Na Bertha Lumala
Unajua kwamba Yanga SC inajipanga kutinga FIFA na Mahakama ya Kazi kuwashtaki baadhi ya wachezaji wake wa zamani? Tega sikio...
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hanspope ameionya Yanga SC kuhusu hatua inazotaka kuzichua za kumshtaki kiungo mshambuliaji Emmanuel Okwi wa Simba SC katika Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
Jumatatu Yanga SC kupitia kwa Mkurugenzi wake wa Sheria, Frank Chacha iliweka ilitangaza kuwa inatarajia kuwafikisha kwenye shirikisho hilo lenye mamlaka ya juu kisoka duniani wachezaji Okwi, Mbrazil Genilson Santos Santana 'Jaja' na kipa mzawa Juma Kaseja ikiwadai fidia ya zaidi ya Sh. bilioni mbili kwa kuvunja mikataba ya kuitumikia klabu hiyo ya Jangwani.
Hata hivyo, Hanspope ameitaka Yanga SC kuwa makini na suala la Okwi kwa vile "mkataba wa Yanga SC na mchezaji huyo ulikuwa batili."
"Hiyo mahakama wanakokwenda, waende wakijua wanafanya kitu gani. Kwa sababu wakishindwa, madai yao yanaweza kuwageuka, sisi tutawageukia wao watulipe fidia ya hela hiyo wanayoitaka.
"Wanaelewa wazi kabisa kwamba mkataba waliambiwa ni batili. Sasa wanadai mkataba gani tena? Nia yao ni kumharibu mchezaji wetu kisaikolojia lakini mchezaji mwenyewe ni mzoefu.
"Tunajua uwezo wake ingawa haukuwa vizuri katika mechi ya fainali ya Kombe la Mapinduzi kutokana na mapumziko lakini ni mchezaji ambaye anafanya mazoezi kwa muda mfupi na kuwa katika kiwango chake," amesema zaidi Hanspope,
Chacha katika maelezo yake Jumatatu alisema Okwi aliyesajiliwa na Yanga SC kwa mkataba wa miaka mitatu mwaka jana, anatakiwa kuilipa Yanga fidia ya dola za Marekani milioni moja (Sh. bilioni 1.7) kwa kuvunja mkataba bila sababu za msingi, Jaja wanamdai fidia ya dola la Marekani 154,000 (Sh. milioni 267,000) na Kaseja Sh. milioni 396.
Chacha alikwenda mbali zaidi kwa kusema kuwa Kaseja watamshitaki pia katika Mahakama ya Kazi lakini Okwi na Jaja watawapeleka moja kwa moja FIFA kwa sababu wao ni wachezaji wa kimataifa.
Kabla ya kufungwa kwa dirisha kubwa la usajili msimu huu, Okwi alijiunga na Simba SC dakika za mwisho akitokea Yanga SC ambako Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilijiridhisha kuwa mkataba wa nyota huyo na wanajangwani ulikuwa umevunjwa kabla ya kumwidhinisha kuitumikia Simba SC.
0 comments:
Post a Comment