Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
Mwadui FC inayonolewa na kocha wa zamani wa Simba SC, Jamhuri Kihwelu 'Julio' imefanikiwa kuiondoa Toto Africans kileleni mwa msimamo wa Kundi B la Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara (FDL) baada ya kuifunga Green Warriors ya Dar es Salaam bao 2-1 jana.
Kwa ushindi huo, Mwadui FC iliyokuwa nafasi ya pili kabla ya mechi ya jana, imefikisha pointi 40, moja mbele ya Toto Africans ya Mwanza iliyokuwa kileleni ambayo leo itapepetana na Oljoro JKT ya Arusha.
Mechi ya Toto Africans dhidi ya Oljoro JKT inatarajiwa kuwa na upinzani mkubwa kutokana na hali halisi ya timu hizo katika msimamo na idadi ya mechi zilizobaki kabla ya kumalizika kwa ligi hiyo kupata timu nne zitakazopanda Ligi Kuu msimu ujao.
Oljoro JKT iliyoshuka daraja msimu uliopita, iko nafasi ya tatu katika msimamo wa Kundi B ikiwa na pointi 32, saba nyuma ya Toto Africans ambao wanaonekana wazi wamepania kurejea Ligi Kuu baada ya kuporomoka daraja misimu mitatu iiyopita.
Mwadui, iliyofanikiwa kupanda daraja msimu uliopita kisha kupokonywa tonge na Stand United ya Shinyanga iliyopewa pointi za mezani na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imebakisha mechi mbili dhidi ya Polisi Tabora na Bukina Faso ya Morogoro kukamilisha ratiba ya FDL msimu huu.
Mechi hizo zote mbili zitapigwa nyumbani kwa timu hiyo ya Mgodi wa Almasi mjini Shinyanga, hivyo ina nafasi nzuri ya kupanda Ligi Kuu kama ikitumia faida ya uwanja wa nyumbani.
Kwa mujibu wa ratiba ya FDL, Jumamosi Mwadui FC itamenyana na Polisi Tabora kabla ya kuivaa Bukinafaso ya Morogoro Jumatano katika mechi ya mwisho ya msimu huu wa FDL
MSIMAMO KUNDI B FDL
Na. Timu Pld W T L GF GD Pts
1 Mwadui 20 11 7 2 34:14 20 40
2 Toto African 19 12 3 4 31:15 16 39
3 JKT Oljoro 18 9 5 4 27:18 9 32
4 Polisi Tabora 18 9 5 4 16:09 7 32
5 Geita 18 7 3 8 19:18 1 24
6 Panone 18 5 8 5 13:14 -1 23
7 Kanembwa JKT 18 6 5 7 11:20 -9 23
8 Rhino Rangers 18 5 7 6 11:14 -3 22
9 Polisi Mara 17 4 7 6 18:26 -8 19
10 Bukinafaso 19 2 10 7 14:16 -2 16
11 Polisi Dodoma 19 3 6 10 9:24 -15 15
12 Green Warriors18 2 4 12 16:31 -15 10
0 comments:
Post a Comment