Baadhi ya Wachezaji wa Kilimanjaro FC
Na Mwandishi Wetu, Moshi
KLABU ya Kilimanjaro FC ya Pasua, inayocheza ligi daraja la tatu ngazi ya mkoa wa Kilimanjaro, imepiga hatua moja mbele katika harakati zake za kutwaa ubingwa wa mkoa wa Kilimanjaro kwa kuifunga Afro Boys ya majengo, goli 1-0.
Goli la Kilimanjaro FC katika mchezo huo mkali wa raundi ya pili, hatua ya sita bora, uliopigwa juzi kwenye uwanja wa Ushirika, mjini Moshi, lilipatinana katika dakika 48, kipindi cha pili, likifungwa na Jackson Obadia "Messi" kwa shuti kali, akiunganisha pasi ya Ayubu Lipati.
Kwa ushindi huo sasa, Kilimanjaro FC, maarufu Mpira Pesa, inahitaji kushinda mchezo mmoja tu kati ya michezo yake miwili iliyosalia ili kutangazwa bingwa wa msimu 2014/2015.
Mpaka sasa timu hiyo, imeshajikusanyia Pointi 19, ambapo inahitaji mchezo mmoja mmoja tu kati yake na Polisi Kilimanjaro, utakaopigwa siku ya Ijumaa, ambao utaifanya ifikishe pointi 22 ambazo hamna timu yoyote inayoweza kufikisha.
Msimamo wa ligi hiyo unaotarajiwa kumalizika, Februari mosi mwaka huu, unaonesha kuwa Kilimanjaro FC inaongoza kwa pointi 19, ikifuatiwa na Hai City, yenye pointi 15 sawa na Afro Boys, iliyoko katika nafasi ya tatu, zikizidiana kwa tofauti ya magoli.
Nafasi ya nne ni Polisi Mwanga yenye pointi 13 na mchezo mmoja mkononi, nafasi ya tano ni Polisi Kilimanjaro yenye pointi 4 huku Sango FC isiyokuwa na Pointi hata moja ikiridhika na nafasi ya mwisho.
0 comments:
Post a Comment