Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
Yanga SC baada ya kushikwa na maafande wa Ruvu Shooting Stars Jumamosi ya wiki juzi, ilipeleka malalamiko katika Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuwafungia marefa waliochezesha mechi hiyo na shirikisho hilo lilitekeleza kwa kumfunguia Mohamed Teofile aliyekuwa refa wa kati siku hiyo.
Simba SC nayo jana imeonekana kama kuiga nyendo hizo za Yanga SC baada ya kukutana na waandishi wa habari Dar es Salaam na kutaka mamlaka ya soka nchini ichukue hatua dhidi ya marefa wa mechi yake ya sare ya 1-1 dhidi ya Azam FC Jumapili kwa madai kwamba "waliachia matukio mengi ya hovyo likiwamo la Okwi kupigwa kiwiko na beki wa kati Aggrey Morris wa Azam FC.
Okwi alianguka na kupoteza fahamu baada ya tukio hilo lilitokea dakika kabla ya saa ya mchezo, na kulazimika kukimbizwa Hospital ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya uchunguzi zaidi baada ya kuzinduka na kuweka wazi kwamba alikuwa akijisikia maumivu makali. Kilichofuata ni nini? Tega sikio....
Uongozi wa Simba SC umewasilisha malalamiko yao kwa TFF kufuatia kitendo alichofanyiwa mchezaji wao huyo ukidai alipigwa kiwiko cha makusudi na beki huyo wa Azam FC.
Katibu Mkuu wa Simba SC, Steven Ally amesema jana Dar es Salaam kuwa wanaitaka TFF itoe adhabu kwa mchezaji aliyefanya kitendo hicho (Aggrey Morris) pamoja na mwamuzi aliyechezesha pambano hilo Keneddy Mapunda.
“Tungependa TFF, ifuatilie kwa makini swala hilo na kulichukulia hatua kwa kutoa adhabu za kikanuni na sheria za soka kwani mchezaji wetu ameumizwa sana na hakikuwa kitendo cha uungwana,” amesema Ally.
"Mbali na tukio la kuumizwa kwa Okwi, kulikuwa na matukio mengine mengi yasiyokuwa ya kiungwana mchezoni ambayo wachezaji wetu walifanyiwa na wapinzani wetu, Azam FC," amesema zaidi Ally.
Simba SC na Yanga SC zimekuwa zikiibuka na malalamiko, hasa dhidi ya marefa pindi zinapopata matokeo mabaya katika mechi zake.
0 comments:
Post a Comment