Hamad Kibopile (kushoto) alihusika kuwaangamiza Simba
WAGONGA nyundo wa Mbeya, Mbeya City fc wanasaka
pointi tatu muhimu mbele ya Polisi Morogoro katika mechi ya ligi kuu soka
Tanzania bara itakayopigwa kesho uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro.
City ambayo ipo nafasi ya saba katika msimamo wa
ligi kuu ikijikusanyia pointi 15 kwa mechi 11 ilizocheza, itaingia uwanjani
kesho ikiwa na morali kubwa ya ushindi kufuatia kuiadhibu Simba mabao 2-1
katika mechi ya kiporo ya ligi kuu iliyopigwa jumatano ya wiki hii uwanja wa
Taifa , Dar es salaam.
Mabao ya City siku hiyo yalifungwa na Hamad
Kibopile na Yusuph Abdallah aliyefunga kwa mkwaju wa penalty, wakati la Simba
lilifungwa na Ibrahim Hajib.
Siku za karibuni wakali hao wa Nyanda za juu
kusini wamekuwa na matokeo mazuri baada ya kuanza vibaya msimu huu wakipoteza
mechi nne mfululizo.
Walianza ligi kwa kutoka 0-0 dhidi ya JKT Ruvu (septemba
20, 2014). Wakashinda bao 1-0 dhidi ya Coastal Union (septemba 27, 2014), mechi
hizo zilichezwa Sokoine Mbeya. Baadaye wakasafiri kwenda Mabatini Pwani (Oktoba
4, 2014) na kuambulia suluhu dhidi ya Ruvu Shootings.
Baada ya mechi hiyo, Mbeya City waliandamwa na
vipigo vinne mfululizo ambapo Oktoba 18, 2014 walifungwa goli 1-0 na Azam fc
uwanja wa Sokoine. Oktoba 26, 2014 katika uwanja huo huo walilala kwa mabao 2-0
dhidi ya Mtibwa Sugar.
Wakasafiri kwenda Tanga Novemba 2, 2014 na
kufumuliwa 2-1 na Mgambo JKT, kabla ya kula kichapo kingine cha 1-0 novemba 8,
2014 kutoka kwa Stand United.
Baada ya vipigo hivyo, Mbeya City wakaanza kupata
matokeo mazuri ambapo novemba 26, 2014 waliifunga Ndanda fc bao 1-0 katika
uwanja wa Sokoine, kabla ya kusafiri januari 17, 2015 na kuifunga 1-0 Kagera
Sugar katika uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Januari 24 walitoka
sare ya mabao 2-2 na mahasimu wao jadi, Tanzania Prisons uwanja wa Sokoine na
juzi jumatano waliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Simba.
Matokeo haya yanaonesha wazi City wamerudisha
makali yao na kurekebisha makosa waliyokuwa nayo hasa safu ya ulinzi ambapo
walimsajili Juma Nyosso anayecheza vizuri na Yusuph Abdallah.
Mazingira haya yanaifanya mechi ya kesho iwe na
mvuto na ushindani mkubwa.
0 comments:
Post a Comment