Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
MBEYA City fc imepata pigo baada ya wachezaji wake
watatu kuumia katika mechi ya jumamosi iliyopita dhidi ya JKT Ruvu iliyomalizika kwa suluhu ya bila kufungana,
uwanja wa Sokoine, Mbeya, na watakaa nje ya uwanja kwa wiki mbili.
Afisa habari wa klabu hiyo, Dismas Ten ameiambia
MPENJA BLOG mchana huo kuwa baada ya mechi iliyopita, wachezaji watano walipata
majeruhi, lakini wawili kati yao watarejea uwanjani jumamosi ya septemba 27 kuchuana
na Coastal Union.
“Kwanza nianze na majeruhi; baada ya mechi
kumalizika jumamosi iliyopita, kuna wachezaji wetu watano walipata majeraha,
lakini wawili kati yao watarejea jumamosi ijayo kucheza dhidi ya Coastal Union kwasababu
maumivu yao hayakuwa makubwa sana. Wachezaji hao ni beki Deogratius Julius ‘Musafwa
wa Kweli’ na kiungo mahiri, Steven Mazanda.” Alisema Dismas.
“Wachezaji wengine watatu kwa maana ya John
Kabanda, Alex Seth na Eric Mawala, hawataweza kucheza kabisa siku ya jumamosi
kwasababu watakaa nje kwa majuma mawili, kwa mujibu wa daktari wetu.”
Dismas aliongeza kuwa maandalizi ya mechi ya pili
nyumbani yanakwenda vizuri na wachezaji wana morali ya kutafuta ushindi na
kuendeleza rekodi yao ya msimu uliopita ambapo walimaliza katika nafasi ya tatu
nyuma ya Yanga na mabingwa Azam fc.
“Hali ya kambi ni nzuri, tunajiandaa vizuri na
tunaamini tutaibuka na ushindi. Tulicheza mpira mkubwa sana dhidi ya JKT Ruvu,
sema wakati mwingine demokrasia ya mpira wa miguu inabidi tukubaliane nayo”
“Kuna kushinda, kushindwa na kutoa sare, lakini
mwisho wa siku tulicheza mpira mzuri na watu waliokuwepo uwanjani waliridhika
na kiwango cha timu”
“Tunataka kulipa kisasi, Coastal walitufunga na
kutuharibia rekodi yetu. Tunataka kuonesha kwamba kutufunga kwao sio kwamba
tulikuwa chini ya kiwango bali walitubahatisha tu”
0 comments:
Post a Comment