MMOJA wa mabeki mahiri kwenye Ligi Kuu Bara anayeichezea Ruvu Shooting, George Osei, amefichua siri ya uwanjani ya straika wa Yanga, Kpah Sherman, kwamba ni miongoni mwa wachezaji ambao mabeki wanapaswa kuwaingia kwa umakini mkubwa.
Beki huyo amekuwa na rekodi za kuwadhibiti mafowadi wajanja akiwemo Amissi Tambwe, lakini amekiri kuchemka kwa Sherman kwa kile alichoelezea kwamba ukimfanyia kitu mchezaji huyo anajibu mapigo hapohapo wala hakulazii damu na atakachokifanya hata wachezaji wenzako wanaweza wasikione.
Beki huyo aliwahi kumchezea ubabe Tambwe kiasi cha kumchana mdomo, lakini amekiri kumshindwa Mliberia huyo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Osei alisema alishangazwa na Tambwe ambaye kwenye mechi dhidi ya Ruvu Shooting alianza kukumbushia vurugu zao jambo ambalo hakulitaka lakini alipojaribu kumchezea ubabe Sherman alikutana na kitu tofauti ambapo alimrudishia kila alichomfanyia.
“Tambwe sikuwa na lengo la kumchezea ubabe, nilijua hayo aliyaacha Simba lakini alipoanza kunichezea vibaya nami nikasema simuachi, lakini huyu Mliberia Sherman ni mbabe sana nilimshindwa,nilimtisha kama mara mbili ili atulie ikiwa ni pamoja na kumfanyia ubabe kama ule wa Tambwe naye hakutulia nilichomfanyia naye alinivizia na kunirudishia kwa siri, anajua kumiliki mpira haogopi beki.
“Siyo mchezaji mlaini, anajua kazi na ukimfanyia kitu anakurudishia hapo hapo kijanja,”alisisitiza mchezaji huyo.
Msuva anena
Kitendo cha Simba na Azam kushinda mechi zao za wikiendi iliyopita kimemkera Simon Msuva wa Yanga iliyotoka suluhu na Ruvu Shooting.
“Niliumia sana kusikia filimbi ya mwisho inapulizwa huku matokeo yakiwa 0-0, nikakumbuka nafasi ambazo tulizipata na hasa mimi nikashindwa kufunga au kuwatengenezea wenzangu, nimeumia sana ndiyo maana naomba radhi kwa wenzangu na hata mashabiki wa timu,” alisema.
“Huwezi kucheza katika ubora wako kila siku lakini pia hili la Simba na Azam kushinda nalo linachangia mashabiki kuwa na hasira zaidi, naomba watulie tutawafurahisha mchezo ujao.” Kocha mkuu wa Yanga, Mholanzi Hans Pluijm anashangaa kikosi chake kucheza mchezo wa kuvutia lakini wanakosa mabao .
Hata hivyo kiungo wake, Mnyarwanda Haruna Niyonzima, amemtuliza kwa kumwambia: “Haikuwa bahati yetu tu, lakini tunapanga kuwapa mashabiki raha mechi ijayo dhidi ya Polisi Morogoro.”
Source: Mwanaspoti
0 comments:
Post a Comment