Kikosi cha Yanga kilichoanza dhidi ya Azam fc jana uwanja wa Taifa katika mchezo wa Ngao ya Jamii. Yanga ilishinda 3-0
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
0712461976
AZAM FC wameendelea kuonewa na Yanga katika mechi
za Ngao ya Jamii baada ya jana kufungwa mabao 3-0 na vijana wa Marcio Maximo uwanja wa Taifa
jijini Dar es salaam.
Mwaka jana katika mechi kama hiyo, bao pekee la
Salum Telela liliwapa Yanga ushindi wa 1-0 dhidi vijana hao wenye makazi yao
kule Chamazi.
Mechi ya jana, Azam walitabiriwa kufanya vizuri
zaidi ya Yanga na makocha wa timu hizo, Mcameroon, Joseph Marius Omog (Azam fc)
na Marcio Maximo (Yanga) walianzisha vikosi vifuatavyo:
Young Africans: 1. Deo Munish "Dida", 2.
Juma Abdul, 3.Oscar Joshua, 4. Nadir Haroub "Cananavao" (C), 5.Kelvin
Yondani, 6.Mbuyu Twite, 7.Said Juma "Makapu"/Hassan Dilunga, 8.Haruna
Niyonzima/Hamis Kizza, 9.Geilson Santos "Jaja"/Hussein Javu,
10.Mrisho Ngasa/Omega Seme, 11.Nizar Khalfani/Saimon Msuva/
Azam FC: 1.Mwadini Ali, 2.Shomari Kapombe,
3.Erasto Nyoni/Gadiel Michael, 4.David Mwantika, 5.Agrrey Morrsi, 6.Kipre
Balou, 7.Himid Mao/Kelvin Friday, 8.Salum Abubakar, 9.Didier Kavumbag, 10.Kipre
Tchetche/Ismail Diara, 11.Leonel st.Pres/Khamis Mcha
Ukitazama wachezaji wote wa Yanga na Azam fc wana
ubora wa hali ya juu.
Kabla ya mechi hiyo ya jana, mchana niliongea na
wachezaji wa zamani wa klabu za Simba na Yanga ambao kwa sasa ni makocha na
wachambuzi wa soka.
Moja ya wanandinga hao wa zamani niliopata fursa
ya kuongea nao ni kiungo mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Seklojo Chambua, beki
wa zamani wa Simba, Boniface Pawasa na beki na kiungo wa zamani wa Yanga, Ally
Mayay Tembele.
Kikosi cha Azam fc kilichoanza jana
Chambua
alisema: “Kwangu mimi nafikiri itakuwa mechi
moja nzuri na yenye kusisimua kwasababu ukiangalia timu zote mbili zimejiandaa
vizuri zaidi, zina wachezaji wazuri, zina uwezo wa kifedha, kwahiyo namna
ninavyoiangalia hii, itakuwa ya upinzani sana na itatoa picha ni timu ipi imejiandaa
vizuri kwa ajili ya msimu huu.”
“Azam sasa
hivi imeimarika, ilivyocheza Kagame kila mtu aliona kuwa timu imebadilika,
natarajia mechi ngumu, lakini matokeo yatapatikana ndani ya uwanja na si
nje ya uwanja. Kiujumla itakuwa mechi nzuri sana”.
Kwa upande wa Mayay yeye alisema: ““Mimi nakwenda
kuona nidhamu ya kiufundi kwa upande wa Yanga, kwasababu Azam ukiangalia kwenye
karatasi, safu yao ya ushambuliaji nafikiri ni nzuri kuliko Yanga, lakini
ukiangalia kwenye makaratasi.” Alisema Mayay.
“Ukiangalia mtu kama Kipre Herman Tchetche, uwepo
wa Mhaiti Leonel Saint Prexu pamoja na Didier Kabumbagu ni hatari sana. Hawa ni
washambuliaji watatu wanaoweza kufanya lolote na wakati wowote. Hata kama
mwalimu (Omog) atawapanga wote au wawili, bado safu yao ni nzuri ukilinganisha
na Yanga”.
Pawasa alisema: ““Ni mechi ambayo
huwezi kuitabiri haraka, lakini ukiangalia takwimu na uzoefu, unaweza kuona
Azam wapo katika nafasi nzuri, kwasababu timu yao imeweza kuelewana, juzi juzi
ilikuwa katika mashindano ya Kagame. Kwahiyo tayari Azam imeshapata mfumo kwa
vile mwalimu wao amekuwa na timu kwa muda mrefu.” Alisema Pawasa.
“Wasiwasi ni mabadiliko ya mfumo wa
Yanga, lakini najua Maximo ni mwalimu anayeujua vizuri mpira wa Tanzania,
Maximo ni mwalimu mshindani, kwahiyo naamini ana kikosi kizuri, lakini wasiwasi
wangu ni timu kombinesheni.”
