Monday, September 22, 2014

SIMBA SC chini ya kocha Mzambia Patrick Phiri wamehitimisha raundi ya kwanza ya ligi kuu soka Tanzania bara iliyoanza septemba 20 mwaka huu kwa kutoka sare ya 2-2 dhidi ya Wagosi wa Kaya, Coastal Union katika mechi yao ya ufunguzi iliyopigwa jana uwanja wa Taifa, Dar es salaam.

Mbali na kipute hicho, jumamosi (septemba 20 mwaka huu), kulikuwa na mechi sita ambazo zilileta matokeo yasiyotarajiwa kwa baadhi ya timu.

Wakiongozwa na kocha Mbrazil, Marcio Maximo katika mechi ya kwanza ya ligi kuu, Yanga walitandikwa 2-0 na Mtibwa Sugar, uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro.

Mabingwa watetezi, Azam fc walishinda 3-1 dhidi ya Polisi Morogoro, wakati washindi wa tatu msimu uliopita, Mbeya City fc wakiwa nyumbani Sokoine waliambua suluhu pacha ya bila kufungana (0-0) mbele ya JKT Ruvu kutoka Pwani.

Mgambo JKT waliifunga Kagera Sugar 1-0 katika uwanja wa Mkwakwani Tanga. Ruvu Shootings wakiwa nyumbani kwao mabatini walifungwa 2-0 na Tanzania Prisons.

Stand United wakiwa kwao Kambarage mkoani Shinyanga, walikula kipigo cha 4-1 kutoka kwa Ndanda fc.

Kama nilivyosema awali, Simba ndio walihitimisha raundi ya kwanza hapo jana na leo hii napenda kuuzungumzia kwa kina mchezo huo.

Kwanza kabisa, Simba washukuru kupata pointi moja kwasababu walicheza hovyo kama timu na kwa mchezaji mmoja mmoja.

Nitawaelezea baadhi ya wachezaji wao nyota ambao ni Paul Kiongera, Piere Kwizera, Ramadhani Singano ‘Messi’, Shaaban Kisiga ‘Malone’ , Emmanuel Okwi na Amissi Tambwe.

Kiukweli, wachezaji wote wa mbele hawakufanya vizuri na ndio maana safu ya ulinzi ya Simba inaonekana mbovu.

Kitaalamu, timu inajengwa kutoka nyuma, maana yake ni kwamba kila mtu anatakiwa kutekeleza majukumu yake kwa nafasi yake.

Ili uweze kupata ubora wa safu ya ulinzi, ni pale idara nyingine zinapotekeleza majukumu yao ipasavyo. Simba kuanzia idara yao ya kiungo mpaka ushambuliaji, wako hovyo kupita maelezo.

Kwa leo tuzungumzie matatizo ya Simba kuanzia safu ya kiungo na Ushambuliaji ambayo chanzo chake ni kusajili hovyo hovyo, bila kufuata utaratibu na mwisho wake wanajikuta wana wachezaji wengi kwenye nafasi moja au wana wachezaji wengi wenye majukumu yanayofanana.

Kwahiyo wamejikuta hawana namna zaidi ya kuwatumia wachezaji wanaofanana, yaani ni kama sare tu. Mfano; wewe una mashati 10 na mashati 8 yote ni mekundu, ukivaa yale yale kwa mfululizo, hutaonekana umebadilisha nguo, bali umevaa nguo ile ile.

Kocha mkuu wa Simba sc, Patrick Phiri

Tukianza na wachezaji waliocheza jana kwenye safu ya kiungo;


PIERE KWIZERA

Ni mchezaji mzuri, lakini hana maamuzi ya haraka. Yuko pole pole kwenye baadhi ya ‘Movement’. Kuna wakati yeye ndiye anatakiwa Kuanzisha ‘movement’ za haraka kwenda kwenye goli la mpinzani, lakini anakosa  maamuzi sahihi kwa muda muafaka, pamoja na kwamba hapotezi pasi.

Kutopoteza pasi sio kigezo. Ni mara mia upoteze pasi nne kati ya sita ambazo zilitakiwa kufika katika eneo sahihi, kuliko kutopoteza pasi nne kati ya nne ambazo hazina faida yoyote wala madhara yoyote.

