Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
0712461976
YANGA SC wanaikaribisha Tanzania Prisons jumapili
(septemba 28 mwaka huu) katika mechi ya raundi ya pili ya ligi kuu soka
Tanzania bara itakayopigwa uwanja wa Taifa, Dar es salaam.
Katika mechi za ufunguzi, Yanga walifungwa 2-0 na
Mtibwa Sugar uwanja wa Jamhuri, Morogoro, wakati Prisons walishinda 2-0 dhidi
ya Ruvu Shootings uwanja wa Mabatini, Pwani.
Kocha wa Yanga, Mbrazil Marcio Maximo baada ya
kufungwa na Mtibwa alisema: “Tulicheza mpira na tukafungwa, lakini ligi ndio
inaanza. Ninachopenda kusema ni kwamba sio vizuri kupoteza matumaini
kwasababu mechi ijayo tutaweza kuimarika na kushinda”
“Tulipoteza nafasi nyingi, mechi ilikuwa ngumu.
Walitumia nafasi zao, sisi hatukutumia nafasi zetu, ni rahisi tu, mpira wa
miguu uko hivyo. Ukipoteza nafasi unahatarisha vitu vingi”
“Kitu cha msingi ni kwamba , kamwe timu
haitakata tamaa , huo ndio mpira, wakati fulani siku inakuwa nzuri na
siku nyingine inakuwa mbaya”.
Yanga hawatakuwa tayari kupoteza mechi ya jumapili
dhidi ya Prisons.
Yanga wamekuwa na historia ya kuwafunga Prisons
uwanja wa Taifa kwa misimu miwili mfululizo, lakini walishindwa kupata matokeo
katika uwanja wa Sokoine, Mbeya.
Yanga dhidi ya Prisons msimu uliopita
Januari 27 mwaka 2013 katika mechi ya mzunguko wa
pili uwanja wa Taifa, Yanga walishinda mabao 3-1 dhidi ya maafande hao wa Jeshi
la Magereza.
Siku hiyo Yanga ikiwa chini ya kocha Mholanzi, Ernie
Brandts ilianza mchezo kwa kasi na ilifanikiwa kufunga goli katika dakika ya 11
kupitia kwa Jerryson Tegete aliyemalizia pasi nzuri ya Saimon Happygod Msuva.
Dakika sita baadaye, mshambuliaji wa Prisons
wakati huo, Elius Maguli (aliyepo Simba sasa hivi) alisawazisha bao hilo
kutokana na uzembe wa mabeki wa Yanga.
Bao la pili lilifungwa na Mbuyu Twite, huku Tegete
akifunga bao la tatu katika dakika ya 66 akimalizia pasi ya Nurdin Bakari.
Wafungaji wa mabao yote manne katika mechi hiyo,
ni Mbuyu Twite pekee ndiye atacheza jumamosi.
Maguli aliondoka Prisons, Tegete anasumbuliwa na
majeruhi. Hata mtoa pasi kwenye moja ya magoli ya Yanga, Nurdin Bakari hayupo.
Msuva bado anatamba Jangwani.
Machi 27 mwaka huu, Yanga iliitandika Prisons
mabao 5-0 katika dimba la Taifa jijini Dar es salaam.
Mabao ya Yanga siku hiyo yalifungwa na Emmuel Okwi
kupitia mpira wa adhabu ndogo, Mrisho Ngassa, Hamis Kiiza (2) na Nadir Haroub ‘Cannavaro’.
Katika wafungaji hao, Okwi pekee hayupo Yanga na
anaichezea Simba msimu huu.
Prisons wamekuwa wakifanya vibaya dhidi ya Yanga
katika uwanja wa Taifa, lakini wakati fulani mpira wa miguu hauheshimu
historia.
Historia ina maana yake katika mpira na ndio maana
hata Yanga hawana historia nzuri na uwanja wa Jamhuri Mkoani Morogoro kama
ilivyo Prisons kwa uwanja wa Taifa.
Lakini mpira umebadilika kwa kiasi kikubwa, timu
inaweza kushinda popote pale. Prisons si watu wa kuwachukulia poa ikizingatiwa
wamebadilika sana kuanzia wachezaji na benchi la ufundi.
