WAGONGA Nyundo wa Mbeya, Mbeya City fc leo jioni
wanakabiliana na CDA ya Dodoma katika mechi ya kirafiki itayofanyika uwanja wa
Jamhuri Mkoani Dodoma.
Afisa habari wa Mbeya City, Dismas Ten ameuambia
mtandao huu kuwa mechi hiyo ambayo ni sehemu ya maandalizi ya mechi ya wikiendi
dhidi ya mahasimu wao wa jiji, Tanzania Prisons itatumiwa na kocha Juma
Mwambusi kuongeza makali ya wachezaji wake.
Kwa upande wa kocha mkuu Juma Mwambusi
amekaririwa na Tovuti ya klabu hiyo leo akisema: “Tumetoka kushinda mchezo uliopita kwenye uwanja wa ccm
kirumba na jumamosi ijayo tutakuwa na mchezo mwingine huko Mbeya dhidi ya
Tanzania Prisons, tuko hapa Dodoma kwa maandalizi ya mchezo huo ingawa kwetu
sisi kucheza na CDA ni sehemu ya kudumisha udugu wetu kimichezo, binafsi
nina imani kubwa na timu yangu na kwa uwezo wa mwenyezi mungu naamini
tutashinda pia mchezo ujao wa ligi kwa sababu tunataka kupata
pointi tatu kwenye kila mchezo unaokuja mbele yetu”. Amesema Mwambusi.
Katika hatua nyingine Afisa masoko
wa City Joseph Semu amesema kuwa jezi za msimu huu zitakuwepo uwanjani
hivyo mashabiki wote wenye kiu ya kuvaa jezi hizo waje uwanjani na zitauzwa
hapo kwa bei nzuri kabisa.
Mbeya City ilianza vibaya ligi, lakini safari hii
imepata ushindi mara mbili mfululizo kwani kabla ya kuifunga Kagera, iliitandika
Ndanda fc bao 1-0 katika mechi ya ligi kuu iliyopigwa desemba 28 mwaka jana.
0 comments:
Post a Comment