
Na Baraka Mpenja
MBRAZIL Marcio Maximo amepoteza mechi yake ya
kwanza akiiongoza Yanga baada ya kukubali kipigo ‘swaafi’ kabisa cha mabao 2-0
kutoka kwa Mtibwa Sugar, uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro jioni hii.
Katika mechi hiyo ya kukata na shoka, Mbrazil
mwingine, Geilson Santos Santana ‘Jaja’ naye ameweka rekodi ya kukosa mkwaju wa
kwanza wa penalti akiichezea Yanga katika mechi yake ya kwanza ya ligi kuu.
Mabingwa hao wa 1999 na 2000 wakiongozwa na
mwanafunzi wa zamani wa Maximo, Mecky Mexime, waliandika bao la kuongoza katika
dakika ya 15 kipindi cha kwanza kupitia kwa mshambuliaji wao hatari, Musa
Hassan Mgossi.
Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’
alifanya makosa ya kumsindikiza Mgosi katika eneo la hatari akiamini kipa Deogratius
Munishi ‘Dida’ ataokoa, lakini hakufanikiwa na kumpa nafasi nyota huyo wa
zamani wa Simba kuandika bao kimiani .
Yondan alishindwa kuosha mpira mrefu wa juu kwa
kichwa na kuangukia eneo ambalo si mabeki wala kipa ambaye angeweza kuokoa kiurahisi.
Licha ya Oscar Joshua kuingia kusaidia kuokoa, Mgosi alimchengua Dida aliyetoka
langoni mwake na kufungwa goli hilo.
Wakati wachezaji wa Mtibwa wakishangilia bao hilo,
nyuki walipita uwanjani hapo na kusababisha baadhi ya wachezaji wa timu zote
kulala chini ili kukwepa madhara.
Dakika ya 32 Jaja almanusura aandike bao safi kwa
kichwa akiunganisha kona iliyopigwa na Haruna Niyonzima, lakini mabeki wa
Mtibwa waliondoa mpira katika mstari wa golini na kuwa kona ambayo haikuzaa
matunda.
Kwa ujumla dakika 45 za kipindi cha kwanza sola lilianza
kwa presha kubwa, na kushuhudia timu zote zikicheza mpira wa ‘butu-butu’.
Hata hivyo, Yanga walionekana kufika mara nyingine
golini na kupiga mashuti 5 yaliyolenga goli wakati Mtibwa walipiga 2 tu.
Yanga walionekana kutofanya vizuri sehemu ya
kiungo mpaka pale kocha Marcio Maximo alipoamua kumtoa Oscar Joshua na
kumuingiza Omega Seme.
Mabadiliko hayo yalimlazimisha Mbuyu Twite arudi
sehemu ya ulinzi wa kushoto na kumpisha Seme sehemu ya kiungo. Mabadiliko hayo
yaliwapa nguvu Yanga na kutawala sehemu ya kiungo.
Hata hivyo licha ya kutawala sehemu ya kati na
kumiliki mpira kwa asilimia 52 kwa 48 katika kipindi hicho cha kwanza, Yanga walikosa mipango sehemu ya mwisho na
kukosa nafasi za kufunga.


Sehemu ya ulinzi ya Yanga haikucheza vizuri katika
dakika za kipindi cha kwanza na hii ilichangiwa na sehemu ya kiungo kushindwa
kufanya kazi yake vizuri.
Haruna Niyonzima na Hassan Dilunga hawakuonekana
kucheza mpira wao uliozoeleka na walitawaliwa na viungo wa Mtibwa akiwemo
Mkongwe Shaban Nditi.
Kutokana na Yanga kufa sehemu ya kiungo, Cannavaro
na Yondani walishindwa kutimiza majukumu yao na mara kadhaa kulitokea presha
kubwa langoni mwao.
Yondani alionekana kukosa utulivu na kufanya
baadhi ya faulo ambazo kwa bahati nzuri mwamuzi hakuziona.
Kipindi cha pili, Yanga walianza mpira kwa kasi
wakishambulia kutoka upande wa kulia ambako Mrisho Ngassa alionekana kuwa
hatari zaidi.
Dakika ya 45 Ngassa alipiga krosi kutoka winga hiyo
ya kulia na ukagonga katika mkono wa nahodha wa Mtibwa, Nditi na mpira kumpata
Jaja aliyetia nyavuni, lakini mwamuzi alikataa goli hilo na badala yake kutoa penalti.


Jaja katika dakika 46 alipewa penalti yake ya
kwanza akiichezea Yanga, lakini alikosa baada ya kipa Said Mohamed kuokoa kwa
mguu wake wa kushoto.
Dakika moja baadaye, Yanga walishambulia kwa kasi
na Saimon Msuva aliyeingia kuchukua nafasi ya Hamis Kiiza alitia nyavuni mpira,
lakini mwamuzi msaidizi alikataa bao hilo akidai winga huyo aliotea.
Dakika ya 51 Niyonzima alipiga mpira wa adhabu
ndogo na kuunganishwa kwa njia ya kichwa na Cannavaro, lakini ‘Mchawi’ wa Yanga
leo hii, Kipa Mohamed aliudaka mpira huo.
Dakika ya 61, Niyonzima alipiga mpira mwingine wa
adhabu ndogo uliotua kichwani kwa Jaja , lakini kipa aliokoa kwa mara nyingine.
Jaja aliyepata mipira minne mizuri, alitia kambani
mmoja lakini goli lilikataliwa na mitatu alipiga vichwa vya hatari. Hii
inaonesha mshambuliaji huyo kutoka Brazil ni mtu wa kuchungwa.
Dakika ya 69, Msuva alienda golini kwa Mtibwa na
kutoa mfuko wa ‘Gloves’ za kipa Said Mohamed ingawa haikujulikani ni kwanini.
Kwa tamaduni za soka la Tanzania, inawezekana
Msuva amehisi mfuko ule ndio unawazuia kufunga magoli. Kifupi ni kama imani za
kishirikina.
Dakika ya 82 Amel Ally alipata mpira mrefu na
kusumbuana na Cannavaro akiwa na mwenzake Yondani, akatishia akapiga mpira wa
juu ambapo kipa Dida alipaa juu na kujaribu
kuokoa, lakini ukazama nyavuni na kuiandikia Mtibwa bao la pili.
Goli hilo lilitokana na uzembe wa mabeki wa Yanga
ambapo kwa muda mrefu timu yao ilikuwa ikishambulia na mpira ulipopigwa
hawakuwa tayari kukuabiliana na shambulizi hilo la kushitukiza
Kwa ujumla kipindi cha pili Yanga walitawala mpira
na kufika langoni kwa Mtibwa mara nyingi zaidi, lakini mambo yalikuwa magumu.
Katika kipindi hicho, Yanga walimiliki mpira kwa
asilimia 54 kwa 46, lakini haikuwasaidia kukwepa kipigo hicho kutoka kwa wakata
miwa wa Manungu Turiani.
0 comments:
Post a Comment