Geilson Santos Santana 'Jaja' (katikati) akishangilia bao lake na Mrisho Ngassa (kulia) na Saimon Msuva (kushoto)
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
0712461976
KAZI ya kwanza ya mshambuliaji uwanjani ni kufunga
magoli, ingawa anaweza kusaidia mambo mengine kama kurudi kusaidia timu pale
inaposhambuliwa, kutoa pasi kwa wenzake na mambo mengine ya kimpira.
Mchezaji anapopewa majukumu ya kuwa mshambuliaji
wa mwisho, hesabu zake lazima zijikite kutafuta nyavu na hapo ndipo atawafurahisha
makocha wake, wachezaji wenzake, viongozi wa timu na hatimaye mashabiki.
Kuna washambuliaji wa aina nyingi duniani na kamwe
hawawezi kufafana kwa aina ya uchezaji wao. Lionel Messi hafanani uchezaji wake
na Cristiano Ronaldo. Karim Benzema hafafani uchezaji wake na Diego Costa, lakini
wote wanaweza kufunga kadri wawezavyo.
Kufunga ni kufunga tu. Unaweza kupiga kichwa,
shuti au kufungia tumbo na likawa goli. Sio lazima kila mshambuliaji afunge kwa
‘staili’ ya Cristiano Ronaldo ya kupiga mashuti.
Baadhi ya mashabiki wa soka wamekariri vitu fulani,
kila muda wanataka kumuona kila mshambuliaji ana kasi, chenga na shabaha ya
kuona lango, kumbe sio lazima iwe hivyo.
Thomas Ulimwengu ana uwezo mkubwa wa kuwasumbua
mabeki kwa ‘manguvu’ yake na akafunga. Ni aina ya wachezaji wenye uwezo wa
kutumia nguvu na kupambana kwa mabavu, lakini hana vitu vingi kama kupiga
chenga au kimtaa zaidi ‘kupaka rangi mpira’.
Uchezaji wa Ulimwengu ni tofauti na Mbwana Samatta. Wote wanaweza kufunga, lakini
Samatta ana vitu vingi, anaweza kuchezea mpira, kukimbia nao kwa kasi, kupiga
chenga akitokea pembeni na hata katikati.
Leo hii huwezi kutaka Samatta acheze kama John
Bocco. Hawa ni watu wawili tofauti na ndio maana mmoja ni Samatta na mwingine
ni Bocco. Kiuchezaji wanatofautiana kabisa, lakini wote wanaweza kufunga.
Naweza jamani!: Jaja akishangilia moja ya bao lake
Mashabiki wa soka la Tanzania
wanabadilika-badilika sana. Leo wanaweza kukuzomea, kesho wakakushangilia kama mfalme.
Siku ya kwanza kwa Geilson Santos Santana
‘Jaja’ kuonekana uwanja wa Taifa ilikuwa
katika mechi ya kimataifa ya kirafiki kati ya Yanga na Thika United ya Kenya.
Jaja alifunga bao pekee katika ushindi wa 1-0,
lakini hakukubalika kwa mashabiki waliofika uwanjani hapo wakidai ni mzito
sana.
Pamoja na uzito wake, aliwafungia bao la ushindi.
Kabla ya bao hilo, Jaja alifunga bao katika mechi ya kirafiki dhidi ya
Chipukizi uwanja wa Gombani, Pemba.
Jaja alikejeliwa sana na pengine kutokujua
Kiswahili kumemsaidia na hata kama aliambiwa na mtu yeyote, bado asingeweza
kushangaa kwasababu mpira ni kazi yake na amezoea presha ya mashabiki.
Imani yangu ni kubwa kwa kocha Marcio Maximo.
Najua alimleta Jaja kwa kazi moja tu ya kufunga mabao.
Maximo ni mwalimu mwenye msimamo na afanyapo jambo
huwa anajua sababu. Alishawahi kusema Jaja ni mfungaji mzuri ‘Goal Machine’,
hivyo apewe muda.
