Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) inaingia kambini kesho (Oktoba 6 mwaka huu) kujiwinda kwa mechi ya Kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) dhidi ya Benin itakayochezwa Oktoba 12 mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager inaingia kambini kwenye hoteli ya Accomondia jijini Dar es Salaam ikiwa na kikosi cha wachezaji 26 walioitwa na Kocha Mart Nooij kwa ajili ya mechi hiyo itakayochezwa kuanzia saa 11 jioni.
Kwa mujibu wa Kocha Nooij, timu hiyo itakuwa na vipindi (sessions) 11 vya mazoezi kabla ya kucheza na Benin (Squirrels). Stars itafanya mazoezi asubuhi na jioni kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa ambapo baadhi yatafanyika Uwanja wa Taifa, na mengine kwenye uwanja mwingine.
Wachezaji Thomas Ulimwengu na Mbwana Samata wanaochezea timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) pamoja na Mwinyi Kazimoto anayechezea timu ya Al Markhiya ya Qatar wanawasili nchini kesho (Oktoba 6 mwaka huu).
Naye mshambuliaji Juma Liuzio anayechezea timu ya Zesco ya Zambia atawasili nchini keshokutwa (Oktoba 7 mwaka huu) kwa ndege ya Kenya Airways akitokea Ndola.
0 comments:
Post a Comment