Uwanja wa
Chamazi Complex ambapo Mabingwa watetezi, Azam fc walichuana vikali na mabingwa
wa Tanzania mwaka 1988, Coastal Union ya Tanga.
Mechi hii
ilivuta hisia za mashabiki wengi kwasababu Azam fc waliingia uwanjani wakiwa na
kumbukumbu ya kutandindwa bao 1-0 katika
mechi mbili mfululizo dhidi ya JKT Ruvu Uwanja wa Chamazi na Ndanda fc uwanja
wa Nangwanda Sijaona, Mkoani Mtwara.
Kabla ya
kipyenga kupulizwa kuashiria kuanza kwa
kipute hicho, kiungo mahiri wa Azam fc, Salum Abubakary maarufu kama ‘Sure Boy’
alizawadiwa ‘mkwanja’ wa shilingi milioni moja ikiwa ni zawadi ya mchezaji bora
wa mwezi kutoka kwa wadhamini wa ligi, kampuni ya Vodacom Tanzania.
Kipindi cha
kwanza, Azam fc waiingia kwa kasi wakilisakama lango la wapinzani wao na katika
dakika ya 6, mshambuliaji aliyekosekana katika vipigo viwili, Kipre Herman
Tchetche alipiga shuti kali lililogonga mtambaa panya.
Azam
waliendelea kulisakama lango la Coastal, lakini mlinda mlango mahiri Shaaban
Hassan Kado alijitahidi kuokoa michomo kadhaa ya hatari.
Kipindi cha
pili, Azam waliendelea kushambulia wakisaka bao la kuongoza, lakini mabeki wa
Coastal walijitahidi kupambana.
Dakika ya
55, Wagosi hao wa Kaya walishambulia lango la Azam kama nyuki, lakini kipa
Aishi Salum Manula alifanya kazi ya ziada kuiokoa timu yake.
Timu zote
ziliendelea kushambuliana kwa kasi na katika dakika ya 84 Azam waliandika goli
la kuongoza kupitia kwa Kipre Tchetche.
Dakika tano
baadaye, Shomari Kapombe aliandika bao la pili, lakini dakika za majeruhi, Rama
Salim aliiandikia Coastal bao la kufutia machozi kwa mpira wa adhabu ndogo.
0 comments:
Post a Comment