Edo akishangilia moja ya goli alilofunga akichezea Simba sc
Na Baraka Mbolembole
Akitokea benchi, mshambulizi Edward Christopher
aliisaidia Simba SC kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Ruvu Shooting.
Ilikuwa ni Septemba 24 wakati kocha Milovan
Circovic alipomuingiza uwanjani kijana wa miaka 20 ( wakati huo).
Christopher
alikuwa ametoka kushinda tuzo binafsi ya ufungaji bora katika michuano ya ABC
Super8, mwezi mmoja nyuma huku akiisaidia klabu yake kutwaa ubingwa huo kwa
kuilaza Mtibwa Sugar kwa mabao 5-3 katika fainali ambayo kabla ya mechi
mchezaji huyo alimuahidi golikipa
Shaaban Kado wa Mtibwa kuwa atamfunga ‘ hat-trick’, na kweli akafanya hivyo.
Mara baada ya michuano hiyo Christopher
alitabiriwa kama mmoja wa wachezaji bora vijana nchini Tanzania ambao watafanya
mambo makubwa. Ilikuwa ni ndoto iliyotimia kwa mchezaji huyo kupangwa katika
kikosi cha kwanza cha Simba katika pambano dhidi ya mahasimu wao Yanga SC,
Jumatano ya Oktoba 3, 2012 katika mchezo wa ligi kuu Tanzania Bara msimu wa
2012/13.
Akiwa kinda wa miaka 20, Milovan alikunwa na
kipaji cha kukotota mpira cha mchezaji huyo, umaliziaji wake wa kiwango cha juu
na namna alivyo na maarifa ya kupasua ngome za timu pinzani.
Mbele ya mashabiki ‘ lukuki’ katika uwanja wa
Taifa, Simba na Yanga zilicheza kandanda safi. Amri Kiemba alifunga bao safi la
mkwaju wa mbali nje kidogo ya eneo la mita 18 akiunganisha moja kwa moja krosi
iliyopigwa na Mwinyi Kazimoto kutoka wingi ya kulia.
Said Bahanunzi alikuja kufunga bao la kusawazisha
kwa mkwaju wa penalti mwishoni wa kipindi cha pili na kutengeneza sare ya
kufunga bao 1-1. Ilikuwa ni moja ya mechi zilizojaza watazamaji wengi katika
uwanja huo, huku timu zote zikicheza soka la kushambulia na nguvu.
Yanga walikuwa wametoka kufungwa mabao 5-0 katika
mchezo wa mwisho wa ligi kuu, iliingia kucheza na Simba ikiwa na ubingwa wa
Kagame Cup, huku usajili wao wa mlinzi Mbuyu Twite ukiwa mchungu kwa Simba.
Ilikuwa
mechi ya Christopher, alimsumbua vilivyo
mchezaji huyo wa Kimataifa wa Rwanda. Edo alikuwa akitokea pembeni ya uwanja
upande wa kushoto jukumu ambalo lilimfanya kuwa tishio kwa Mbuyu kila alipokuwa
na mpira.
Mbuyu alimpiga sana viatu kijana huyo ambaye
alivumilia na kuendelea kuwasumbua walinzi wa Yanga na kuwa tishio langoni mwao.
Kasi ya kijana huyo ilikuwa juu mno na kufanya Simba kushambulia muda wote
ambao alikuwepo uwanjani kabla ya kuumizwa na Mbuyu.
Mchezaji huo aliuguza majeraha yake lakini kila
aliporudi uwanjani aliendelea kusumbuliwa na maumivu. Simba ilimvumilia kwa
muda wote na kufikiri kuwa mchezaji ataimarika na kurejesha kiwango chake
lakini aliishia kugombana na Walimu, Jamhuri Kiwelo na Abdallah King Kibadeni msimu
uliopita, hata alipokuja Zdravko Logarusic
bado mchezaji huyo alitajwa kama mmoja wa wachezaji ambao wanacheza kwa viwango
vya chini katika timu hiyo. Alirudishwa benchi na Loga na baadaye mwalimu huyo
raia wa Croatia alipendekeza mchezaji huyo aachwe.
Christipher aligoma kuuzwa kwa mkataba wa mkopo
hivyo alikwenda katika timu ya Mtibwa Sugar kujifua wakati akisikilizia ni wapi
hasa anaweza kucheza na kuendeleza kipaji chake. Mwalimu Adolf Richard
alimsaini mchezaji huyo kwa mkataba wa mwaka mmoja katika kikosi cha Polisi
Morogoro.
Ikiwa
tayari imepoteza mchezo wa kwanza mbele ya Azam FC wiki iliyopita, Polisi
itacheza mchezo wa pili mfululizo ikiwa katika jiji la Dar es Salaam, na
Jumamosi hii watacheza na moja ya timu yenye uhasama nayo kwa muda mrefu ndani
ya uwanja.
Polisi imekuwa ‘ nyanya’ katika uwanja wa Taifa
mbele ya Simba lakini mabingwa hao mara 19 wa kihistoria wamekuwa na wakati
mgumu kila wanapotua katika uwanja wa Jamhuri, Morogoro.
Ukitoa
uwepo wa Christopher, Adolf atakuwa na wachezaji wengi wa kujivunia katika
mchezo huo kama nahodha, Nahoda Bakari, Lulanga Mapunda, Danny Mrwanda na nyota
wengine wengi. Simba SC v Polisi
Morogoro hii ni nafasi pekee ya ‘ Edo Boy’ kuwakumbusha watu kuhusu kipaji chake
akiwa na miaka 22 hivi sasa.
Je, Christopher atafunga katika mchezo wa kesho?.
Inawezekana kwa sababu tayari safu ya ulinzi ya Simba imeruhusu mabao mawili katika
mchezo wa kwanza, huku Polisi wakiwa tayari wamefunga bao moja katika uwanja wa
Azam Complex Chamanzi. Simba watamchunga sana Christopher sababu wanamfahamu
lakini atawafunga wakijisahau kidogo tu.
0714 08 43 08
0 comments:
Post a Comment