Maximo (kushoto) alifurahia ushindi wa 2-1 dhidi ya Prisons jana uwanja wa Taifa
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
KOCHA mkuu wa Yanga, Mbrazil, Marcio Maximo kwa
mara ya pili alikutana na kocha Mzawa katika michuano ya ligi kuu soka Tanzania
bara.
Ikitokea nchi ya mbali (Brazil) ambayo hunukia harufu
ya soka kila kona, Maximo alitandikwa 2-0 uwanja wa Jamhuri, Morogoro na Mtoto
wa Kitanzania, Mecky Mexime , kocha wa Mtibwa Sugar.
Jana akakutana na Mtanzania mwingine, David
Mwamwaja, kocha wa Tanzania Prisons na kufanikiwa kushinda 2-1.
Katika mechi zote hizo mbili, maarifa ya Maximo
yalionekana kuelekeana na pengine kuzidiwa kwa kiasi kikubwa na ya wazawa.
Kama Prisons wangekuwa makini safu ya ushambuliaji
na kuongeza nidhamu ya ulinzi, dhahiri walikuwa wanamharibia siku Maximo.
Lakini kocha huyu aliyewahi kuifundisha timu ya
Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, kati ya 2006 na 2010 ameendelea kuzungumza
mpira na sio unazi kila baada ya mechi.
Hajisifu hata kidogo, pale anapokosea anakiri
waziwazi na kuahidi kujipanga zaidi.
Alipofungwa Morogoro aliwasifu Mtibwa kwa kucheza
vizuri, akaisifu timu yake kwa kucheza vizuri ingawa ilifanya makosa sehemu ya
ushambuliaji na safu ya ulinzi.
Alisema hakuna haja ya kukata tamaa, mpira ndivyo
ulivyo, ligi ndio inaanza, lakini akaahidi kuwa mechi ijayo (ya jana dhidi ya
Prisons) timu itaimarika zaidi.
Katika mechi hiyo, Yanga walionesha kubadilika,
lakini safu ya ulinzi iliendelea kuwa na makosa mengi.
Lakini Maximo hajakata tamaa, anajiona kuwa ana
nafasi ya kuboresha zaidi eneo hilo.
Baada ya mechi, Mtandao huu uliinasa kauli ya
Maximo kwa umakini kabisa akisema: “Lakini tunatakiwa kukaa chini na
kujiboresha kiukweli, wachezaji wanakuja-kuja, baada ya wiki moja watakuwa
wazuri zaidi. Tuna wiki moja ya maandalizi kabla ya mechi, tutafanya mazoezi
zaidi na tutakuwa imara zaidi mechi ijayo”.
Kwa upande wa Kocha wa Prisons, David Mwamwaja,
hali ilikuwa tofauti. Alimlalamikia mwamuzi, Andrew Shamba akidai aliipa
mbeleko Yanga.
Mwamwaja alisema: “Kiujumla vijana walijituma na
kuonesha uwezo mkubwa wakiwa wachache. Nina masikitiko kwasababu waamuzi
hawakunitendea haki. Wale wachezaji wa Yanga walishika mpira mara tatu ndani ya
penalti boksi, lakini hawakupewa adhabu yoyote”
“Hii mechi ingekuwa tofauti kama wangetoa haki.
Mimi najali uwezo wa vijana. Mchezaji wangu alioneshwa kadi nyekundu (Jacob
Mwalobo), lakini ilikuwa sio. Tutajitahidi zaidi mechi ijayo”.
0 comments:
Post a Comment