
OKTOBA 18 mwaka huu, Dar Young Africans ilichuana na
mahasimu wake wa jadi, Simba Sports Club
katika dimba la Taifa jijini Dar es salaam.
Mechi hii ilikuwa na mvuto wa aina yake kutokana na
matokeo ya mechi za nyuma kwa timu zote.
Simba waliingia uwanjani wakiwa na kumbukumbu ya
sare tatu katika mechi tatu za mwanzo ambapo walianza ligi kwa kutoka sare ya
mabao 2-2 dhidi ya Coastal Union, wakalazimishwa sare ya 1-1 mara mbili dhidi
ya Polisi Morogoro na Stand United.
Mnyama aliingia kwa hesabu za kutafuta pointi tatu
za kwanza mbele ya mtani wake wa jadi na wakaamua kujificha nchini Afrika
kusini kusaka makali.
Hata hivyo kambi hiyo iliyowekwa ‘Bondeni kwa Mzee Madiba’
haikuwasaidia vijana wa Patrick Phiri kuifunga Yanga.
Yanga wao waliingia uwanjani wakiwa tayari
wameshaonja ladha ya ushindi mara mbili, ingawa walianza kwa kutandikwa mabao
2-0 na Mtibwa Sugar katika mechi ya ufunguzi wa ligi kuu iliyopigwa septemba 20
mwaka huu uwanja wa Jamhuri Mkoani Morogoro.
Yanga walishinda mabao 2-1 mara mbili dhidi ya Maafande wa Tanzania Prisons ‘wajelajela’ na JKT
Ruvu.
Mechi ya Yanga na Simba ilihudhuriwa na mashabiki
lukuki, lakini ilimalizika kwa suluhu pacha ya bila kufungana.
Timu zote zilicheza kwa umakini, ufundi na nguvu,
lakini washambuliaji wa timu zote walishindwa kutumia nafasi walizopata.
Rekodi
iliyowekwa baada ya matokeo hayo ni timu hizo kongwe kutoka sare katika
mechi zao tatu za ligi kuu zikiwa na makocha tofauti.
Msimu
uliopita mzunguko wa kwanza, Simba na Yanga zilitoka sare ya mabao 3-3.
Yanga walianza kufunga mabao 3-0 kipindi cha kwanza,
lakini Simba walikuja juu kipindi cha pili na kusawazisha yote.
Wakati huo, Simba ilikuwa chini ya kocha mkuu Alhaj
Abdallah Athuman Seif maarufu kwa jina la King Abdallah Kibadeni akisaidiwa na
kocha mwenye maneno mengi, Jamhuri Kiwhelo ‘Julio’.
Yanga wao walikuwa chini ya kocha Mholanzi, Ernie
Brandts akisaidiwa na Fred Felix Minziro.
Mzunguko wa pili timu hizo zilitoka sare ya 1-1,
Simba ikiwa chini ya kocha Mcroatia, Zdravko Logarusic ‘Loga’ akisaidiwa na
Selemani Matola na Yanga ilikuwa chini ya Mholanzi Hans van Der Pluijm
akisaidia na Charles Boniface Mkwasa.
Msimu huu mechi ya mzunguko wa kwanza timu zimetoka
suluhu, Simba wapo chini ya kocha
Mzambia Patrick Phiri akisaidiwa na Matola wakati Yanga inanolewa na Mbrazil
Marcio Maximo akisaidiwa na Mbrazil mwenzake Leonardo Neiva.
0 comments:
Post a Comment