua kwamba wanalambalamba watalazimika kusaka kipya mzoefu kama watashindwa kumwongeza mkataba mpya kipa Mwadin Ali Mwadin ambaye mkataba wake unamalizika mwaka huu.
Mwadin anahusishwa kutaka kuihama Azam FC na kujiunga na Yanga SC kwa dau linalotajwa kuwa Sh. milioni 60.
Msemaji wa Simba SC, Humphrey Nyasio amesema: "Sijapewa taarifa hizo na uongozi, kama suala hilo lipo, litaanikwa baada ya kila kitu kukamilika maana hiki si kipindi cha usajili."
Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar, Mecky Mexime alisema katika mahojiano na kituo cha redio visiwani Zanzibar wiki hii: "Mtibwa itaendelea kusajili wachezaji wazuri kutoka Zanzibar. Tumeona wachezaji wazuri wakati wa michuano hii (Kombela Mapinduzi), hatuwezi kuweka wazi nani tutakayemsajili baadaye maana si wakati mwafaka."
0 comments:
Post a Comment