Vitu vya mjomba: Mrisho Ngassa (kushoto) akitafuta namna ya kumtoka Erasto Nyoni (kulia)
Ukiwafuatilia Pawasa, Mayay na
Chambua na watu wengine niliopata nafasi ya kuzungumza nao, waliipa nafasi Azam
kutoa changamoto kubwa, isipokuwa Chambua aliongea kwa tahadhari.
Chambua alikiri kuwa Azam ni wazuri,
lakini hakuwapa nafasi ya kushinda moja kwa moja na alihitaji kusubiri matokeo
ya uwanjani.
Wengine kwa asilimia kubwa waliamini Azam
fc ilikuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kushinda kuliko Yanga.
Hoja yao ya msingi ni jinsi Azam fc walivyokaa
pamoja kwa muda mrefu. Kumbuka kocha Joseph Omog alikuja nchini baada ya
kumalizika kwa mzunguko wa kwanza wa ligi kuu mwaka jana akirithi mikoba ya
Muingereza aliyeachia ngazi, Stewart John Hall.
Mcameroon huyu amekuwa na timu kwa
muda mrefu zaidi ya Marcio Maximo aliyetua nchini mwishoni mwa mwezi wa sita
mwaka huu.
Kutokana na namna Omog alivyoiandaa
timu yake kwa muda mrefu, akashiriki kombe la Kagame na kucheza vizuri, ingawa
aliishia robo fainali, watu wengi waliamini timu yake ingefanya vizuri.
Wengi waliitazama Yanga dhidi ya
Thika United, kiukweli haikucheza vizuri. Wengine waliiona ikicheza mechi za
kawaida pale Loyola, wakadhani haina kitu.
Ngassa na Nyoni mambo yalipamba moto
Lakini jana walikuja kivingine, timu
ilionekana kuwa imara kuanzia nyuma, kati mpaka mbele.
Walicheza kwa kuelewana, hawakuwa na presha,
walijilinda vizuri, walidhibiti katikati, wakapanga mashambulizi na kupata
mabao matatu.
Yanga walistahili kushinda kwasababu
kimbinu na kiufundi walikuwa wazuri zaidi ya Azam fc, lakini haimaanishi wana
Lambalamba ni wabaya.
Usijaribu kuwabeza Azam fc kwasababu
wamefungwa na Yanga. Kuna mambo mengi hutokea katika mpira.
Kama unakumbuka, Azam walicheza
vizuri kipindi cha kwanza, walishambulia mara kadhaa, lakini washambuliaji
wake, Didier Kavumbagu, Kipre Herman Tchetche, Leonel Saint-Prexu walishindwa
kutumia nafasi.
Baada ya kufungwa bao la kwanza
dakika ya 58 na Jaja, wachezaji wa Azam walionekana kuchanganyikiwa kwa kiasi fulani.
Pengine hawakuwa na utayari wa kufungwa katika mechi yao kutokana na maandalizi
waliyofanya.
Unapokwenda kwenye mechi ni lazima
ujue kuna kufunga na kufungwa, lakini ukiingia na akili ya kufunga na
ukafungwa, basi unakosa utayari wa kupokea matokeo na hatimaye unaweza kutoka
katika mfumo wa uchezaji.
Azam walishindwa kujipanga kabisa
pale walipofungwa bao la pili dakika ya 66. Timu ilionekana kutokuwa na mipango
na hapo ndipo Yanga walionekana kuwa bora zaidi.
Lakini kiuhalisia, Azam bado wana
kikosi kizuri na ni timu inayokubali changamoto.
Azam huwa hawakati tamaa, mara zote
wanakubali kimpira na ndio maana kama uliwasikia viongozi wake jana, walisifu
kiwango cha Yanga na kuwapa hongera kwa ushindi.
Timu hii ipo kimpira kama vile Marcio
Maximo alivyo kimpira. Kabla ya mechi kocha huyu wa Brazil aliwasifu Azam na
kusema anawaheshimu, hivyo ataingia kwa tahadhari kubwa.
Maximo hana tabia za Kiswahili za
‘ooooh! Azam hawatoki au Simba hawatoki, tutawageuza Azam kitoweo cha krismas’,
Yeye anazungumza ‘football’.
Mwaka jana Yanga iliwafunga katika
mechi ya Ngao ya Jamii, lakini wakawafunga Yanga 3-2 katika mechi ya mzunguko
wa kwanza wa ligi kuu na mechi ya mzunguko wa pili wakalazimisha sare ya 1-1.
Bahati mbaya Azam wakawazidi kete
kwenye mbio za ubingwa. Kuwashinda iwe changamoto ya kujipanga zaidi kwasababu
Omog anawarudisha vijana darasani.
Jumatatu njema!
0 comments:
Post a Comment