Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
KADI nyekundu ya Jacob Mwalobo aliwaathiri Prisons
kwa kiasi kikubwa, lakini kwa upande wa pili iliwaongezea nguvu zaidi na kuweza
kupambana na Yanga iliyokuwa katika morali ya hali ya juu.
Mwalobo alioneshwa kadi mbili za njano na kutolewa
nje kwa kadi nyekundu ‘umeme’ kufuatia kurudia kosa kwa kumfanyia madhambi ‘Anko’
Mrisho Khalfan Ngassa.
Wakiwa pungufu walishambuliwa sana, lakini walikuwa
imara kuanzia katikati. Walijaa eneo lao na kuwanyima uhuru akina Ngassa, Andrey
Coutinho, Jaja, Hassan Dilunga kufika golini kirahisi.
Kipindi cha pili, kocha mkuu wa klabu hiyo, David
Mwamwaja, aliwaelekeza wachezaji wake kuwa hawana cha kupoteza, waingie kucheza
mpira na kujituma hata kama wako pungufu.
Kweli walikuja juu mno, waligongeana pasi,
walipandisha timu juu na kuwapa shida mabeki wa Yanga walioongozwa na Nadir
Haroub ‘Cannavaro’ na Kelvin Yondani/Rajab Zahir.
Walipata goli safi la kusawazisha kupitia kwa
Ibrahim Kasaka Hassan kutokana na makosa ya mabeki wa Yanga.
Bao hilo liliwaamusha Prisons, lakini wakawa na nidhamu
ndogo ya kujilinda na kujikuta wakifungwa goli la pili dakika chache baadaye.
Ilitegemewa kuwa baada ya kusawazisha warudi nyuma
kwa muda, watulize akili na kulinda lango lao. Wakishakuwa sawa, waende mbele
zaidi kutafuta goli la pili.
Lakini wakisahau kuwa wako pungufu, waliendelea
kwenda mbele zaidi baada ya kufunga na kuamini kuwa wanaweza kupata la pili. Ni
kweli wangeweza, lakini walitakiwa kuongeza nidhamu ya ulinzi kwasababu
walikuwa pungufu.
Kwa kujiamini kwao waliona pointi moja sio ishu,
wangeweza kushinda uwanja wa Taifa na kuvuna tatu, ghafla wakafungwa kutokana
na kupoteza nidhamu ya ulinzi.
Baada ya mechi, nahodha wa Prisons, Lugano
Mwangama alizungumza machache, lakini kubwa aliisifia timu yake kwa kucheza
soka safi.
Mwangama alisema: “Tumekubali tumepoteza mchezo
dhidi ya Yanga, lakini ni sehemu ya matokeo ya mpira, tunajipanga kwa mechi
ijayo, tunakwenda kufanyia marekebisho makosa tuliyoyafanya”.
Akiizungumzia kadi nyekundu ya Jacob Mwalobo
katika dakika ya 38 ya kipindi cha kwanza, Mwangama alisisitiza: “Unajua katika
mpira tunategemeana na ndio maana ikawekwa idadi ya wachezaji 11 kwa 11, kwahiyo
mnapokuwa pungufu, lazima mtapata hitilafu, lakini naipongeza timu yangu,
imecheza vizuri, tumeweza kupambana tukiwa pungufu, tumecheza vizuri kiujumla,
lakini matokeo hayakuwa mazuri kwetu”.
Baada ya mechi mbili za ugenini, Prisons wanarudi
Sokoine Mbeya ambapo Oktoba 4 mwaka huu wataikaribisha Azam fc.
Azam fc watakwenda katika mechi hiyo wakiwa na
ushindi wa asilimia 100 katika mechi zao mbili.
Waliifunga 3-1 Polisi Morogoro katika mechi ya
ufunguzi na mechi ya pili jumamosi iliyopita waliibamiza 2-0 Ruvu Shootings ya
Pwani, mechi zote zilipigwa Azam Complex, Chamazi, Dar es salaam.
0 comments:
Post a Comment