Kocha huyu raia wa Brazil anajua fika kuwa Jaja
sio mtu wa vitu vingi, hajui kuchezea mpira, hana kasi kubwa, yaani anacheza
‘kivivu’, lakini amejaaliwa kitu cha msingi sana kama mshambuliaji.
Jaja (wa pili kulia, waliosimama wima) alifunga mabao mawili katika ushindi 3-0 dhidi ya Azam fc
Anajua kukaa kwenye nafasi na kuliona goli. Jana dhidi
ya Azam fc alianza ‘Mdogo mdogo’.
Kipindi kizima cha kwanza hakuonekana kabisa zaidi ya kuwaona akina Mrisho
Ngassa, Niyonzima, Nizar Khalfan wakicheza mpira.
Alionekana kuwakera mashabiki na wengine
walimzomea. Kipindi cha pili alitumia vyema nafasi alizopata. Aliitendea haki
pasi ya Saimon Msuva katika dakika ya 58 na kuifungia Yanga bao la kuongoza na
katika dakika ya 66 alifunga bao la pili akimalizia pasi aliyopenyezewa na Kiungo
Hassan Dilunga.
Jaja aliupata mpira, akatazama na kufikiria kwa
haraka nini cha kufanya. Akakokota mpira kwa hatua moja na kumchambua kiufundi
kipa Mwadini Ali, akinyanyua mpira na
kuuzamisha nyavuni.
Uwanja mzima ulilipuka kwa shangwe. Huwezi amini
wale wote waliokuwa wanazomea, walishangilia na kuimba jina la Jaja.
Baada ya mechi yule, Jaja aliyekuwa akionekana si
lolote, aliimbwa na kusifiwa sana.
Nilichojifunza ni kidogo tu, mashabiki wa soka
huwa wana kiu kubwa ya kuona mchezaji anafanya vizuri na akifanya vibaya wanazomea.
Sio Tanzania tu, hata duniani huwa mashabiki wakati fulani wanawachukia
washambuliaji wanaposhindwa kufanya vizuri.
Nilisema awali, kazi ya msingi ya mshambuliaji ni
kufunga. Kazi ya kwanza ya Jaja ni kufunga. Kumjadili kwa uchezaji wake, sio
jambo la msingi.
Kama anacheza kivivu, lakini anafunga, ndio jambo
la msingi kwasababu alisajiliwa aje kufunga magoli.
Kama kuna mtu anataka chenga, wapo akina
Niyonzima, wataalamu wa vionjo na hata Andrey Coutinho anajua kuuchezea mpira.
Kwa Jaja kazi yake ni kufunga.
Mashabiki wa Yanga, Jaja ni mfungaji mzuri kwa
mechi nilizomtazama, anajua kukaa maeneo sahihi na kufanya kile afikiriacho.
Wanayanga wakitaka kumuona Jaja akifanya kazi
nzuri, wamwache acheze mpira afikiriavyo. Wasimzomee, wamwache awe huru, acheze
mdogo mdogo kama afanyavyo, cha msingi ni kufunga.
Kikubwa, Wanayanga, wajifunze kuwaamini wachezaji
wao na kukaa pamoja nao pale wanaposhindwa kufanya vizuri. Ni muhimu kujua aina
ya staili ya uchezaji kwa wachezaji wote.
Usitake Niyonzima acheze kama Ngassa, hapana, kama
mchezaji ana aina ya mpira wake unaoleta matokeo, basi aachwe acheze vile
afikiriavyo.
Jaja ataendelea kuwafunga kwasababu ni mchezaji
anayejua nini anafanya anapofika langoni. Inawezekana asifunge mabao mengi
katika mechi za ligi kuu au akafunga, cha msingi ni kumuamini na kusubiri nini
atafanya.
0 comments:
Post a Comment