Ukimsikiliza kocha wake mkongwe, David Mwamwaja,
utagundu ni mwalimu ambaye anajua anachokifanya.
Jana alizungumza kitu kimoja kwamba, Yanga ni timu
kubwa, wana wachezaji hatari, lakini haiwapi hofu. Wataingia kucheza mpira vile
wawezavyo.
Mwamwaja alisema vijana wake wamejiandaa vizuri na
amekuwa akiwafundisha jinsi ya kukabiliana na nyota wa Yanga.
Ameonekana kumhofia Genilson Santos Santana ‘Jaja’
Mrisho Ngassa, Saimon Msuva na Haruna
Niyonzima ambao walicheza vizuri katika mechi iliyopita mkoani Morogoro.
Kocha wa Prisons, David Mwamwaja (wa kwanza kulia)
Hata hivyo kocha huyo ametahadharisha kuwa mwamuzi
wa mechi hiyo asijekuwa na upendeleo kwa baadhi ya wachezaji kama Jaja. Maana
yake inazungumzia maamuzi ya haki.
Kwa jinsi Yanga walivyocheza na Mtibwa Sugar,
idara zote zilionekana kucheza vizuri achalia mbali makosa makubwa mawili
waliyofanya walinzi wa timu hiyo.
Hassan Dilunga, Haruna Niyonzima, Mrisho Ngassa
walicheza vizuri kuanzia safu ya kiungo na kumpigia mipira kadhaa Jaja
aliyekuwa mshambuliaji wa kati.
Jaja alipata mipira kama minne ya ukweli, mitatu
alipiga vichwa vya hatari na almanusura afunge magoli, lakini moja alifunga
ingawa mwamuzi alikataa na kutoa penalti ambayo ilikoswa na Mbrazil huyo.
Vipindi vyote viwili, Yanga walimiliki mpira
kuliko Mtibwa, lakini wakata miwa hao walitumia mipira mirefu kuwaadhibu Yanga.
Mabao ya Musa Hassan Mgosi na Ame Ali yalitokana
na mipira ya aina hiyo na kwa bahati mbaya Cannavaro na Yondani walikosa
umakini katika eneo lao.
Kwa muda mrefu Yanga walikuwa wanashambulia na
kucheza katika eneo la Mtibwa, hivyo wakawa wanajisahau na kila
waliposhitukizwa kwa mipira mirefu, walishindwa kujipanga na kufungwa kirahisi.
Kocha wa Yanga, Marcio Maximo
Lakini Maximo atakuja kivingine na atalazimika
kucheza kwa kushambulia zaidi ili kupata magoli mengi.
Mbrazil huyu anayependelea zaidi mfumo wa kujaza
viungo wengi, atalazimika kutafuta pointi tatu ili kurudisha hali ya utulivu
Jangwani.
Bado namuona Jaja akifunga siku hiyo. Huyu ni
mchezaji hatari anapopigiwa pasi za krosi na viungo wake au washambuliaji
waliopo nyuma yake.
Kama Prisons watashindwa kumuzuia Mrisho Ngassa na
Saimon Msuva, basi watafungwa mengi kwasababu winga hao wana kasi na wanapiga
krosi sahihi.
Prisons watahitaji kukata mipira yote ya Yanga
kuanzia safu ya kiungo ambapo Haruna Niyonzima ataongoza. Kama wataacha Yanga
wacheze wanavyotaka katika eneo hilo, mvua ya magoli inaweza kuonekana.
Lakini tahadhari kwa Yanga, Prisons ya 3-1, 5-0 si
hii ya David Mwamwaja. Kocha huyu ana historia nzuri na ndio maana alipochukua
timu mzunguko wa pili mwaka jana, alifanya kazi kubwa kuinusuru timu hii.
Wamekuwa na mipango ya kufanya vizuri, wana
wachezaji vijana na morali yao imekuwa
juu hasa baada ya kuanza kwa ushindi ugenini.
Watapambana kwa kila jinsi na kama hawatafungwa
mapema, basi itakuwa rahisi kukabiliana na presha ya Yanga.
Kwa mazingira ya mechi hii, Yanga nawapa asilimia
70 ya kushinda dhidi ya 30 ya Prisons. Tusubiri ya uwanjani!.
0 comments:
Post a Comment