Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
Wakati kikosi cha Kagera Sugar FC kimepoteza mechi tatu mfululizo kwenye uwanja mpya wa CCM Kirumba jijini Mwanza, Kocha Mkuu Jackson Mayanja 'amekikimbia' kwa muda kikosi hicho ili apate muda wa kutosha wa kushiriki kozi ya mafunzo ya ukocha ya Leseni A ya Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF).
Mtandao huu umenasa taarifa kutoka nchini Uganda zikieleza kuwa Mayanja na makocha wengine 10 wa Kiganda wamo nchini humo wakiendelea na mafunzo ya kiwango tajwa hapo juu.
Mtandao wa Kawowo Sports wa Uganda umeripoti muda mfupi uliopita kuwa makocha tisa wa kiume na mmoja wa kike wa UIganda, jana Jumatatu walianza mafunzo hayo maalum ya ukocha wa kiwango cha juu maeneo ya Njeru, Jinja nchini Uganda, mafunzo ambayo yameandaliwa na Shirikisho la Soka Uganda (FUFA).
Mbali na Mayanja, makocha wengine wa Kiganda wanaoshiriki kozi hiyo ni; Paul Sali, Frank Anyau, Sam Simbwa (SC Vila), Mike Mutebi, George Semogerere (Somalia), Paddy Kintu , Moses Basena (Kira Young), aliyewahi kuinoa Simba SC ya Tanzania, Golola Edward (Vipers SC), Timothy Ayiekoh (SC Kakira) na Majidah Nantanda (Cranes).
Makocha hao 10 wako chini ya wakufunzi wa ufundi wa CAF Waganda; Jackson Nyiima, Asuman Lubowa, Tom Lwanga, Mujib Kasule na Livingstone Kyambadde pamoja na Mkufunzi Mkuu wa Ufundi wa CAF, Sunday Kayuni kutoka Tanzania.
Awali FUFA iliandaa kozi ya leseni B ya CAF iliyomalizika juzi Jumapili.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya FUFA na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya shirikisho hilo, Hamid Juma ndiye aliyefungua kozi hiyo jana.
Kozi hiyo itaendelea hadi Januari 31, hivyo kikosi cha Kagera Sugar kitakuwa chini ya Kocha Msaidizi Mrage Kabange kitakapokivaa kikosi cha 'maafande' wa Tanzania Prisons Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine mjini Mbeya siku hiyo ya kufunga kozi.
Makocha wazaliwa wa Uganda wanaokosekana katika kozi hiyo ni pamoja na Fred Kajoba wa Bright stars ya Ligi Kuu ya Uganda na Leo Adra wa Atlabara ya Afrika Kusini.
Uganda tayari ina makocha sita waliofuzu leseni A ya CAF, hivyo 10 wanaoshiriki kwa sasa wataongeza idadi kama wakifaulu.
CAF ‘A’ ndicho kiwango kikubwa cha ukocha barani Afrika ambacho pia ni sawa na UEFA ‘A’ barani Ulaya.
0 comments:
Post a Comment