 Maana yangu ni kwamba kama ulitaka kupiga pasi katika eneo sahihi ukakosea, ule mpira bado utakuwa katika eneo lile lile la hatari na mtu mwingine anaweza kuupitia na kusababisha madhara. Hii ina faida kuliko kupiga pasi ambayo haina madhara yoyote.

Uwezo wa Kwizera kufanya maamuzi ni mbovu kabisa. Sijawahi kumuona akicheza huko nyuma zaidi ya kumuona Simba, labda hiyo sio nafasi yake sahihi. Nijitolee mfano mimi mwenyewe Shaffih Dauda.

Mwaka 2002 nakumbuka Simba ilikuwa inatafuta wachezaji wa kusajili pale nje ya uwanja wa Taifa ambapo sahizi pana uwanja mpya wa Taifa.

Walikuja wachezaji wengi mno kufanya majaribo na mimi nilienda. Lakini kwenye nafasi yangu ya kiungo nikakutana na mtu mmoja anaitwa Salim Lyandungu, Yahya Akilimali, William John,  Mpandachi na Joel Noel.

Nikagundua kuwa ushindani ni mkubwa, lakini kwenye safu ya ulinzi kulikuwa na wachezaji wachache akiwemo Patrick Betweli, Aman Mbarouk, Benito John na Chacha Marwa. Na mimi nikajifanya beki kwasababu ilikuwa ni rahisi katika nafasi ile. Ulikuwa unapata nafasi ya kucheza kwa muda mwingi kuliko nafasi ya ushambuliaji au kiungo ambayo walikuwepo watu wengi sana.

Katika mchujo huo, Benito John na Chacha Marwa hawakufanikiwa, wakati mimi, Patrick Betweli na Aman Mbarouk tulifuzu majaribo.

Mimi na Mbarouk tulisajiliwa siku moja katika klabu ya Simba mwaka 2003 na Rais wa Simba wa sasa, Evens Elieza Aveva ndiye alitusainisha fomu katika Hoteli ya Embassy ambako alikuwa anafanya kazi zamani .

Nilipata nafasi ya kucheza Simba kama beki wakati mimi nilikuwa kiungo na baadaye nilipopata nafasi, nikataka kucheza nafasi yangu.


Lakini kwa bahati mbaya sikuendelea kucheza mpira wa ushindani kutokna na sababu zilikuwa nje ya uwezo wangu na badala yake nikajikita katika masomo.

Nini maana ya mfano huu? Kwizera mimi siwezi kumlaumu, inawezekana baada ya kuja Simba ndio nafasi iliyopata, yawezekana kuna nafasi nyingine ambayo anacheza vizuri zaidi. Kwasababu hakuna mtu aliyemuona kabla, anajikuta anajaribiwa.

SHAABAN KISIGA ‘MALONE’.

Kisiga ni namba 10 na sio namba 8. Ili upate kiwango cha Kisiga ni pale anapocheza kama mshambuliaji, yaani wacheze washambuliaji wawili au acheze nyuma ya mshambuliaji, kwa mfano acheze na Tambwe au nyuma ya Tambwe.

Kwa vile Simba kwenye idara ya ushambuliaji wana Tambwe, Emmanuel Okwi na Paul Kiongera, Kisiga anarudishwa kucheza namba 8. Eneo ambalo hawezi kucheza vizuri kama anavyocheza namba 10.

Simba wanashindwa kupata kiwango bora cha Kisiga kwasababu anacheza eneo ambalo hachezi vizuri. Inatokea hivi kwa sababau lile eneo analotakiwa kucheza yeye kuna wachezaji wengine, hivyo amembidi atafute eneo lingine la kucheza na hatimaye kupata namba 8 ingawa sio eneo lake sahihi.

Kwa mfano jana kwenye mechi, Kisiga alikuwa anapiga pasi vizuri, lakini hakuwa na kasi, alikuwa polepole sana, hakupiga zile ‘killer pass’ na sababu kubwa ni kutocheza katika eneo lake.

