
SIKU zote mechi ya watani wa jadi inakuwa na
upinzani mkubwa ndani na nje ya uwanja.
Upinzani huu upo mpaka kwa mashabiki, wachezaji na
viongozi wa timu hasimu, mfano Simba na Yanga.
Ligi ya kuu Tanzania bara imekuwa na mechi
mbalimbali za timu hasimu katika mikoa tofauti. Kwa Dar es salaam na nchi nzima
watani wa jadi, Simba na Yanga wamekuwa na mvuto zaidi kila wanapokutana, iwe
mechi ya mashindano au ‘Bonanza’ kama la ‘Nani Mtani Jembe”.
Pia zimeongezeka mechi mbili kali Dar, Simba dhidi ya Azam na Yanga dhidi ya Azam
fc.
Lakini ukitoka nje ya Dar, mkoani Morogoro, Mtibwa
Sugar na Polisi Morogoro wamekuwa wapinzani wa kweli na kila wanapokutana
wanakaziana sana. Kwa Tanga, Coastal Union na Mgambo ni mahasimu wa jiji hilo
na kila wanapokutana cheche zinawaka moto.
Kibarua kingine kizito kimekuwepo jijini Mbeya
ambapo Mbeya City fc na Tanzania Prisons wamekuwa mahasimu wakubwa wa kisoka. Hizi
ni timu zinazotumia uwanja mmoja wa nyumbani ambao ni CCM Kumbukumbu ya
Sokoine.
Kesho jumapili zinakutana katika mechi ya ligi kuu
soka Tanzania bara.
Kikosi cha Prisons
TAKWIMU:
Prisons wapo nafasi ya mwisho wakijikusanyia
pointi 8 katika mechi 10 walizoshuka dimbani.
Wajelajela hao wameshinda mechi moja, wametoa sare
5 na kufungwa 4. Wamefunga magoli 6 na kufungwa 8. Tofauti ya mabao ya kufunga
na kufungwa ni -2.
Mbeya City fc wapo nafasi ya 11 wakijikusanyia
pointi 11 baada ya kushuka dimbani mara 9.
Wameshinda mechi 3, wamefungwa 4 na sare 2.
Wamefunga magoli 4 na kufungwa 6. Tofauti ya mabao ni -2.
Ukiangalia takwimu hizi, timu zote zimefungwa
idadi sawa ya mechi (4), lakini Prisons wamecheza mchezo mmoja zaidi ya City.
Prisons wamefunga magoli mengi zaidi ya City
(magoli 6), tafsiri yake wana safu yenye makali zaidi ya wapinzani wao
waliofunga magoli manne.
City wamefungwa magoli machache (6) kulinganisha na Prisons waliofungwa mabao 8,
hii maana yake safu ya ulinzi ya City ina ubora kiasi kulinganisha na Prisons.
Lakini tatizo kubwa la City lilikuwa safu ya
ulinzi na hata kocha Juma Mwambusi alikiri hilo. Alimsajili Juma Nyosso na safu
yake imeonekana kuimarika zaidi wakishirikiana na Yusuph Abdallah pamoja na
Yohana Morris.
Mbali na takwimu hizi, City walishinda 1-0 katika
mechi yao ya Mwisho iliyopigwa uwanja wa CCM Kirumba dhidi ya Kagera Sugar
januari 17 mwaka huu, wakati siku hiyo hiyo Prisons walitoka suluhu na Mgambo
JKT.
Kikosi cha Mwambusi kilianza vibaya, lakini mechi
mbili zilizopita dhidi ya Ndanda waliyoshinda 1-0 pamoja na ya KageraSugar wameonekana kubadilika na kuwa katika morali
kubwa.
Hata mashabiki wameendelea kuwa na moyo na timu
yao, hawajakata tamaa. Wanaingia katika mechi ya kesho wakilindwa na historia
ya ushindi dhidi ya Prisons.

Mashabiki wa Prisons
Hii ni mechi ya mahasimu wa mji wa Mbeya, kuna
mambo mawili makubwa ya kuzingatia;
Mosi; nidhamu ya wachezaji uwanjani, tunahitaji
kuona wachezaji wakifuata sheria zote 17 na kucheza mpira wa kiungwana. Mechi
za watani zinakuwa na presha kubwa, hata ufundi huwa hauonekani. Wachezaji mara
nyingi wanakamiana na walimu wanaingia kwa mbinu za kusaka matokeo zaidi kwa
lengo la kulinda heshima na sio kucheza soka la burudani.
Kwa mechi hii tunategemea kuona ufundi na mbinu za
Mwambusi na David Mwamwaja zikileta matokeo kwa timu itayokuwa bora.
Hakuna haja ya kucheza soka la kitemi kama mechi
za nyuma, mpira umebadilika, tunapenda kuona soka la kisasa na ufundi wa timu
nzima na mchezaji mmoja mmoja.

Pili; busara kwa mashabiki; mechi ya Prisons na Mbeya City mwaka jana
kulitokea tafrani kubwa ambapo mashabiki wanaodaiwa kuwa wa Mbeya City
walilishambulia gari la wachezaji wa Prisons na kupasua vioo. Baadhi ya
wachezaji walijeruhiwa. City walipigwa faini na TFF kwa makosa kama haya na
mengine yaliyowahi kutokea nyuma mfano siku walipocheza na Yanga Sokoine msimu
uliopita.
Safari hii hatutegemei kuona aina ya ushangiliaji
huu. Mpira ni mchezo wa furaha. Ushangiliwe kwa uungwana na kukubaliana na kinachotokea
uwanjani. Kila timu ina haki ya kushinda na kufungwa pia.
Mashabiki wasiingie na matokeo ya nje ya uwanja,
mechi inachezwa kadharani. Kinachotokea kiheshimike.
Kunaweza kuwa na makosa ya waamuzi kutokana na
ubinadamu, lakini isitumike njia ya vurugu kutatua mapungufu. Kuna njia sahihi
za kudai haki kama kuna tatizo kubwa la uwanjani.
Kila la kheri timu za Mbeya City na Prisons katika
mechi yenu ya kesho.
0 comments:
Post a Comment