Na Bertha Lumala
Licha ya kuipoka taji la Kombe la Mapinduzi, Kocha Mkuu wa Simba, Goran Kopunovic amekimwagia sifa kikosi cha Mtibwa Sugar akidai ndicho kikosi bora katika michuano hiyo mwaka huu.
Simba chini ya kocha huyo mpya, ni kama imeipoka taji Mtibwa Sugar ambayo haijapoteza hata mechi moja ya mashindano msimu huu ilipotwaa taji la tatu la Kombe la Mapinduzi baada ya kuifunga timu hiyo ya Manungu, Turiani penalti 4-3 baada ya kutoka suluhu katika dakika 90 za mechi ya fainali ya michuano hiyo mwaka huu iliyochezwa Uwanja wa Amaan, Zanzibar Janjuari 13.
"Mtibwa ni timu nzuri sana, imekamilikia kila idara. Ni timu nzuri kuliko zote zilizoshiriki michuano hii lakini haijawa na bahati katika penalti dhidi ya Simba.
"Pongezi nyingi kwa wachezaji wangu kwa kupigana mwanzo-mwisho dhidi ya timu ngumu ya Mtibwa, ninaamini tutaendelea kuimarika na kuwa na kikosi bora zaidi katika ligi kuu," amesema Kopunovic.
Taji hilo lilichagizwa kwa kiasi kikubwa na mabadiliko ya dakika ya mwisho yaliyofanywa na Mserbia huyo kwa kumtoa kipa kinda Peter Manyika Jr na kumuingiza 'kiboko ya matuta Kenya', Ivo Mapunda ambaye alipangua penalti mbili za Ibrahim Rajab 'Jeba' na Vicent Barnabas, ambaye kabla ya mechi hiyo alipiga penalti mbili maridhawa katika hatua ya robo-fainali na nusu-fainali.
Waliofunga penalti za Simba SC ni Awadh Juma, Hassan Kessy, Hassan Isihaka na Danny Sserunkuma wakati Shaaban Kisiga alikosa. Ally Lundenga, Shaaban Nditi na Ramadhan Kichuya walifunga penalti za Mtibwa Sugar FC.
"Ninawapongeza wachezaji wetu kwa kupambana hadi tumefika fainali, ni mafanikio makubwa kwetu maana penalti hazina mwenyewe. Sasa tunahamishia makali yetu tuliyoyanoa hapa Zanzibar katika Ligi Kuu ya Vodacom (VPL), " amesema Mecky Mexime, kocha mkuu wa Mtibwa Sugar FC.
Mtibwa Sugar FC imewahi kutwaa taji hilo mara moja 2010 ikiifunga Ocean View wakati Simba SC imetwaa taji la tatu. Tofauti na Simba SC na Azam FC, hakuna timu iliyowahi kutwaa ubingwa wa michuano hiyo zaidi ya mara moja tangu ianzishwe 2007 kuenzi Mapinduzi Tukufu ya Zanzibar yaliyofanywa Januari 12, 1964.
0 comments:
Post a Comment