Messi (kushoto) akifanya mambo yake

RAMADHANI SINGANO ‘MESSI’.

Labda jina la Messi linamharibia. Kila mpira yeye anataka awatie watu njaa, akokote vile anavyotaka. Hata Lionel Messi mwenyewe wa Barcelona, kuna mipira mingine anapiga pasi moja na huwa hakimbizi kwasababu anahofia kuchoka.

Uwepo wa Singano uwanjani una faida kwa dakika chache kwasababu muda mwingi unataka kila mpira unaoenda kwakwe akimbize, na akishapoteza hawezi kukaba, hawezi kurudi kuisaidia timu kujilinda na matokeo yake anaigharimu.

Ili  Singano aweze kuisaidia timu, sio kila mpira ukienda kwake aburuze. Wakati fulani aachie pasi moja moja na akifanya hivyo atampa mtu mwingine nafasi ya kucheza vizuri na yeye mwenyewe hatachoka.

PAUL KIONGERA

 Simba wamemsajili mchezaji mwenye pancha mwili mzima. Ana majeruhi ya goti na hapa ndipo unapata madhara ya kujisajiliwa hovyo hovyo tu.

 Mchezaji katoka huko, hamjui historia yake, mnamsajili kishabiki tu kwaajili ya kuwahi siku ya mwisho ya usajili ‘Deadline’. Matokeo yake mnapata mchezaji mwenye majeruhi. Mimi nimemfuatilia katika mechi za Simba, mchezaji  huyu ana jeraha ambalo hawezi kupona leo wala kesho.

Kama unabisha,  baada ya kuumia katika mechi ya jana, ukiangalia lugha ya mwili ‘Body language’, yule mchezaji ana majeraha na Simba wamemsajili akiwa na majeraha.

Wazungu sio wajinga wanapofanya vipimo vya afya, wanataka kujua kama mchezaji ni mzima. Simba wangekuwa makini wasingesajili mchezaji mwenye pancha. Hapa wamepata hasara na hatakuja kuitumikia timu vile inavyotakiwa.

EMMANUEL ANORD OKWI

Huyu ndiye mchezaji aliyecheza chini ya kiwango mno licha ya kutoa pasi moja iliyozaa goli alilofunga Tambwe.

Okwi (kulia) akimtoka beki wa Coastal Union

Okwi amekwisha, huo ndio ukweli, labda inabidi awe na mazoezi maalumu “Special Training’ kwaajili ya kurudisha kiwango chake. Yaani Okwi yule wa 5-0 na yule wa Setif, sio huyu wa sasa hivi.

Simba walijua fika kuwa mchezaji huyu alikuwa hachezi, alikuwa kwenye matatizo na klabu yake. Wamekurupuka kumsajili na kumpa mechi, lakini kiukweli hana ‘Match fitness’ hata kidogo, watake wasitake, ndivyo ilivyo.

Haikatazwi kumsajili mchezaji ambaye hana ‘fitness’ kwasababu unajua umuhimu wake, lakini asiharakishwe kucheza. Ni bora wakacheza watu wengine ambao tayari wameshajiandaa kwa msimu.

Kwani Okwi kacheza Simba lini? Si kasajili juzi juzi tu dakika za mwisho? Alikuwa anafanya mazoezi wapi? Wamemsajili kutoka timu gani? Kafanya wapi maandalizi ya kabla ya msimu?

Labda viongozi watukumbushe. Okwi hana ‘fitness’ ,  Simba wanatakiwa kumtengenezea program maalumu ili kurudisha kiwango chake, lakini kama wanataka kuwafariji mashabiki wao basi waendelee kumtumia. Lakini haitakuwa na maana kama timu itaathirika kiufundi na kimbinu na wakati wanagundua watakuwa wameshachelewa.

Okwi alikuwa mchezaji wa kutegemewa katika timu ya taifa ya Uganda, lakini leo hii hayupo. Na tatizo ni kwamba hana ‘Match fitness’ na kilichochangia ni kutocheza mpira. Sasa Simba wanapata wapi ushujaa wa kumchezesha? Au kwasababu ni Okwi? Kwanini wasianze na wachezaji waliokuwa nao katika maandalizi ya kabla ya msimu na yeye akacheza na wenzake baadaye? Okwi hakuna kitu pale.

