Na Bertha Lumala, Morogoro
Mshambuliaji Danny Mrwanda wa Yanga SC ameanza kuhesabu katika timu yake hiyo mpya baada ya kuifungia bao katika ushindi wa 1-0 dhidi ya Polisi Moro katika mechi pekee ya leo ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) Uwanja wa Jamhuri mjini hapa jana jioni.
Mrwanda ameifunga timu yake ya zamani, Polisi Moro dakika ya 42 akimalizia mpira uliotemwa na kipa Tony Kavishe wa Polisi Moro kufuatia shuti kali la krosi ya beki wa pembeni kulia Juma Abdul wa Yanga SC.
Hilo ni bao la tano kwa Mrwanda baada ya kufunga pia mabao manne katika mechi saba alizokichezea kikosi cha Kocha Adolf Richard cha Polisi Moro mwanzoni mwa msimu huu kabla ya kujiunga na Yanga SC dirisha dogo.
Mrwanda, ambaye hakufunga katika mechi mbili zilizopita ambapo Yanga SC ilitoka sare ya 2-2 dhidi ya Azam FC na 0-0 dhidi ya Ruvu Shooting, sasa yuko sawa na Ame Ally Amour wa Mtibwa Sugar FC na Rashid Mandawa wa Kagera Sugar wenye mabao matano pia.
Mrwanda pia hakufunga bao hata moja katika mechi nne za Kombe la Mapinduzi visiwani Zanzibar mapema Januari mwaka huu, sawa na mshambuliaji mpya mwenzake kwenye kikosi cha Jangwani Mrundi Amisi Tambwe ambaye pia aliambulia kapa Zanzibar.
Mliberia Kpah Sherman alifunga mabao mawili Zanzibar ingawa hajaonesha cheche za mabao VPL. Tambwe, ambaye leo alikuwa benchi muda wote wa mechi, ameifungia Yanga SC bao moja katika mechi tatu za VPL zilizopita tangu ajiunge nayo dirisha dogo baada ya kutemwa Simba SC.
Kwa ushindi huo, Yanga SC ambayo imeshinda mechi nyingine nne msimu huu dhidi ya Tanzania Prisons, JKT Ruvu, Stand United na Mgambo ikishikwa kwa sare na Simba SC, Azam FC na Ruvu Shooting Stars na kufungwa na wakatamiwa Mtibwa Sugar FC na Kagera Sugar FC, imefikisha pointi 18 baada ya kucheza mechi 10.
Kikosi hicho cha Pluijm sasa kiko kimepanda hadi nafasi ya pili ya msimamo wa VPL kikizidiwa pointi mbili na vinara Azam FC ambao pia wamecheza mechi 10 na leo wanakipiga dhidi ya Simba SC Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
WAKALI WA KUCHEKA NA NYAVU
7. Didier Kavumbagu Azam FC
------------------------------
5. Ame Ally Amour Mtibwa Sugar
Rashid Mandawa Kagera Sugar
Danny Mrwanda Polisi/Yanga SC
------------------------------
4. Rama Salim Coastal Union
Simon Msuva Yanga SC
Samwel Kamuntu JKT Ruvu Stars
------------------------------
3. Ally Shomary Sharif Mtibwa Sugar
Emmanuel Okwi Simba SC
------------------------------
2. Aggrey Morris Azam FC
Amisi Tambwe Simba/Yanga SC
Deus Kaseke Mbeya City FC
Ibrahim Hassan Tanzania Prisons
Jabir Aziz JKT Ruvu Stars
Jacob Masawe Ndanda FC
Mussa Mgosi Mtibwa Sugar FC
Najim Magulu JKT Ruvu Stars
Nassoro Kapama Ndanda FC
Nicholas Kabipe Polisi Moro
Shaban Kisiga Simba SC
------------------------------
0 comments:
Post a Comment