IPO misemo mingi ambayo huashiria kutokea kwa
jambo liwe nzuri au baya, moja ya misemo hiyo ni ule usemao dalili ya mvua ni
mawingu.
Msemo huu unaweza ukawa na na maana kubwa hivi
sasa kwa golikipa wa timu ya Dar es salaam Young African, Juma Kaseja
ambaye hivi sasa inaonekana hana mawasiliano mazuri na uongozi wa timu hiyo
yenye maskani yake mitaa ya Twiga na Jangwani jijini Dar es salaam.
Mchezaji huyo mwenye heshima kubwa nchini mwishoni
mwa mwaka uliopita aliachwa katika kikosi cha timu hiyo kilichoelekea visiwani
Zanzibar kushiriki michuano ya mapinduzi, lakini isitoshe jina la Kaseja
halijaonekana kwenye orodha ya wachezaji wa timu hiyo iliyotumwa shirikisho la
soka barani Afrika CAF kwa ajili ya ushiriki wa kombe la shirikisho.
Matukio hayo yote yameibua maswali mengi kwa
wapenzi na mashabiki wa timu hiyo juu ya hatma ya mlinda mlango huyo, hatua
iliyotufanya tumtafute afisa habari na mawasiliano wa klabu hiyo Jerry Muro
kutaka kufahamu kinaga ubaga kinachoendelea kati ya Kaseja na Yanga..
Muro amesema Kaseja kutohusishwa katika kikosi
kilichopo Zanzibar na kilichotumwa CAF ni kujitakia mwenyewe.
Jerry Muro
“Ni vizuri tukianza kuwakumbusha wapenzi wetu
tulipotoka tulipo na tunapoelekea na mimi nilipoingia nililikuta hili tatizo lipo
na tulipoamua kulifuatilia na kulipatia ufumbuzi, lazima tuseme ukweli na kweli
itatuweka huru, matatizo ya Juma Kaseja na Yanga yalisababishwa na yeye
mwenyewe alipoona hana kipaumbele na
Yanga”.
Na hii ilitokana na kutokupangwa mara kwa mara
katika michezo mingi ya Yanga tofauti na zamani watu walivyokua wakimuelewa
kama kipa bora Tanzania, lakini kwa mabadiliko ambayo klabu imekua ikipitia kwa
namna moja na kwa mahitaji ya timu labda yalikua hayamfurahishi Juma kama
binadamu’’ alisema.
Muro ameendelea kusema kwamba “ndani ya uongozi wa
yanga benchi la ufundi liliamua kumtumia Dida kutokana na uwezo wake jambo
ambalo Juma hakupata nafasi kutokana na mahitaji ya timu hali iliyopelekea
baadhi ya mashabiki kulalamika kwa nini hapangwi”
“Lakini tuweke kumbukumbu zetu vizuri Kaseja
kapangwa mechi ya Mtibwa kafungwa magoli mawili, kachezeshwa mechi dhidi ya CDA
ya kirafiki na nyingine kule Shinyanga,
pia ikumbukwe wakati Juma yupo Simba na hata na Yanga alikuwa anapangwa
michezo yote hadi ya kirafiki, mbona wenzake hawakulalamika hadi kuamua
kuondoka?
“ Lakini kwanini watu wanahoji kipindi hiki
ambacho klabu imeamua kuinua vipaji na kutafuta watu wengine wa kuchukua nafasi
ya Juma …? Aliuliza Muro, na kuongeza huo ndio mgogoro na Juma na sio wa
maslahi…
Kuhusiana na kutoonekana mazoezini Muro
amesema juma alipoona hapewi nafasi akaamua mwenyewe kuacha kuhudhuria mazoezi
na tatizo hili lilianza taratibu.
“Ghafla Juma akasema haji mazoezini kwa sababu
anaidai Yanga mara akageuka akaandika barua akasema hana matatizo na Yanga,
mara mwanasheria wake akatuandikia barua ya masuala ya kisheria”
Hata hivyo, Muro amesema kuhusu ni lini Juma
hajafika mazoezini aulizwe mwenyewe lakini kama hafanyi kazi hakuna
atakacholipwa na wanataratibu zao.
“Hata kama una mkataba haufanyi mazoezi haulipwi
na hili hatupepesi macho kama hatuna taarifa zako kutoka kwa mwalimu au daktari
wa timu hatujui kuhusu mambo yako ya familia huji mazoezi hulipwi chochote na hatulipi
chochote”.
Huo ni upande wa Yanga ambayo bado ina mkataba na
Kaseja, mchezaji mwenyewe anasemaje! Juhudi za kumtafuta Juma Kaseja
zinaendelea.
0 comments:
Post a Comment