Na Francis Kivuyo
Ukitaja taasisi zenye nafasi na nguvu kubwa katika jamii,
huwezi kuwacha kutaja Makanisa na Misikiti. Misikiti na Makanisa zimekuwa na
msaada mkuwa sana katika jamii katika kufundisha masuala ya kiroho lakini pia
wakifundisha mambo muhimu ya kijamii ikiwemo maendeleo kama vile; Kilimo, Elimu
pamoja na uongozi bora kwa kutaja
vichache tu.
Kama Misikiti na Makanisa zimefanikiwa kutengeneza na
kuendeleza miradi mikubwa ndani na nje ya nchi; mfano ujenzi wa shule,
mahosipitali na mabenki, basi taasisi hizi zinauwezo mkubwa wa kuchangia kwa
namna moja ama nyingine katika maendeleo ya soka letu.
Kwa mfano; Misikiti na Makanisa zina nafasi nzuri ya kujenga vituo vya soka (football
academy) kubwa na za kisasa kwa ajili ya
kuwajenga vijana wetu kiafya, kimaadili na kuwatengenezea njia nzuri ya ajira
mbeleni kwa kuwa michezo ikiwemo mpira wa miguu ni ajira sasa hivi kwa vijana
wengi. Nasema hivyo kwa sababu, taasisi hizi zinaaminika kuwa na umoja na
ushirikiano mkubwa, wakisema wafanye kitu siyo rahisi kurudi nyuma.
Kwa maana hiyo ni mategemeo yangu kwamba shirikisho la kandanda nchini, TFF chini ya
raisi Jamal Emil Malinzi litalitazama suala hili kwa mtazamo chanya kuona ni
jinsi gani wanaweza wakashirikiana na taasisi zetu za kidini katika
kulisasaidia soka la vijana wetu kwa
maendeleo yetu sisi wenyewe. Hata kama hawataweza kujenga vituo vya soka
lakini, bado wanaweza wakawa wanatia mikono yao katika hiyo program maalumu ya
soka la vijana ambayo ipo chini ya TFF.
Tukifanya hivyo, naamini mpango wa kutengeneza vipaji vya soka kuanzia ngazi ya chini itawezekana tena kwa
mafanikio makubwa na kwa muda mfupi tofauti
na kuwaachia shirikisho peke yao kulifanya.
Tukitumia nchi ya Uingereza kama mfano, kuna timu
zinazoshiriki ligi kuu nchini humo
ambazo chimbuko lao ni makanisani; mfano Everton FC ambayo iliundwa na kanisa
la Methodist la mtakatifu Domingo mwaka 1878 na inajaribu kufanya vizuri katika
ligi mbalimbali za nchini Uingereza. Mfano mwingine ni timu ya Bolton Wanderers
ambayo inamilikiwa na kanisa pia.
Kama hawa wamefanya na wamefanikiwa kwa kiasi hicho, kwa nini sisi tusiweze? Tunaweza sana, kikubwa ni TFF kutengeza mahusiano mazuri na ya karibu na taasisi za kidini ambayo itawafanya kutengeneza mipango kama hiyo ambayo tunaamini itakuwa na msaada mkubwa katika kuendeleza soka letu.
0 comments:
Post a Comment