Mchezaji bora wa mechi, Kessy (kulia)
HASSAN Ramadhan Kessy aliyechaguliwa kuwa mchezaji
bora Simba ikitinga nusu fainali ya kombe la Mapinduzi kwa kuifunga mabao 4-0
Taifa ya Jang’ombe katika kipute cha robo fainali kilichofanyika uwanja wa
Amaan jana usiku ameigomea zawadi hiyo.
Akizungumza jana na mtandao huu dakika chache
baada ya mechi kumalizika, Kessy
alimshukuru Mungu kwa kucheza vizuri na kuchaguliwa kuwa mchezaji bora wa mechi
na kupewa zawadi ya King’amuzi cha Azam TV.
Hata hivyo beki huyo wa kulia aligoma kupewa hadhi
ya kuwa mchezaji bora badala yake alisema mfungaji wa mabao matatu katika
ushindi wa Simba, Ibrahim Hajibu ‘Mido’ ndiye alistahili kuwa mchezaji bora.
“Nimepewa zawadi, nashukuru. Lakini sijui
wametumia vigezo gani, mimi naona Hajibu (Ibrahim) alistahili kuwa mchezaji
bora”. Alisema Kessy.
Nyota huyo aliyejiunga na Simba wakati wa dirisha
dogo la usajili desemba mwaka jana akitokea Mtibwa Sugar alisema kikosi cha
Simba kinazidi kuimarika chini ya kocha mpya.
“Tunashukuru Mungu tunacheza vizuri. Kocha amekuja
na mbinu mpya. Mashabiki ‘waisapoti’ timu yao. Simba ni timu yetu sote, tukiwa
na umoja tutafanya vizuri”. Alisisitiza Kessy.
Dakika za lala salama katika mechi hiyo, Kessy
alitolewa na nafasi yake ilichukuliwa na beki mkongwe, Masoud Nassor ‘Cholo’.
Simba inasubiri mpinzani wake wa nusu fainali
katika mechi ya mapema leo saa 9:00 alasiri baina ya mabingwa watetezi wa kombe
hilo, KCC ya Uganda na Polisi Zanzibar.
Mechi nyingine ya robo fainali itaanza majira ya
saa 11:00 jioni baina ya Azam fc na Mtibwa Sugar, wakati saa 2:15 usiku katika
uwanja huo wa Amaan, Yanga watahitimisha
hatua hiyo kwa kuchuana na JKU ya Zanzibar.
0 comments:
Post a Comment