Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
MTIBWA SUGAR wamejiamini kuwafunga Simba katika
mechi ya fainali ya kombe la Mapinduzi itakayopigwa leo majira ya saa 2:15
usiku uwanja wa Amaan Zanzibar.
Baada ya mazoezi ya jana asubuhi katika uwanja wa
Mao Dse Tung mjini Zanzibar, Mtibwa walipumzika kutwa nzima na jioni
hawakufanya mazoezi kabisa wakidai wamemaliza kazi.
“Hatuwezi kufanya mazoezi mara mbili kwa siku
kwasababu ya Simba, tumefanya mazoezi asubuhi Mao Dse Tung, tumepumzika,
tunawasuburi Simba kesho (leo). Tuko vizuri kwa kila kitu, waleteni”. Alisema
msemaji wa klabu hiyo, Tobias Kifaru.
Mtibwa Sugar FC inayonolewa na nahodha wake wa zamani na
Taifa Stars, Mecky Mexime , imewahi kutinga mara tatu katika hatua ya fainali
ya michuano hiyo tangu ianzishwe 2007 ikifungwa na Yanga SC (2007), ikapoteza
dhidi ya Simba SC (2008) kabla ya kutwaa taji lake la kwanza 2010 ilipoifunga
Ocean View.
Timu
hiyo ya Manungu, Turiani takriban km 100 kutoka mjini Morogoro, itaingia
uwanjani leo ikiwa na nia ya kulipa kisasi kwa kufungwa na Simba SC katika
fainali ya pili ya michuano hiyo 2008.
Mtibwa
Sugar FC inaingia uwanjani pia ikihitaji kulinda heshima yake ya kutopoteza
mechi hata moja ya mashindano msimu huu.Timu hiyo imecheza mechi 8 za Ligi Kuu
ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu huu ikishinda nne (2-0 dhidi ya Yanga SC,
3-1 dhidi ya Ndanda FC, 1-0 dhidi ya Mgambo Shooting na 2-0 dhidi ya Mbeya
City) na kutoka sare nne (0-0 Polisi, 1-1 Simba SC, 1-1 Kagera Sugar FC na 1-1
Stand United).
Aidha,
Mtibwa Sugar FC haijapoteza hata mechi moja katika mechi zote tano zilizopita
za Kombe la Mapinduzi mwaka huu, tatu za Kundi C ilizoshinda 1-0 dhidi ya Simba
na kutoka suluhu na Mafunzo FC na sare ya 1-1 na JKU FC. Ikashinda kwa penalti
7-6 baada ya kutoka sare ya 1-1 na Azam FC robo-fainali kabla ya kuiondoa JKU
kwa penalti 4-3 baada ya suluhu katika dakika 90 nusu-fainali jana.
Wachezaji wa Simba wakishangilia moja ya goli walilofunga mechi za nyuma kombe la Mapinduzi
Mtibwa
Sugar FC iliifunga Simba SC mabao 4-2 katika mechi yao iliyopita ya kirafiki
kwenye Uwanja wa Azam, mechi iliyokuwa maalum kujipima nguvu kabla ya kuikabili
Yanga SC katika mechi ya Nani Mtani Jembe 2.
Kwa
kifupi, Simba SC haijawahi kuifunga Mtibwa Sugar FC nje ya Uwanja wa Taifa, Dar
es Salaam tangu kufariki kwa kiungo Mkongo Patrick Mafisango miaka mitatu
iliyopita.
Kwa
upande wao, wekundu wa Msimbazi, Simba SC, wamewahi kutinga fainali za Kombe la
Mapinduzi mara nne wakiifunga Mtibwa Sugar FC 2008, wakaifunga Yanga SC 2011
kabla ya kufungwa na Azam FC 2012 na mwaka jana kufungwa na KCCA ya Ligi Kuu ya
Uganda.
Simba
SC wataingia uwanjani kesho wakisaka taji na pia kulipa kisasi cha kugeuzwa
vibonde wa Mtibwa Sugar FC katika miaka mitatu iliyopita wanapocheza nje ya
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
0 comments:
Post a Comment