
Rahim Kangezi
BODI ya ligi kuu Tanzania bara amemtoza faini ya
laki mbili (200,000/=) na kumfungia miezi sita kutojihusisha na soka mmiliki wa
Africa Lyon ya Dar es salaam inayoshiriki ligi daraja la kwanza Tanzania bara,
Rahim Kangezi Zamunda.
Kwa mujibu wa barua yenye KUMB.TPLB/FDL/KF/499
iliyotumwa na Bodi kwenda kwa Kangezi leo hii januari 16 na mtandao huu kupata
nakala yake imeelezwa kuwa kikao cha bodi ya ligi na TFF kimekutana na kupitia
taarifa za makamisaa na waamuzi wa michezo iliyopita.
Barua hiyo iliyoandikwa na kaimu mkurugenzi wa
Bodi ya ligi, Fatma Abdallah imefafanua kuwa katika mchezo namba 70 (Africa
Lyon v African Sports) uliofanyika uwanja wa Karume, Kangezi ‘alimkwida’
mwamuzi na kumtolea lugha chafu, hivyo alivunja kanuni ya 40 (Udhibiti wa
viongozi) ambayo atatumikia adhabu ya kufungiwa kujishughulisha na michezo kwa
kipindi cha miezi sita (6) na kulipa faini ya Tsh 200,000.
Fatma katika barua yake ameeleza kuwa faini hii
lazima ilipwe kwa Bodi ya ligi kabla ya adhabu ya kufungiwa miezi sita kuisha,
vinginevyo Kangezi hataruhusiswa kujihusisha na michezo mpaka atakapolipa faini
hiyo.
Aidha barua imefafanua kuwa adhabu hiyo inaanzia
tarehe ya barua hiyo ambayo ni leo januari 16, 2015.
Pia kupitia barua hiyo, Kangezi ameonywa
kutokurudia kosa hilo, vinginevyo hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.
Nakala ya barua hiyo imetumwa kwa Mwenyekiti wa
Bodi ya ligi kuu na Mkurugenzi wa Mashindano TFF.
0 comments:
Post a Comment