Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu yaVodacom Tanzania Bara (VPL), Azam FC wamewasili salama DR Congo tayari kwa mashindano mafupi yaliyoandaliwa na timu ya TP Mazembe ya nchini humo.
Katika michuano hiyo inayotarajia kuanza kesho na kufikia tamati februari 3 mwaka huu, timu nne zitachuana ambazo ni Azam FC, TP Mazembe, Don Bosco na mabingwa wa Zambia, Zesco FC.
Azam FC kesho saa 11 jioni kwa masaa ya Tanzania iikiwa ni saa 10 jioni DR Congo, watacheza dhidi ya TP Mazembe. mechi itakayotanguliwa na mchezo kati ya Zesco dhidi ya Don Bosco.
Azam FC waliondoka alfajiri ya leo kuelekea DR Congo ambapo kwa mujibu wa taarifa iliyowekwa katika ukurasa wa Azam FC, wamewasili salama.
"Kikosi cha Azam FC kimetua salama Lubumbashi, DRC kwa Kenya Airways," imeeleza taarifa hiyo iliyopo ndani ya ukurasa wa Azam FC wa facebook.
Katika hatua nyingine, kituo cha televisheni cha Azam TV kitaonesha michezo hiyo kwa mujibu wa taarifa iliyowekwa kwenye ukurasa huo.
Azam FC inayonolewa na Mcameroon Joseph Marius Omog, inayatumia mashindano hayo kujiandaa kwa mechi yao ya kwanza ya hatua ya awali ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika dhidi ya mabingwa mara 19 wa Ligi Kuu ya Sudan, El-Merrikh itakayochezwa Februari 15 Uwanja wa Azam, Dar es Salaam.
0 comments:
Post a Comment