SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) septemba 19 mwaka huu lilitangaza kupokea kwa masikitiko makubwa taarifa
zilizoandikwa kwenye baadhi ya Vyombo vya Habari zikielezea tuhuma za hujuma
kwa timu ya Taifa (Taifa Stars) katika mechi za kufuzu mashindano ya AFCON.
Taarifa hiyo ilifafanua kuwa TFF
pamoja na kutokuwa na uthibitisho wa tuhuma hizi nzito haliwezi kuzikalia kimya
na litateua jopo la kuchunguza.
TFF alieleza kuwa wanafamilia wa mpira
wa miguu Tanzania (Members of TFF Family) watakaohitajika kuhojiwa na jopo hilo
kwa mujibu wa Ibara ya 37 ya Kanuni za Maadili za TFF watalazimika kutoa
ushirikiano. Atakayeshindwa kutoa ushirikiano atachukuliwa hatua za kimaadili.
Pia wadau wa mpira wa miguu
ambao sio wanafamilia wa TFF, watakaoitwa na jopo hili wanaombwa watoe
ushirikiano kwa nia ya kujenga mpira wetu.
Kufanya vibaya kwa timu ya taifa, TFF
wasitafute watu wa kuwabebesha lawama kutokana na mambo ya kimjini
tuliyoyazoea.
Kwasisi ambao ni wakazi wa Dar es
salaam kuna mambo mengi yanazungumzwa, lakini haya ni maneno tu kwa ajili ya
kusherehesha vikao, vijiwe vya kahawa na majungu.
Sababu kubwa ya mambo haya kuzungumzwa
ni matatizo yanayolikabili soka la nchi hii. Tukubali tukatae, kadri siku
zinavyokwenda mbele, mpira wa Tanzania unazidi kudidimia kila kukicha.
Jumamosi iliyopita katika mechi ya ufunguzi
wa ligi kuu soka Tanzania bara baina ya Mtibwa Sugar dhidi ya Yanga iliyopigwa
uwanja wa Jamhuri Morogoro, Wanajangwani walikufa 2-0.
Yanga ilikuwa na wachezaji sita wa
timu ya Taifa ambao ni Deogratius Munishi ‘Dida’, Oscar Joshua, Kelvin Yondani,
Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Mrisho Ngassa na Saimon Msuva pamoja na wachezaji
wanne wa kimataifa ambao ni Mbuyu Twite Jr, Geilson Santos Santana ‘Jaja’ ,
Haruna Niyonzima na Hamis Kiiza.
Yanga ikiwa na wachezaji sita wa timu
ya Taifa na wanne wa kimataifa alicheza dhidi ya Mtibwa Sugar ambayo haina hata
mchezaji mmoja wa timu ya Taifa wala wa kimataifa na ikaambulia kipigo hicho.
Miaka ya 1980 wakati wengi wetu walikuwa
wanazaliwa na wengine wanakua mpira ulikuwa unachezwa kwa kiwango cha juu,
lakini kutokana na teknolojia kutokuwa rafiki miaka hiyo, tumejikuta
tukihadithiwa tu na hakuna DVD za kuona matukio ya zamani.
Tumehadithiwa na wazee wetu na kusoma vitabu
vilivyotangulia. Nakumbuka nilipata nafasi ya kukaa na mzee mmoja wa Morogoro,
Mohamed Msomari ambaye alikuwa mchezaji wa zamani wa Cosmo, kocha aliyeingoza Pan
Africa kuchukua ubingwa mwaka 1982 na kocha timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa
Stars.
Huyu ndiye kocha aliyeibua kipaji cha
mchezaji hatari wa wakati ule, Zamoyoni Mogela.
Msomari aliniambia kwamba katika miaka
ya 1980, timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars iliifunga timu ya Taifa ya
Kenya, Harambee Stars mabao 5-0.
Kikosi hicho cha Stars kilikuwa na
wachezaji wawili tu kutoka Simba na wawili kutoka Yanga tofauti na ilivyo sasa
hivi.
Rais wa TFF, Jamal Malinzi
Timu ya wakati ule, mchango wa wachezaji wa Simba na Yanga ulikuwa mdogo mno na wengi walitoka timu za madaraja ya chini. Kwa mfano; Leopard Taso Mukebezi alikuwa anacheza timu ya Balimi ya Bukoba iliyokuwa daraja la pili. Kiungo Idrissa Ngulungu alitoka Tumbaku ya Morogoro, Peter Tino kutoka African Sport ya Tanga, Leodigar Chila Tenga, Jela Mtagwa, Adolf Rishard walitoka Pan Africa.
