Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
Magoli mawili ya mshambuliaji Mrundi Didier Kavumbagu na moja la Muivoru Coast Kipre Tchetche yameirejesha kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) Azam FC baada ya kuichapa Kagera Sugar FC magoli 3-1 katika mechi pekee ya ligi hiyo iliyochezwa leo Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Matokeo hayo yameifanya Azam FC, iliyopoteza mechi mbili msimu huu dhidi ya JKT Ruvu Stars na Ndanda FC, ifikishe pointi 20 na kurejea kileleni mwa msimamo ikifuatwa na wababe Mtibwa Sugar FC wenye pointi 17 wakiwa ni timu pekee ambayo haijapoteza mechi hata moja msimu huu.
Nafasi ya tatu inakaliwa na JKT Ruvu Stars yenye pointi 17 pia, mbili mbele ya Yanga SC na Polisi Moro FC waliopo nafasi za nne na tano. Kagera Sugar FC imeendelea kubaki nafasi ya sita ikiwa na pointi 14. JKT Ruvu Stars, Kagera Sugar FC na Polisi Moro FC wamecheza mechi 11 wakati Mtibwa Sugar FC na Yanga FC wamecheza mechi tisa huku vinara Azam FC wakiwa wamecheza mechi 10.
Azam, watakaovaana na Simba SC Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Jumamosi, wamekwenda mapumzikoni wakiwa mbele kwa mabao 2-0 yaliyofungwa na Tchetche na Kavumbagu dakika za 3 na 49. Mchezaji Bora wa Novemba, Rashid Mandawa ameifungia bao la kufutia machozi Kagera Sugar FC kabla ya Kavumbagu kuongeza la tatu na kuifanya timu hiyo ya Kagera ipoteze mechi ya pili mfululizo kwenye Uwanja mpya wa CCM Kirumba.
Kagera Sugar FC inayonolewa na Mganda Jackson Mayanja, ilipoteza 1-0 dhidi ya Mbeya City FC katika mechi iliyopita kwenye uwanja huo Jumamosi.
Kavumbagu amefikisha mabao 7 msimu huu akimkimbia Ame Ally Amour wa Mtibwa Sugar FC kileleni mwa wafumania nyavu hatari msimu huu. Mandawa naye amefikisha mabao matano sawa na Amour, bao moja mbele ya Samuel Kamuntu wa JKT Ruvu Stars, Rama Salim wa Coastal Union FC, Simon Msuva wa Yanga SC na Danny Mrwanda wa Yanga SC, ambaye hata hivyo mabao yote manne aliyafunga akiwa na kikosi cha Adolf Richard cha Polisi Moro FC.
Baada ya mechi dhidi ya Simba SC, Azam FC itakwea pipa kwenda DRC kushiriki mashindano maalum ya kimataifa nchini humo kabla ya kuivaa El Merriekh FC katika hatua ya awali ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika katikati ya mwezi ujao.
Usiku huu El Merreikh iliyotwaa taji la Ligi Kuu ya Sudan mara 19, inamenyana na timu isiyokuwa na kocha mkuu, KCCA ya Uganda katika mechi ya kimataifa ya kirafiki inayochezwa mjini Khartoum, Sudan.
Kocha Mkuu wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Uganda KCCA, Abdallah Mubiru hakusafiri na timu yake hiyo kwenda Sudan kutokana na kuhudhuria mafunzo ya kozi ya CAF ya ukocha inayoendelea mjini Njeru, Uganda.
Msaidizi wake John Luyinda ndiye anayekiongoza kikosi hicho kilichovuliwa ubingwa wa Kombe la Mapinduzi baada ya kutolewa kwa penalti robo-fainali na Polisi Zanzibar.
Baada ya mechi ya leo, Meneja wa Azam FC, Jemedari Said amesema: "Kabla ya hatujaja Kanda ya Ziwa, nilisema tuna malengo ya kukusanya pointi 9 dhidi ya Stand United FC, Kagera Sugar FC na Simba SC kabla ya kwenda DRC."
"Tumemaliza kazi Kanda ya Ziwa, kilichobaki ni kuchukua pointi kwa Simba SC kabla ya kwenda kushiriki mashindano ya kimataifa DRC kujiandaa vyema kwa ajili ya mechi zetu za Klabu Bingwa Afrika mwezi ujao," amesema zaidi Jemedari.
Kikosi cha Azam FC leo kimeanza na Aishi Manula, Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, Said Morad, Serge Wawa, Michael Bolou, Mudathir Yahya/ Amri Kiemba, Frank Domayo/ Gaudence Mwakimba, Didier Kavumbagu, Kipre Tchetche na Brian Majwega.
0 comments:
Post a Comment