HARUNA CHANONGO (pichani kushoto)


Huyu ni mchezaji mzuri, lakini mambo yetu ya U-simba na U-yanga yamemharibu. Moja ya wachezaji ambao wangekuwa wamefika mbali mpaka sasa hivi ni Chanongo.

 Kutokana na tetesi za kuuza mechi, mfano ile ya Simba na Yanga ambayo alisimamishwa kwa madai kuwa amekula mlungula au rushwa, Chanongo ameathirika sana.

Ukiangalia uchezaji wake, Chanongo amepungua. Alikuwa anachukua mpira anazama ndani katika eneo la hatari, lakini leo hii kila sehemu akienda anaogopa, anadhani akikosea watu watasema ameuza mechi.

Kwahiyo anatafuta njia rahisi ya kujisafisha. Kila mpira anataka ageuke na kupiga pasi nyuma ili asipoteze, lakini Chonongo kama angecheza Chanongo yule yule wa Bank ABC, Chanongo yule wa msimu uliopita, angekuwa mchezaji mzuri, lakini kutokana na mambo ya U-simba na U-yanga. Wameshindwa kulea kipaji cha mchezaji. Chanongo ni muoga, anaogopa kuingia, anajihami kukosea.

Chanongo mdogo wangu ninayekujua mimi sio. Usiogope maneno ya watu, cheza mpira, mabeki wawili wafuate, ingia kwenye boksi. Leo hii mbona sikuoni ukiingia kwenye boksi, unageuka na kurudi nyuma, kulikoni?

AMISSI TAMBWE

Mchezaji wa mpira wa miguu  ili akamalike anahitaji mambo manne. Utimamu wa mwili, Ufundi, mbinu na Saikojolia.

Kama mchezaji ana vitu vitatu vya kwanza, lakini kisaikolojia hayuko vizuri, hivyo vingine ni kazi bure.

Kisaikolojia, Tambwe hayuko vizuri kwasababu yeye alikuwa Wayne Rooney wa Simba, lakini ghafla kafanywa kama wachezaji wale wale waliokuja kufanya majaribio na wamesajiliwa.

Zile taarifa  za kusema jina lake lilitakiwa kukatwa ili asajiliwe Okwi anazo. Binadamu yeyote yule hawezi kuwa sawa kisaikolojia. Sasa hivi kwenye timu anapoona yeye ni chaguo la tatu mbele ya Kiongera, na Okwi, halafu akikumbuka kuwa yeye ndiye mfungaji bora wa ligi msimu uliopita, kisaikolojia hawezi kuwa sawa.

Lakini  pamoja na hayo yote, nampongeza Tambwe kwasababu amebaki kuwa Tambwe yule yule na alifunga goli. Kama Simba wangetengeza nafasi kwa kumuamini yeye angewafungia magoli, lakini kwa staili hii ya kuonesha hawamuamini na kumfanya kama mchezaji wa ziada, basi wanampoteza na maisha yake yataishia hapo.

Tambwe bado ndiye mchezaji hodari wa Simba, lakini kwasababu ya kasumba ya viongozi kupenda wachezaji waliowasajili, matatizo hujitokeza.

Kwa mfano uongozi ulioingia madarakani, kuna wachezaji wapya wamewasajili na wanaamini wale waliowakuta sio wachezaji. Watake wasitake, Amissi Tambwe ndiye mshambuliaji wa Simba.

Kwasababu wachezaji wengine hawakucheza vizuri kama nilivyoeleza, ubora wa Tambwe haukuonekana. Lakini pale Okwi alipopiga pasi, iliona namna Tambwe alivyokaa katika nafasi na kufunga goli?, huyo ndiye Tambwe tunayemjua sisi.

Kuanzi sehemu ya nyuma, Simba timu yao haiko vizuri kabisa. Wakae chini wajipange, panapo majaaliwa, Mungu atawasaidia.

Jumatatu njema!

Chanzo: shaffihdauda.com


0 comments:

 
voyeur porn porn movies sex videos hd porno video