Ibrahim Hajibu akiwa na mpira wake uliopewa jana usiku baada ya kufunga 'Hat-trick'
MFUNGAJI wa mabao matatu ‘Hat-trick’ Simba
ikishinda mabao 4-0 dhidi ya Taifa ya Jang’ombe
katika mchezo wa robo fainali ya kwanza ya kombe la Mapinduzi, Ibrahim
Hajibu ‘Mido’ alipewa jukumu maalumu la kuwaliza Wazanzibar uwanja wa Amaan
Zanzibar jana usiku.
Nyota huyo aliyeingia mapema kipindi cha pili
akitokea benchi na kuchukua nafasi ya Elius Maguli aliuambia mtandao huu baada
ya mechi kuwa kocha Goran aliona mapungufu ya wapinzani wao, hivyo akampa mbinu
ya kwenda kufunga magoli.
“Nimefurahi sana kufunga mabao matatu. Kocha
alinipa majukumu ya kufunga, namshukuru Mungu nimefanikiwa”. Alisema Hajibu.
“Kinachosumbua ni nafasi, kila mwalimu anaponipa
nafasi lazima nifanye vizuri”.
“Mashabiki wa Simba watarajie mambo mazuri kwani
timu inazidi kuimarika”
Nyota huyo alikabidhiwa mpira wake baada ya ‘Hat-trick’
na alifafanua kuwa ni jambo kubwa kwake na kwa Wanasimba wote.
Hiyo ni ‘Hat-trick’ ya pili katika mashindano haya
kwani ya kwanza ilifungwa na Saimon Msuva katika mechi ya kwanza ya kundi A
Yanga ikishinda mabao 4-0 dhidi ya Taifa ya Jang’ombe.
Taifa ya Jang’ombe imeweka rekodi ya kusababisha
‘Hat-trick’ mbili katika mashindano haya mpaka kufikia hatua hii ya robo
fainali.
Pia ndio timu iliyopata kipigo kinachofanana cha
mabao 4-0 dhidi ya timu Kurwa na Doto za Kariakoo yaani Simba na Yanga katika
mashindano haya.
0 comments:
Post a Comment