MCHEZO wa ligi kuu ya soka Tanzania Bara
kati ya Mbeya City Fc na Kagera Sugar uliopigwa kwenye uwanja wa CCM Kirumba
jijini Mwanza jana umemalizika kwa City kuibuka na ushindi wa bao 1-0,
lililofungwa na Peter Mapunda katika dakika ya 80.
Mara baada ya mchezo huo kocha wa City Juma Mwambusi aliwashukuru vijana wake kwa kucheza vizuri huku pia akiwapongeza kwa kuiwezesha timu yao kupata ushindi wa pili mfululizo.
“Tumecheza vizuri, nawapongeza waachezaji kwa kucheza kwa kiwango kizuri, hakika wamefanyia kazi yale yote tuliyowaeleza, huu ni ushindi wa pili mfululizo kwetu, sasa tunarudi nyumbani kujiandaa na mchezo unaofuata dhidi ya Prisons, shukurani zangu pia kwa mashabiki wetu ambao wamesafiri umbali mrefu kutoka Mbeya kuja kuisapoti timu yao hapa Mwanza “alisema Mwambusi akiongea na Tovuti ya klabu hiyo.
Katika mchezo huo
ambao City ilicheza ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa bao 1-0 iliyoupata kwenye
mchezo wa mzunguko wa 8 dhidi ya Ndanda Fc uliochezwa kwenye uwanja wa Sokoine
jijini Mbeya wiki mbili zilizopita, ilianza kwa mashambulizi ya nguvu ambapo Themi
Felix nusura aipatie bao la kuongoza mapema dakika ya 5 baada ya kupiga mpira
uliogonga mwamba wa juu na kuokolewa na walinzi wa Kagera Sugar.
Ikicheza kwa pasi
fupi na zenye kuonana City ilifanya shambulizi jingine kwenye lango la Kagera
Sugar kwenye dakika ya 15 lakini shuti la Fredy Cosmas lilishindwa kulenga
lango na mpira kutoka nje, Kagera walijibu shambulizi dakika ya 19 na
kupata kona ambayo haikuweza kuzaa matunda hivyo hadi kipindi cha kwanza
kinamalizika timu zote zilikuwa hazijafungana.
Mabadiliko
aliyoyafanya Kocha Juma Mwambusi katika dakika ya 75 kwa kumtoa Cosmas Fredy na
kumuingiza Peter Mapunda yalikuwa na manufaa makubwa kwa City kwani
dakika tano baadae Mapunda aliandika bao hilo baada ya kuvisha kanzu
golikipa wa kagera Sugar aliyetoka golini kujaribu kuwahi mpira uliokuwa umepigwa
na Paul Nonga.
katika kipindi hicho
cha pili Kagera Sugar walijitahidi kucheza kwa pasi fupi fupi na za haraaka
kujaribu kurudisha bao hilo lakini uimara wa safu ya kiungo ya City iliyokuwa
ikiongozwa na Stive Mazanda na pia Rafael Daud ilitosha kabisa kuvuruga
mbinu zote walikuwa wakizipanga huku uimara wa walinzi wa
kati Juma Nyoso na Yusuf Abdalah ulikuwa makini kusafisha hatari
zote , hivyo hadi mwisho matokeo yalisomeka 1-0.
0 comments:
Post a Comment