Timu ya wakati ule, mchango wa wachezaji wa Simba na Yanga ulikuwa mdogo mno na wengi walitoka timu za madaraja ya chini. Kwa mfano; Leopard Taso Mukebezi alikuwa anacheza timu ya Balimi ya Bukoba iliyokuwa daraja la pili. Kiungo Idrissa Ngulungu alitoka Tumbaku ya Morogoro, Peter Tino kutoka African Sport ya Tanga, Leodigar Chila Tenga, Jela Mtagwa, Adolf Rishard walitoka Pan Africa.
Miaka hiyo ya 80 Simba ilikuwa moto wa
kuotea mbali, ilikuwa ni kali kwelikweli ikiwa na wachezaji kama Nico Njohole,
Abdallah Mwinyimkuu maarufu kama British, Mohamed Tall, Ezekiel Greyson ‘Juju
Man’, Jumanne Hassan Masimenti.
Wachezaji hawa pamoja na ukali wao na
kuichezea Simba ambayo ilikuwa kwenye kiwango cha hatari na Taifa Stars ikiitandika
Kenya 5-0, hawakupata nafasi ya kuitwa, licha ya kwamba waliwahi kuichezea siku
za nyuma.
Nafasi zilichukuliwa na wachezaji
kutoka timu hadi za madaraja ya pili kutoka mikoani. Maana yake kulikuwa na
ushindani mkubwa, wachezaji walikuwa wengi na haikuwa rahisi kuteuliwa Taifa
Stars.
Leo hatuoni wachezaji kutoka kila kona
ya Tanzania. Kuna tatizo sehemu fulani na hapo ndipo tunatakiwa kutumia muda
mwingi kutafuta sababu na suluhisho
sahihi.
Kwa mfano ligi iliyoanza mwishoni mwa
wiki iliyopita ndio moja kati ya kaburi la timu ya Taifa ya Tanzania.
Haizalishi wachezaji wa kutosha, haina ushindani na kwa maana hiyo ni ndoto
kuwa na Taifa Stars bora.
Badala ya Rais wa TFF, Jamal Emil
Malinzi kupoteza muda kutafuta watu wanaoihujumu timu ya Taifa, inatakiwa
apoteze muda mwingi kutafuta muundo bora na chombo huru cha kuendesha ligi
katika uweledi wa hali ya juu.
Ligi ikishakuwa bora na ushindani kuwa
mkubwa, itasababisha kujenga wigo mpana wa kuchagua wachezaji wa timu ya Taifa.
Kwa kifupi, ligi yetu ni mbovu,
haivutii, haitoi wachezaji bora, sasa tujiulize, tutapata wapi timu ya Taifa
iliyo bora?
Kuchunguza hujuma kwa Taifa Stars
inayofanya vibaya hakuna maana, lazima tukubali kuwa hatuna mfumo wa kuzalisha
wachezaji ambao wako tayari kushindana na wachezaji wa mataifa mengine.
Nimeeleza kuwa zamani walikuwa
wanateuliwa wachezaji kutoka daraja la pili kuliko wanaocheza Simba na Yanga.
Sababu ni kwamba mpira ulikuwa unachezwa mno na wachezaji walikuwa wengi
mchangani.
Siku hizi hakuna wachezaji kabisa, na
ndio maana unakuta wachezaji wengi wa timu ya Taifa wanatoka klabu za Simba, Yanga
na sasa hivi Azam fc.
Siku hizi mashabiki wanakwenda
uwanjani kupoteza muda, kubadili fikra, kuonana na watu tofauti waliopoteana
kwa muda mrefu. Ladha ya mpira haipo uwanjani, na watu wanaenda kwa mazoea tu.
Suluhisho ni kurudi nyuma, kukaa
pamoja na kuunda mpango mkakati wa kitaifa ili kuboresha soka letu kuanzia
ngazi za chini mpaka juu.
Utengenezwe mfumo wa kuibua, kulea na
kukuza vipaji kuanzia ngazi ya chini ili kupata wachezaji wengi wa timu Taifa
kama ilivyokuwa miaka ya 1980.
TFF itafute njia za kuboresha ligi kuu
na kuunda chombo bora cha kusimamia na kusiwepo kubebana wala kuoneana aibu. Vinginevyo
hatutafanikiwa hata siku moja na tutaendelea kutiana moyo, kushikana uchawi na
kuwekeana ahadi hewa.
Tatizo la Taifa stars sio kuhujumiwa,
ni kukosa njia sahihi ya kutafuta wachezaji na sababu ni ubovu wa ligi, haina
uwezo wa kutupatia vipaji mbalimbali.
Chanzo: shaffihdauda.com
0 comments:
Post a Comment